Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii
MAMLAKA ya Hali ya Hewa nchini(TMA),mvua zinazotarajia kunyesha katika maeneo mengi yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka zinatarajia kuwa za wastani hadi juu ya wastani zinazoweza kusababisha athari mbali mbali yakiwemo magonjwa ya mlipuko.

Mkurugenzi wa TMA, Dkt. Agness Kijazi, ameyasema hayo wakati akitoa utabiri wa muelekeo wa mvua za msimu Novemba hadi Aprili 2019/2020 na kusema kuwa mvua nyingi inatarajia kunyesha katika nusu ya kwanza ya msimu kutokana na uwezekano wa uwepo wa upepo kuvuma kutoka upande wa magharibi.

Amesema upepo huo unatarajia kubeba unyevunyevu Kutoka misitu ya Kongo kuelekea katika maeneo ya nchi yetu huku kwa upande wa kipindi cha nusu ya pili cha msimu mvua zinatarajiwa kupungua katika baadhi ya maeneo kutokana na joto la bahari sehemu ya kati ya bahari ya Hindi kuendelea kuongezeka ikilinganishwa na maeneo mengine ya bahari ya Hindi.

"Mvua za msimu ni mahsusi katika maeneo ya magharibu mwa nchi ,kanda ya kati ,nyanda za juu kusini magharibi,kusini mwa nchi,ukanda wa pwani ya kusini pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro ambapo maeneo haya yanapata msimu mmoja wa mvua ambazo zinaanza mwezi Novemba hadi Aprili ya mwaka unaofuata," amesema Dk.Kijazi

Amesema, katika mkoa wa Tabora mvua inatarajia kunyesha juu ya wastani hadi wastani  huku mkoa wa Kigoma na Katavi ikitarajiwa kunyesha mvua za wastani hadi juu ya wastani  na kutarajia kuanza wiki ya nne ya mwezi Oktoba 2019katika mkoa wa kigoma na kusambaa Kwa mikoa ya Katavi na Tabora katika wiki ya kwanza ya mwezi Novemba.

"Mvua katika maeneo ya Singida na Dodoma zinatarajia kuanza katika wiki ya Kwanza hadi wiki ya pili ya mwezi Novemba 2019na maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani hadi wastani," alisema na kuongeza

"Katika mikoa ya Rukwa,Songwe,Mbeya,Iringa,Njombe,Ruvuma pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro mvua zinatarajia kuanza kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba 2019 na kutarajia kuwa za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi," alisema

Aidha alisema katika mikoa ya Lindi na Mtwara mvua zinatarajia kunyesha kati ya wiki ya kwanza na wiki ya pili ya mwezi Novemba 2019 na zinatarajia kuwa za juu ya wastani hadi wastani.

Dkt.Kijazi amesema, matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa yanaweza kujitokeza hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani.

Alisema migandamizo midogo ya hewa pamoja na vimbunga katika eneo la kusini magharibi mwa bahari ya Hindi inatarajiwa kuvuta upepo wenye unyevunyevu kutoka misitu ya Kongo na hivyo kusababisha mvua katika maeneo mengi hapa nchini.

Aidha Dk. Kijazi amesema mvua hizo zinaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko, yanayohusiana na Maji hivyo ni vema tahadhari ikachukuliwa mapema kwa kumwaga madawa ya kinga na hatua zingine stahiki ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

Pia mamlaka za maji na jiji zimeshauriwa kuchukua tahadhari hasa katika kuhakikisha miundombinu inabaki salama ili kuepusha kutuwama kwa maji na kusababisha mafuriko uharibifu wa miundombinu na upotevu wa maisha na mali.

TMA pia wamewashauri menejimenti ya afya kutoa taarifa Mapema kwa wakazi wa maeneo ya mabondeni na miundombinu iwapo kutatokea uharibifu wowote ili kupunguza athari na hasara zinazoweza kutokea.

Aidha Dk. Kijazi ametoa ushauri Kwa watumiaji wote wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima,wafugaji,mamlaka za wanyamapori,sekta za maji na afya kuendelea kufuatilia na kutumia ushauri wa kitaalam katika shughuli zao za kila siku.
 Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA Dkt. Agnes Kijazi akizungumza wakati alipotangaza utabiri wa hali ya hewa kuhusu uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka katika makao mkuu ya mamlaka hiyo jengo la Ubungo Plaza jijini Dar es salaam leo
  Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA Dk. Agnes Kijazi akizungumza na waandishi wa habari alipokuwa akitangaza utabiri wa hali ya hewa kuhusu uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka katika makao mkuu ya mamlaka hiyo jengo la Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni , Bw. Samwel Mbuya Meneja Kituo Kikuu cha Utabiri TMA na kushoto ni Hamza Kabelwa MKurugenzi wa Huduma za Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...