*Familia yake ikamkalia kooni
*Sasa achomoka na 'Mapenzi Kazi'
HAKUNA
jambo lolote linaloanza kwa utelezi hapa duniani. Kila kazi ina
changamoto na msoto wake. Na katika kupitia changamoto hizo, baadhi yao
wanafikia kukata tamaa kabisa, licha ya kuwa na kila kitu kinachoweza
kuwapatia mwangaza katika mambo wanayopigania.
Hata
katika sanaa ya muziki wa kizazi kipya tunachoshuhudia vijana wengi
wakichanua na kujimudu kiuchumi, pia una suluba na changamoto lukuki,
msoto mzito unaowakumba wasanii wengi tangu siku walipoamua kujiingiza
kwenye tasnia hiyo.
Katika
kuangalia vijana hao wanaopitia katika msoto mzito ni Maneno Mohamed
'Man Mo'. Kijana huyu mwenye uwezo wa juu wa kuimba na kutunga nyimbo za
muziki wa kizazi kipya, anapitia katika tanuri la moto, barabara yenye
miba mikali kiasi cha kuwahi kukata tamaa ya kuendelea na sanaa yake.
Ndio,
hii ni kwa sababu msanii huyo licha ya kuwa kwenye sanaa kwa muda mrefu
sasa, lakini mlango wa mafanikio ulionekana kuchelewa kufunguka, licha
ya kuwa na kipaji cha uimbaji na utunzi wa nyimbo kali, ukiwamo wimbo wa
'Nasimama' ulioimbwa na msanii nyota Judith Wambura 'Lady JayDee',
ambao uliandikwa na Man Mo.
Katika
mazungumzo na Gazeti hili, Man Mo anasema kwamba alianza kujihusisha na
muziki tangu alipokuwa mdogo, akimfuatilia mama yake Bi Salama Mussa
Kaduga, aliyekuwa anajihusisha na sanaa katika Matukio mbalimbali haswa
ya kisiasa, huko kijijini kwao Kimange, mkoani Pwani.
"Muda
mwingi nilikuwa namfuatilia mama yangu katika sanaa yake, jambo ambalo
lilichochea kwa kiasi kikubwa mimi kupalilia kipaji changu cha kimuziki
na kuweka nia kubwa ya kuja kuwa msanii nyota duniani kama wengine.
"Pamoja
na mambo mengine, msanii mwingine ambaye kwa namna moja ama nyingine
aliendelea kukuza kipaji changu ni Ali Kiba, ambaye muziki wake
niliuelewa, haswa nilipofanikiwa kukutana naye katika studio za
Sharobaro Records za jijini Dar es Salaam zilizokuja kuvuma kwa kutoa
wasanii wengi mahiri, akiwamo Bob Junior, Diamond Platnumz, Shetta, Rich
Mavoco na wengineo kibao ambao mara kwa mara walikuwa wakikutana kwenye
studio hizo,"Alisema Man Mo.
Msanii
huyo mwenye kiu kubwa kisanaa anasema rasmi kuingia kwenye sanaa
ilikuwa ni mwaka 2010 ambapo kama vijana wengine, aliamua kuondoka
kijijini kwao na kuvamia jiji la Dar es Salaam, akiwa na matarajio
makubwa ya kuvuna kwa kupitia muziki wa kizazi kipya.
Kwa
bahati mbaya jiji lilimlaki vibaya na kumchoma na jua tangu alipofika
na kuamua kukimbilia kwenye kiwanda Cha nguo Cha Urafiki ili apunguze
makali ya kimaisha kwa kufanya kibarua katika kitengo cha kuchambua
nyuzi.
Mkali huyo wa kizazi kipya anasema licha ya kufanya kibarua
Urafiki, lakini hamu ya kimuziki ilikuwa kubwa na kujikuta akienda
Sharobaro kurekodi wimbo wake kwa pesa yake, hata hivyo baadae uongozi
wa Studio hizo ulimpa ahueni kwa kumtaka awe chini ya Sharobaro Records
ili akue kimuziki.
Hata hivyo anakiri uamuzi huo pia ulichangiwa kwa
kiasi kikubwa na bidii yake pamoja na kujituma kwa kila aina ikiwamo
kufanya usafi kwenye studio hizo, akitafuta upenyo wa kuchomoka kisanaa.
"Nikiwa
Sharobaro Records nilifanikiwa kurekodi nyimbo nyingi na kupata
marafiki wengi ambao naweza kusema nilikua kwa kiasi kikubwa mno
kulinganisha na wakati ule natokea kwetu kijijini nikiwa sina mtandao
wowote kisanaa na hata kula yangu ikawa ni mashaka matupu.
"Nyimbo
ambazo nilitengeneza wakati ule ni Binti wa Kibara, Binti wa Kimasai na
nyingine nyingi ambazo hazikuachiwa hewani bila kusahau zile
nilizoandikia wasanii wengine ukiwamo ule wa dada yangu Lady JayDee
uliojulikana kama Nasimama ambao ulifanya vizuri mno katika ulingo wa
Bongo Fleva,"Alisema.
Wakati
anaamini anaelekea pazuri, ghafla mambo yalibadilika na kurudi tena
kwenye msoto ambapo kila alilopanga lilishindwa kutimia, ikiwamo
kuwapata mameneja ambao bila wao ni ngumu msanii kutokea peupe. Anasema
wakati anaelekea kuchoka, akapata meneja aliyempa sharti la kuimba
muziki wa injili na sio muziki wa kidunia.
"Huyu
ndugu yangu alikuwa anaitwa James Albert Katagira anayemiliki shule za
Tusiime, ambaye alinionea huruma na msoto wangu na kunishawishi nihamie
kwenye injili ili anisimamie jambo ambalo nililitekeleza haraka, kwa
sababu lengo langu lilikuwa ni sanaa.
"Nilifanikiwa
kurekodi nyimbo mbili na video zake ambazo ni Jicho Langu na Nimuimbie,
ambazo zilifanya vizuri katika muziki wa injili na kuanza kupata shoo
nyingi katika mikoa mbalimbali kwa kuunganishwa na wasanii wengi wa
muziki huo bila kusahau kushiriki makongamano mengi ya kidini,"Alisema.
Man
Mo anasema muziki huo ulikuwa unampa mwelekeo mzuri, licha ya kufikia
kutengwa na familia yake kwa madai alitokea katika chimbuko la waumini
wa dini ya Kiislamu, hivyo jamii ilishindwa kumuelewa, wakiwamo marafiki
zake waliomkosoa kwa kitendo chake cha kuacha Bongo Fleva na kukimbilia
injili.
Ili jamii
imuelewe akiwamo mama yake mzazi, alitumia muda mwingi kuzungumza nao,
huku akikiri kuwa aliingia kanisani na kuimba injili kama njia ya
kumfikisha kileleni na sio nia ya kubadili dini, ingawa anasema katika
kipindi chote hicho, jamii ya kikristo na wasanii hao wameishi kwa
upendo na kushirikiana kwa kiasi kikubwa, akiwamo Madame Frola ambaye
alishiriki naye katika matamasha kadhaa likiwamo la Tanga Mjini akiwa
kama mwimbaji wa injili.
Man
Mo anasema msoto haukumuacha, kwani msaada wake uligota, hivyo kuamua
kuachana kabisa na muziki, akiingia katika biashara ya kilimo pamoja na
kuuza kuku, biashara ambazo zilitokana na umri kuendelea kumtupa mkono
huku akishindwa kutokea peupe.
Kijana
huyo mwenye ndoto na maneno mengi mdomoni mwake anasema baada ya kukaa
kwa miezi kadhaa bila kujihusisha na lolote linalohusu muziki,
alishtushwa na simu kutoka kwa Belo Master, aliyekuwa anafanya wimbo
kwenye Studio za classic Sound chini ya mtayarishaji wake Monagenster za
Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
"Wakati
ananipigia simu, sikuwa na ari, lakini kwakuwa jamaa anajua uwezo wangu
na alitaka nikamuimbie kiitikio, hivyo nikaenda Studio kurekodi kama
alivyotaka, jambo ambalo lilianza upya kunitekenya rohoni mwangu.
"Kwakuwa
niliimba vizuri kwenye wimbo ule, viongozi wa Monagenster walivutiwa na
mimi na kunivuta karibu ili waendelee kuangalia uwezo wangu ambapo
walinikubali zaidi haswa kwa uwezo wangu wa kuandika nyimbo kali,
ukizingatia wengi nilikuwa nawatungia, hivyo kupata upenyo
rasmi,"Alisema.
Kijana
huyo anasema kwa Sasa anasimamiwa kazi zake chini ya Kampuni ya African
Network Entertainment (ANE) kwa kushirikiana na Monagenster kwa kupitia
classic Sound ambapo hadi sasa nimeachia nyimbo mbili kali pamoja na
video matata ambazo ni 'Tike na Mapenzi Kazi zinazofanya vizuri katika
ulimwengu wa muziki.
Msanii
huyo anayetokea kwenye familia ya watoto wanne, huku yeye akiwa wa
kwanza kuzaliwa mwaka 1994 huko Kimange, anawataja wadogo zake kuwa ni
Mwahija, Sauda na Muhsin huku kiwango chake cha elimu kikiwa ni kidato
cha nne, akiishia kiwango hicho kutokana na kuhangaikia muziki licha ya
baba yake kutamani mtoto wake asome sana, aliishia njiani.
Man
Mo alisoma elimu ya msingi katika shule mbili za Kimange na Bagamoyo,
wakati elimu ya Sekondari aliipata katika shule ya Air wing ya Banana,
jijini Dar es Salaam, huku akisema kuwa maisha ya muziki kabla ya kutoka
ni magumu yanayoweza kukatisha tamaa wasanii wengi wenye vipaji.
"Kwa
sasa sina ninachokifanya zaidi ya kusikiliza ushauri wa viongozi wangu
wa ANE, nikiamini kuwa uwezekano wa kupasua anga ni mkubwa kutokana na
Kampuni kuwa na watu wanaojua muziki na ndoto za sisi vijana kufika
mbali.
"Lengo langu ni
kufanya muziki mzuri wa kibiashara, nikitumia uzoefu wangu na kipaji
changu cha kuimba na kuandika nyimbo kali ili nipate mafanikio ya
kutimiza ndoto zangu, ukizingatia kuwa nimesota sana, nimekula ngarambe
nyingi, hivyo hakuna kinachoweza kuniweka chini tena,"Alisema Man Mo.
Man
Mo anasema kuwa licha ya muziki kuwa na ushindani mkubwa, lakini
ukiweka bidii unafanikiwa, huku akisema kuwa anataka kuwa msanii
'simple' kama Ali Kiba lakini afanye muziki mzuri wa biashara kama
Diamond Platnumz jambo linalompa utajiri mkubwa.
Msanii
huyo anaendelea kusema kwa kuwataka wasanii kufanya juhudi kubwa
kuutangaza muziki wao pamoja na chipukizi kukaza msuri ili nao wafikie
malengo licha ya kwamba wasanii wachanga wengi huishia njiani kwa
kushindwa kwenda na kasi ya msoto katika sanaa.
Man
Mo anakumbuka jinsi alivyoshindwa kuwa na maelewano mazuri na baba yake
kiasi cha kununiana, kisa kuwa kwenye muziki huku maisha yakiwa magumu
kwa mtoto wao, ambapo juhudi za mama yake zilikuwa zinamlainisha mzee
wake japo kwa uchache.
Mwimbaji
huyo mwenye ndoto kubwa anasema muziki umezidi kupiga hatua kutokana na
juhudi za wasanii wenyewe wanaokwenda na mabadiliko, ikiwamo mbinu ya
kutumia vizuri mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, YouTube nk,
ambapo kama ilivyokuwa kwa wasanii wengine, Man Mo pia anamiliki
akaunti mbalimbali zinaoenda kwa jina la manmoofficial katika mitandao
mbalimbali kwa ajili ya kutangaza muziki wake pamoja na kupata ulingo wa
kujadiliana na mashabiki wake.
Anasema
hali hiyo umeufanya muziki kuwa biashara nzuri licha ya msoto kabla ya
kutoka kuwa pale pale, jambo linaloongeza hamasa ya kufanya vizuri kwa
wasanii wote nchini Tanzania, ambapo nyimbo zake zinapatikana kwenye
YouTube kwa akaunti ya Kampuni ya Africa Network Entertainment pamoja na
kupatikana pia Audiomack, Boomplay, Spotify na kwingineko.
Kuhusu
serikali, Man Mo anaitaka iendelee kushirikiana na wasanii wote sanjari
na kuwatafutia upenyo katika muziki wa Dunia, bila kusahau kufanikisha
wasanii wa ndani kutoka nje mara kwa mara ili wakaongeze wigo mkubwa
katika sanaa yao, akisisitiza kuwa bila wasanii wa ndani kupata
maonyesho ya Kimataifa muziki wao hautapiga hatua.
Huyo ndiye Man Mo, mmoja ya wasanii waliopokewa na msoto na mwenye ndoto lukuki za kisanaa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...