Mwenyekiti wa Taasisi ya Agri Thamani Foundation Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda akizungumza kwenye hafla ya viongozi wa dini kusaini makubaliano ya mapambano ya ugonjwa wa Kifua Kikuu kupitia majukwaa ya nyumba za ibada jana jijini Mwanza.
…………….



NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA

MWENYEKITI wa Taasisi ya AGRI THAMANI Foundation, Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda, amesema mauaji ya watu wenye ualbino na sakata la kuchinja Kanda ya Ziwa lilimfanya auone Uwaziri Mkuu mchungu.

Pinda alisema jana jijini Mwanza wakati akizungumza kabla alisema viongozi wa dini kabla ya kusaini makubaliano ya kutumia nyumba za ibada kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa wa Kifua Kifuu (TB).

Alidai anafarijika na kupata matumaini mkutano huo kufanyika Mwanza kwa sababu wakati akiwa Waziri Mkuu yaliibuka mauaji ya watu wenye ualbino lakini pia ubishani wa nani achinje kati ya Wakristo na Waislamu mambo ambayo yalimfanya Uwaziri Mkuu auone mchungu lakini yaliisha salama baada ya kushirikiana na viongozi wa dini na kukafanikiwa na leo hayapo.

Alisema viongozi wa dini wana nguvu mbili, moja ni ukaribu wao na Mungu, wanapowaombea watu kiroho wanapona, ya pili wamebeba kundi kubwa la jamii, wanasikilizwa na wakisema jambo linakwenda sawia hivyo ushiriki wao kwenye vita ya kupambana na TB utakuwa na tija na makubaliano hayo kusainiwa Kanda ya Ziwa, unaweza kuwa uwanja mzuri wa vita ya TB kutokana na kanda hiyo kuwa na watu milioni 12 ambapo asilimia 20 ikiwekwa pamoja inawezekana kupata matokeo chanya..

Alisema ugonjwa huo unasumbua taifa kwa sababu ya maadui waliotajwa na Mwalimu Nyerere ( umaskini, ujinga na maradhi) hivyo umaskini na ujinga ukiondolewa TB itatokomezwa na kushauri kila halmashauri kujenga uwezo wa watendaji na mifuko ya lishe itumike ipasavyo na kutafuta mbinu ya kuzungumza lugha moja.

Utiaji saini huo ulishuhudiwa na Spika wa Bunge Job Ndugai ambaye alikuwa mgeni rasmi, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda,Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Jenister Mhagama, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Serikali za Mitaa na Tawala za mikoa Joseph Kandege na mwenyekiti wa Kamati ya wabunge hao, Oscar Mukasa.

Miongoni mwa viongozi wa dini waliosaini makubaliano ya mapambano ya TB yalioasisiwa na Mtandao wa Wabunge walio kwenye mapambano ya kudhibiti ugonjwa huo wa Kifua Kikuu nchini ili kutumia nyumba za ibada kufikisha ujumbe na elimu kwa jamii ni kutoka Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (TEC), Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste (CCT), Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA).

Aidha, Askofu Renatus Nkwande (TEC), Askofu Mark Malakana (SDA), Sheikh Hassan Chizenga (BAKWATA) na Askofu Cheyo,walisema kwa nyakati tofauti kuwa jukumu hilo wamelibeba kwa maslahi ya watanzania kuhakikisha hawaathiriwi na vimelea vya TB.

“Kujadili na kuunganisha nguvu na viongozi wa dini kupamban na TB ni wazi watafikisha ujumbe kwa waumini sababu kanisa tiba kwao ni wajibu .Kutuhusisha kuelemisha jamii ni wazi jambo hili litakwisha,”alisema Askofu Nkwande.
“Jambo hili tumelipokea kwa mikono miwili, kwangu na wachungaji wa SDA suala la mafundisho ya afya ni sawa na kumsukuma mlevi.Magonjwa yanaletwa kwa kukiuka misingi iliyowekwa na Mungu.Tunataka Tanzania bila TB inawezekana, hivyo vita hiyo ni wajibu wa kila mmoja kuibeba ili tulifute;tutalifikishaje, ni kutoa elimu kwani watu kufa si heshima, waliumbwa wafurahie maisha yao,”alisema Askofu Malekana.

Mwenyekiti wa mtandao wa wabunge hao Oscar Mukasa kabla ya hafla hiyo alisema majukwaa ya nyumba za ibada yanalenga kuifikia jamii elimu itakayosaidia kuongeza ufahamu wa TB, namna ya kujikinga na kupata tiba lakini pia maelekezo ya serikali yatafika kwa usahihi , eliemu ambayo itawafikia watanzania wengi na itakuwa endelevu

Kwa mujibu wa takwimu watu milioni 18 nchini wanavimelea vya TB ambapo watu 100,000 kati ya 142,000 wana tatizo hilo, pia mwaka 2018 watu 75000 waligundulika kuwa na TB, asilimia 67 hawakuwa kwenye tiba, 39,000 walipoteza maisha na watu 60 hufariki kila siku mtu mmoja anaweza kuambukiza watu 10 hadi 20 kwa mwaka.

Aidha, watu milioni 1.5 walipoteza maisha mwaka 2018 ambapo watu milioni 7 walikuwa kwenye tiba huku milioni 3 wakiwa hawajulikani walipo ama walikufa jambo linaloonyesha TB bado ni tishio ikizingatiwa theluthi moja ya watu duniani wameambukizwa vimelema vya ugonjwa huo.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema jumuiko na dhamira ya viongozi wa dini kwenye mapambano ya TB litaongeza chachu, kuja na ubinifu na jamii kuacha mazoea ambapo serikali kupitia wizara hiyo itaendelea kuchukua hatua ya kupambana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja kutoa dawa bure, vifaa tiba na vitendanishi.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi, Vijana na Ajira, Jenister Mhagama, alisema tatizo la TB ni pacha na Ukimwi pamoja na dawa za kulevya nchini hivyo nguvu inayotumika kuhakikisha maambukizi mapya hayatokei ipelekwe kwenye vita hiyo.

Alisema nguvu kazi ya taifa ni vijana ambao ni asilimia 56 ndio waathirika wakubwa na bila kujipanga vizuri tutajikuta tunaingia kwenye uchumi wa viwanda tukiwa na tatizo na kupoteza malengo tunayoweka lakini serikali itaendelea kutoa mchango mkubwa ili kupambana na maradhi hatarishi.

Mgeni rasmi Ndugai alisema aliamua mkutano huo ufanyike Mwanza ili kufikisha elimu vizuri na kuwaeleza wananchi wa Kanda ya Ziwa kuna tatizo kubwa la TB na kuonya waachane na imani potofu za kuamini kila ugonjwa na kifo una mkono wa mtu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...