Kama tunavyofahamu kuwa siku ya Jumapili Novemba 24, 2019 Watanzania kote nchini watafanya uchaguzi wa viongozi ngazi ya Serikali za Mitaa. Hatua hiyo ya uchaguzi imetanguliwa na uandikishaji wapiga kura, uteuzi wa wagombea na kampeni za wagombea, hatua ambazo zimetekelezwa kwa mafanikio makubwa. 

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeridhishwa na idadi ya watu waliojitokeza kujiandikisha kupiga kura. Idadi hiyo imeongezeka ukilinganisha na idadi ya watu waliojiandikisha katika uchaguzi kama huo uliofanyika mwaka 2014. 

Katika kipindi kama hiki cha uchaguzi zipo taasisi za ndani na nje ya nchi ambazo zimeteuliwa kama waangalizi wa uchaguzi kwa mujibu wa Sheria ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura 287 na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288. 

Napenda kuujulisha umma wa Watanzania kuwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ni mojawapo ya taasisi ambayo itafanya ufuatiliaji wa uzingatiwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi huo kama Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Na. 7 ya 2001 inavyoelekeza. 

Tume inashiriki katika ufuatiliaji wa uchaguzi huu kama ilivyokuwa kwa chaguzi nyingine zilizopita ili kuhakikisha kuwa uchaguzi utakaofanyika unakuwa huru na wa haki. 

Hivyo basi, ili azma hiyo iweze kufikiwa ni muhimu kwa mamlaka na vyombo vinavyohusika katika zoezi hili kuhakikisha kuwa vinasimamia Sheria, Kanuni na Miongozo iliyowekwa na kutenda haki. 

Aidha, wapiga kura na wagombea kwa upande wao, wahakikishe kuwa wanatumia haki yao na kutelekeleza wajibu wao wa kikatiba wa kupiga kura na kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo iliyotolewa na mamlaka mbalimbali za nchi ili uchaguzi uweze kuwa huru na wa haki. 

Tume inatoa rai kwa wananchi wote nchini kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zote za upigaji kura na kuhakikisha kuwa zoezi la upigaji na uhesabu kura linafanyika kwa utulivu na amani. 

Mwisho, Tume inatoa wito kwa Wananchi wote waliojiandikisha kujitokeza kwa wingi siku ya Jumapili Novemba 24, 2019 na kutumia haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi watakaotuongoza kwa muhula mwingine wa miaka mitano. 

Tume inawatakia Watanzania wote uchaguzi huru na wa haki! 

Imetolewa na: 
Mhe. (Jaji Mstaafu) Mathew Pauwa Mhina Mwaimu 
Mwenyekiti 
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA 

Novemba 20, 2019 


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...