*Spika Ndugai azishauri ofisi za Balozi kutoa ushirikiano wa kutosha

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

SERIKALI ya China kupitia Ubalozi wake hapa nchini umeingia makubaliano na asasi saba za kiraia; huku mlengo mkubwa wa makubaliano hayo ukiwa ni kushirikiana na wanajamii ikiwa ni pamoja na kubadilisha uzoefu na teknolojia ili kuweza kujenga uchumi imara kwa wanajamii pamoja na kupunguza umaskini.

Akizungumza katika hafla hiyo mgeni wa heshima na Spika ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Yustino Ndugai amesema kuwa, viongozi wa asasi hizo zisizo za Kiserikali kutoka Tanzania na China watashirikiana katika kuleta maendeleo kupitia nyanja mbalimbali ikiwemo kubadilishana uzoefu na teknolojia sambamba na kuwashirikisha wananchi katika fursa mbalimbali za kiuchumi.

Spika Ndugai amesema kuwa mpango huo ni wa muda mrefu ambao Rais wa nchi hiyo Xi Jinping aliuanza mwaka 2003, Rais Jinping alianzisha ushirikiano huo ili kuleta maendeleo ya pamoja na hiyo ikiwa sambamba na uimarishaji wa miundombinu, biashara ya pamoja na mahusiano bora ya wanajamii.

Amesema kuwa Tanzania na China wamekuwa ndugu Sasa kutokana na kuwa na urafiki na ushirikiano uliobora zaidi;

"Tanzania ina marafiki wengi, ila urafiki wetu na China umekuwa urafiki wa pekee, uliodumu kwa muda mrefu na tumekuwa tukishirikiana kwa mambo mengi yenye tija katika mataifa yetu" ameeleza Ndugai.

Ndugai amezishauri ofisi za Balozi za mataifa hayo mawili kutoa ushirikiano wa kutosha ili malengo ya yaliyowekwa ikiwemo kupunguza umaskini, kubadilishana uzoefu hasa teknolojia na kutoa fursa kwa wananchi kushiriki katika shughuli za kiuchumi kupitia asasi za kiraia yalete mafanikio makubwa.

Kwa upande wake Naibu Spika wa Bunge la Jumuiya wa watu wa China na kiongozi mkubwa wa Chama cha Communist nchini humo Ji Bingxuan amesema kuwa mahusiano hayo ambayo yana zaidi ya miaka 50 sasa yalijengwa na waasisi wa mataifa hayo na matunda ya misingi hiyo yanashuhudiwa sasa.

Spika Bingxuan amesema kuwa uhusiano wa Tanzania na China ni wa kipekee huku akitolea mfano kwa Waziri Mkuu Mstaafu Dkt. Salim Ahmed Salim kuwa kiongozi wa kwanza kutoka bara la Afrika kutunukiwa tuzo heshima ya kuwa na kuimarisha mahusiano baina ya mataifa hayo nchini.

Vilevile Balozi wa China nchini Wang Ke amesema kuwa fursa hizo zitawanufaisha wanajamii wa nchi hizo kupitia asasi hizo za kiraia na kuleta maendeleo ya pamoja.

Wang Ke amesema kuwa mwaka 2013 Rais Xi Jinping aliichagua Tanzania kuwa nchi ya kwanza kuitembelea mara tu alipochaguliwa na kadri miaka inavyokwenda wameshuhudia namna mahusiano hayo yanavyozidi kuwa imara na tija kwa wananchi wa mataifa hayo.

Mbali na taasisi zinazohusika na masuala ya wanawake na afya  moja ya asasi iliyoingia makubaliano hayo ya kuleta maendeleo ya pamoja kwa wanajamii wa China na Tanzania ni Taasisi ya Maafa, Majanga na Uokoaji (SUKOS) iliyochini ya Mstaafu, Kamanda wa Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam Suleiman Kova.
 Balozi wa China nchini Tanzania Wang Ke (kushoto) akimuongoza njia Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Yusto Ndugai (katikati) Mara baada ya kuzindua rasmi ushirikiano wa maendeleo ya pamoja kupitia asasi za kiraia, leo jijini Dar es Salaam.
 Mstaafu Kamanda wa Kanda maalumu ya Dar es Salaam Suleiman Kova (aliyeketi kushoto) akisaini makubaliano ya ushirikiano wa kimaendeleo kupitia asasi za kiraia za nchini za Tanzania na China, leo jijini Dar es Salaam.

Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Yustino Ndugai akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Spika wa Jumuiya ya watu wa China Ji Bingxuan, Balozi wa China nchini Wang Ke, Balozi wa Tanzania nchini China Mbelwa Kairuki pamoja na viongozi wa asasi za kiraia kutoka nchini China na Tanzania baada ya kuzindua rasmi ushirikiano wa kuleta maendeleo ya pamoja baina ya mataifa hayo kupitia asasi za kiraia, leo jijini Dar es Salaam.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Yusto Ndugai (kushoto) akibadilishana mawazo na Naibu Spika wa Bunge la Jumuiya wa watu wa China Ji Bingxuan (katikati) kulia ni Balozi wa China nchini Wang Ke.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...