Charles James, Michuzi TV

Ndalichako amesema ni katika kuangalia hili Serikali ilikuja na Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) na kuomba ufadhili wa Benki ya Dunia. Ndalichako amesema kuwa anaamini Benki ya Dunia itaridhia na kupitisha mradi huo muhimu kwa taifa kwa sababu unakwenda kutatua mahitaji ya haraka ya kielimu ya watoto wa Kitanzania na kutimiza Malengo Endelevu ya maendeleo.

SERIKALI imesema inaamini Benki ya Dunia itaridhia na kupitisha ombi lao la ufadhili wa mradi wa kuimarisha elimu ya Sekondari (SEQUIP) kwa sababu inakwenda kutatua mahitaji ya haraka ya kielimu ya watoto wa kitanzania kutimiza ndoto zao.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako wakati alipokua akizungumza na wanafunzi, walimu na watumishi wa Shule ya Sekondari ya Msalato leo jijini Dodoma alipofanya ziara ya kukagua miundombinu ya shule hiyo kongwe nchini.

Waziri Ndalichako amesema mradi huo wa SEQUIP unalenga kuongeza idadi ya shule za sekondari ambazo zitajengwa katika maeneo ya karibu na jamii ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira salama na rafiki.

" Lengo la serikali ni kukuza kiwango cha elimu nchini, kuhakikisha vijana wetu wanasoma katika mazingira salama. Kupitia mpango huo tutaongeza shule za bweni hasa za wasichana pamoja na upanuzi wa shule kongwe zipatazo 50.

Tunaamini kupitia mradi huu vijana wetu wa kike na kiume wapatao Milioni sita watanufaika nao kwa kipindi cha miaka mitano ijayo," Amesema Prof Ndalichako.

Amesema kuwa matokeo chanya ya sera ya elimu bila malipo ni kuongezeka kwa wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na kutakiwa kujiunga na kidato cha kwanza, ambapo takwimu zinaonesha kuna ongezeko la wanafunzi kutoka 366,296 mwaka 2016, kufikia 680,000 mwaka 2020, na inatarajiwa Mwaka 2023 watakuwa 1,400,00 na hivyo kuhitajika kuongeza  miundombinu ya shule za sekondari kwa zaidi ya asilimia 100.

“Nawapongeza kwa kuwa shule ya wasichana yenye matokeo mazuri kwa kipindi kirefu, niwaombe ongezeni bidii ili matokeo ya elimu bila malipo yaweze kuonekana kwani rais anapambana kuhakikisha elimu inakuwa bora ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti ya Elimu sekondari kwa asilimia 70 mwaka uliopita” Amesema Prof Ndalichako.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Gerald Mweli amesema wizara yake itaendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu kuhakikisha inakamilisha ukarabati wa shule kongwe kwa kukarabati maeneo ambayo hayakufikiwa katika awamu ya kwanza huku akipongeza juhudi za walimu wa shule hiyo kwa kuondoa daraja sifuri.

Nae Mkuu wa shule hiyo, Neema Maro ameishukuru serikali kwa namna inavyokarabati shule kongwe ikiwa pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya ufundishaji na ujifunzaji, huku akiomba kutatuliwa changamoto ya uzio, uchakavu wa baadhi ya miundombinu ambayo bado haijakarabatiwa shuleni hapo.

Katika ziara hiyo Waziri Ndalichako alikagua miundombinu ya shule hiyo kongwe hasa mabweni na madarasa na kuahidi kuipa nafasi ya upendeleo shule hiyo katika awamu ijayo ya shule kongwe zitakazofanyiwa maboresho baada ya kuvutiwa na kiwango cha ufaulu kwenye shule zao hasa katika kutokomeza daraja sifuri na la nne.
 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akikagua miundombinu ya maji katika shule ya Sekondari Msalato alipofanya ziara leo shuleni hapo.
 Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Msalato wakimshangilia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako wakati alipofanya ziara ya kukagua miundombinu ya Shule hiyo na kuzungumza nao.
 Mkuu wa Shule ya Sekondari Wasichana Msalato, Neema Maro akisoma taarifa ya Shule hiyo kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako (kulia).
 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako akikagua mojawapo ya bweni la shule ya Sekondari ya wasichana Msalato wakati alipofanya ziara ya kukagua miundombinu leo.

 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako akizungumza na Wanafunzi, Walimu na Watumishi wa Shule kongwe ya Sekondari ya Wasichana Msalato jijini Dodoma leo.
 Naibu Katibu Mkuu anaeshughulikia elimu kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Gerald Mweli akizungumza na wanafunzi, walimu na watumishi wa shule kongwe ya wasichana Msalato. Kushoto ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako.
 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako akiagana na wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Wasichana Msalato jijini Dodoma baada ya kumaliza kuzungumza nao.
 Mojawapo ya bweni lililopo katika shule kongwe ya Sekondari Msalato ambapo Waziri wa Elimu na Msafara wake walifika kukagua miundombinu ya shule hiyo.
 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako akizungumza na walimu, watumishi na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Msalato alipofanya ziara ya kukagua miundombinu ya shule hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...