Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Profesa Mohammed Janabi akizungumza na waandishi wa habari wakati alieleza mafanikio ya taasisi hiyo ndani ya miaka minne ya utawala wa Rais Dkt. John Joseph Magufuli na kueleza kuwa Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha taasisi hiyo inaendelea kutoa huduma bora zaidi, leo jijini Dar es Salaam.
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
TAASISI ya moyo ya JKCI ndani ya miaka minne ya utawala wa Rais Dkt. John Joseph Magufuli imefanikiwa kutoa huduma kwa wagonjwa 300,836 katika kliniki (outpatients) ambao walitibiwa na kuruhusiwa huku wagonjwa 14,960 walilazwa kwa ajili ya kupata matibabu zaidi kutoka katika taasisi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati wa kueleza mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha mwaka 2015/2019 Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete Profesa. Mohammed Janabi amesema kuwa Serikali na wadau mbalimbali wamekuwa sehemu ya mafanikio ya taasisi hiyo.
"Taasisi imefanikiwa kufanya pasuaji kubwa kwa kusimamisha moyo kwa wagonjwa 1,537 kwa mafanikio makubwa huku vifo vikiwa ni asilimia 6 sawa na wagonjwa 92, na kwa upande wa upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu dogo linalotobolewa mtambo wa cathlab wagonjwa 4,207 walipata huduma hii huku vifo vikiwa ni asilimia 1.3 tuu sawa na wagonjwa 42" Ameeleza Janabi.
Amesema kuwa huduma zitolewazo na taasisi hiyo zimeweza kuokoa shilingi bilioni 86 kwa kufanya upasuaji kwa wagonjwa 5,744 na kueleza kuwa wagonjwa hao wangetibiwa nje ya nchi Serikali ingetumia zaidi ya shilingi bilioni 172 katika kulipia gharama za upasuaji.
Aidha amesema kuwa ndani ya miaka mitano watakuwa wamefanikisha programu ya kupandikiza moyo na hadi sasa Serikali tayari imetoa shilingi bilioni 4.6 kwa ajili ya kununua vifaa ili kuweza kutoa huduma bora zaidi.
Vilevile amesema kuwa ujuzi kwa wataalamu umeongezeka kwa kiasi kikubwa na pasuaji zikizofanyika zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Kuhusiana na wingi wa wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hiyo Prof. Janabi amesema;
" Kwa siku wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hiyo ni kati ya 300 hadi 500 kwa siku na Serikali yetu kwa kushirikiana na Serikali ya China itajenga hospitali kubwa ya moyo katika eneo la mloganzila na hatua za awali zimeshakamilika" amesema.
Janabi amesema kuwa pia taasisi hiyo imefanikiwa kununua mashine mpya za matibabu ya moyo zikiwemo za kuchunguza jinsi moyo unavyofanya kazi, mashine ya kuchunguza mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi, mashine ya X-RAY pamoja na vifaa vya upasuaji.
Kwa niaba ya taasisi hiyo Profesa Janabi amehaidi kuendelea kutoa huduma bora na za utaalamu wa hali ya juu na hiyo ni pamoja na kutoa elimu ya magonjwa ya moyo kupitia vyombo vya habari pamoja na kutembelea hospitali za Mikoa na Wilaya na kuendelea kutoa huduma kupitia taasisi hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...