Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Biashara wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), CPA Josephine Kolola leo akizungumza na Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani wa Mamlaka hiyo, wanaoshiriki mafunzo ya uandaaji na uwakilishwaji wa vitabu vya Hesabu za fedha kwa kuzingatia viwango vya Kimataifa vya Uhasibu kwa Taasisi za serikali (IPSAS accrual), yanayofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Jengo la Pili la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA_TB2). Mafunzo hayo yamefunguliwa na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Renatus Msanjira.
Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wakimsikiliza kwa makini aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Renatus Msangira akifungua mafunzo ya uandaaji na uwakilishwaji wa vitabu vya Hesabu za fedha kwa kuzingatia viwango vya Kimataifa vya Uhasibu kwa Taasisi za serikali (IPSAS accrual), yaliyoanza leo kwenye ukumbi wa mikutano wa Jengo la Pili la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA_TB2).
Aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Renatus Msangira akifungua mafunzo ya uandaaji na uwakilishwaji wa vitabu vya Hesabu za fedha kwa kuzingatia viwango vya Kimataifa vya Uhasibu kwa Taasisi za serikali (IPSAS accrual), yaliyoanza leo kwenye ukumbi wa mikutano wa Jengo la Pili la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA_TB2), kwa kushirikisha Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani.
Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Paul Rwegasha (kushoto) akizungumza na Kamishna Msaidizi wa Zimamoto na Uokoaji (ACF) Bakari Mrisho (wa pili kushoto), aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Renatus Msangira (kulia), na Meneja wa Utawala na Rasilimali Watu na Mafunzo, Abdi Mkwizu.
Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), leo wakiwa kwenye mafunzo ya uandaaji na uwakilishwaji wa vitabu vya Hesabu za fedha kwa kuzingatia viwango vya Kimataifa vya Uhasibu kwa Taasisi za serikali (IPSAS accrual), yanayofanyika kwa siku tano kwenye ukumbi wa mikutano wa Jengo la Pili la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA_TB2).
******************************

Na Bahati Mollel, TAA.

MAFUNZO ya uandaaji na uwakilishwaji wa vitabu vya Hesabu za fedha kwa kuzingatia viwango vya Kimataifa vya Uhasibu kwa Taasisi za serikali (IPSAS accrual), yameelezwa kuwa yataondoa hoja za Wakaguzi wa ndani na nje.

Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Biashara wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), CPA Josephine Kolola amesema hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyoanza leo kwenye Jengo la Pili la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB2) kwa kushirikisha Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani wa Mamlaka hiyo, ambapo yanashirikisha washiriki 56 kutoka Viwanja vya ndege vya serikali vilivyopo Tanzania Bara.

“Pia ni matarajio yangu baada ya mafunzo haya kutawezesha kupungua kwa kiasi kikubwa na hata kutokuwepo kabisa kwa hoja za wakaguzi wa ndani na nje kutokana na uelewa utakapopatikana kwa washiriki,” amesema CPA Kolola.

CPA Kolola amesema mafunzo hayo pia yatashirikisha suala zima la maadili ya Uhasibu (Code of Conduct & Ethics for Professional accountants); uzingatiaji wa miongozo mbalimbali ya kifedha kadiri inavyotolewa na serikali (MoFP), hivyo kutoa taarifa za fedha zenye kuonesha uhalisia na mwelekeo wa Mamlaka wenye tija kwa watumiaji wa taarifa hizo.

“Mafunzo haya yatawakumbusha wahasibu wote wa Mamlaka dhamana waliyonayo katika masuala yote ya kifedha hivyo kuwa makini katika kazi zao za kila siku kwa kuhakikisha umakini wa kuingiza data za mapato, matumizi, madeni nk, hivyo kuepusha makosa kwenye vitabu vya hesabu,” amesema CPA Kolola.

Awali akifungua mafunzo hayo aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa TAA, Renatus Msangira akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu Mhandisi Mshauri Julius Ndyamukama, aliwataka wahasibu na wakaguzi hao wa ndani kuhakikisha wanatunza siri za hesabu ya taasisi hiyo, kwa kuwa ni kosa la kisheria kuzitoa kwa watu wasiohusika.

“Hesabu za taasisi au ofisi yeyote ya Umma hazipaswi kusambazwa hovyo kwa watu wasiostahili hizo ni moja ya siri na zinapaswa kutunzwa vyema, na hutolewa kwa kibali maalum endapo itahitajika, lakini sio zaidi ya hapo” alisisitiza Msangira.

Pia amewataka washiriki hao wapatao 56 kutoka viwanja mbalimbali vya ndege Tanzania Bara watumie fursa hiyo kwa kuboresha utendaji wao wa kazi kwa kushirikiana vyema na Vitengo na Idara zilizopo, ili kufanikisha lengo la Mamlaka la kuwa na hesabu bora.

Hatahivyo, aliwasisitizia kufanya kazi kwa upendo, uadilifu na amani kwa kutojiwekea msongo wa mawazo kwani wanaweza kuharibu kazi kutokana na akili kutokuwa sawa.

“Nina imani kubwa kwamba mafunzo haya yatawaongezea kitu kikubwa sana katika kada zenu, hivyo mjaribu kuzingatia kazi na kada zenu na msiingilie kazi zisizowahusu,” amesema.

Halikadhalika aliwasisitizia kujiendeleza zaidi kitaaluma ili wapate CPA, ambayo itawaruhusu kukafanya kazi kwa viwango vinavyohitajika kitaifa na kimataifa.

Mafunzo hayo ya siku tano yanaendeshwa na Wataalam kutoka Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi Tanzania (NBAA).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...