Veronica Simba – Chato

Walimu wa Shule ya Msingi Tumaini iliyopo kijiji cha Imalabupina, Kata ya Iparamasa, wilayani Chato, Mkoa wa Geita, wameishukuru Serikali kwa kuunganisha umeme shuleni hapo wakisema nishati hiyo italeta mapinduzi makubwa ya taaluma.

Wametoa shukrani hizo Februari 24, 2020 baada ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani kuwasha rasmi umeme katika Shule hiyo.

Akieleza namna shule hiyo itakavyonufaika, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule hiyo, Goodluck Mamele amesema uwepo wa umeme utarahisisha zoezi la uchapaji wa karatasi za mitihani na majaribio mbalimbali ambayo hufanyika mara kwa mara shuleni hapo.

Alisema, awali walikuwa wakilazimika kupeleka mitihani kwenye ‘stationeries’ kwa ajili ya kuchapisha huku wakiingia gharama kulipia huduma hiyo.

“Sasa naamini taaluma itapanda maana badala ya kuchangisha fedha za kuchapishia mitihani, tutaifanya kazi hiyo hapahapa shuleni.”
Aidha, alisema uwepo wa umeme shuleni utawasaidia baadhi ya walimu ambao hawana elimu ya kutumia Kompyuta, kujifunza utaalamu huo katika muda wao wa mapumziko baada ya saa za kazi.

Kwa upande wake, Mwalimu Moses Manyilizu, amesema uwepo wa umeme utawezesha sasa kufundisha somo la TEHAMA kwa wanafunzi kwani awali mazingira yalikuwa siyo rafiki.

Kwahiyo, sasa hivi kwakuwa tuna umeme, najua kupitia Mfuko wa Shule, tutajitahidi kupata kompyuta kwa ajili ya kuwafundisha watoto somo la TEHAMA.”

Naye Mwalimu Habi Nyanda ameeleza kuwa umeme utawawezesha wanafunzi wanaopenda kujisomea kwa muda wa ziada kufanya hivyo hata nyakati za usiku shuleni hapo hivyo kuboresha zaidi kiwango cha ufaulu kwao.

Akizungumza baada ya kuwasha umeme, Waziri Kalemani amewaasa wanafunzi na walimu wa shule hiyo, kuitumia nishati hiyo kama chachu kwao katika kuboresha taaluma shuleni hapo.

Katika ziara hiyo, Waziri pia aliwasha umeme kwenye taasisi mbalimbali za umma na makazi ya wananchi katika vijiji vya Butobela na Mwendakulima vilivyopo Kata ya Butengolumasa.
 Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, akiwaasa wanafunzi na walimu wa Shule ya Msingi Tumaini, iliyopo Kata ya Iparamasa wilayani Chato, kutumia umeme kuboresha taaluma baada ya kuwasha rasmi nishati hiyo shuleni hapo Februari 24, 2020 akiwa katika ziara ya kazi.
 Baadhi ya Walimu wa Shule ya Msingi Tumaini, iliyopo Kata ya Iparamasa wilayani Chato, wakifuatilia hafla ya uwashaji rasmi umeme shuleni hapo, Februari 24, 2020 ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani).
 Sehemu ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Tumaini, iliyopo Kata ya Iparamasa wilayani Chato, wakifuatilia hafla ya uwashaji rasmi umeme shuleni hapo, Februari 24, 2020 ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani).
 Mashine ndogo ya kusaga nafaka katika kijiji cha Butobela, Kata ya Butengolumasa, wilayani Chato ikiwa imeunganishwa umeme. Taswira hii ilichukuliwa Februari 24, 2020 wakati Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) alipokuwa akiwasha rasmi umeme eneo hilo.
 Baadhi ya viongozi waandamizi na wataalamu kutoka Wizarani, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakifuatilia hafla ya uwashaji rasmi umeme katika Shule ya Msingi Tumaini iliyopo Kata ya Iparamasa, wilayani Chato, Februari 24, 2020 ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani).
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Imalabupina, Kata ya Iparamasa, wilayani Chato. Kulwa Mapembe akimkaribisha Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa pili-kushoto), aliyefika kuwasha rasmi umeme katika Shule ya Msingi Tumaini iliyopo kijijini hapo, Februari 24, 2020 akiwa katika ziara ya kazi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...