Daktari Bingwa wa Macho wa MNH-Mloganzila, Dkt. Catherine Makunja akimfanyia uchunguzi wa awali, Bi. Ashura Abdallah aliyefika hospitalini hapa kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa awali wa macho.
Mtaalam wa kupima macho wa MNH-Mloganzila, Dkt. Martin Francis akimpima uwezo wa macho kuona, Bi. Nasra Yusuph.

Mtaalam wa kupima macho MNH-Mloganzila, Dkt. Nestory Massawe akimpima uwezo wa macho kuona mbali na karibu, Bi. Sophia Shomari.

Baadhi ya wananchi waliofika kufanyiwa uchunguzi wa macho.
 
Na Lightness Mndeme

Mamia wajitokeza kufanyiwa uchunguzi wa awali wa macho katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila katika maadhimisho ya Siku ya Presha ya Macho Duniani.

Kauli mbiu katika maadhimisho haya ni ‘Tokomeza Shinikizo la Macho lililojificha’ lengo ikiwa ni kufanya uchunguzi wa macho, kupima presha ya macho, kutoa ushauri juu ya magonjwa ya macho pamoja na matibabu yake.

Daktari wa Macho wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Catherine Makunja amesema ugonjwa wa presha ya macho unathiri sana watu wenye umri wa miaka 40 na kuendelea sababu ikiwa ni magonjwa ya kurithi katika familia, kisukari, unywaji pombe kupita kiasi, uvutaji sigara na matumizi ya dawa bila kufuata ushauri wa daktari.

Akifafanua juu ya ugonjwa wa presha ya macho, daktari amesema kuwa ugonjwa huu mara nyingi hauna dalili hivyo ni vema watu wakajijengea tabia ya kufanya uchunguzi wa macho mara kwa mara.

“Tatizo la presha ya macho huwa mara nyingi linapoanza halina dalili na wagonjwa mara tu wanapofanyiwa vipimo huwa wanakutwa na ugonjwa huu ndio maana tunatoa hamasa kwa watu kuja kufanya uchunguzi mara kwa mara” amesema Dkt. Makunja.

Sambamba na hilo daktari wa macho wa MNH-Mloganzila, Dkt. Judith Mwende amefafanua kuwa mbali na wagonjwa kufanyiwa uchunguzi wa macho na kugunduliwa kuwa na presha ya macho, madaktari hufanya uchunguzi wa kina ili kutambua aina ya presha ya macho aliyonayo mgonjwa.

Kwa upande wake mmoja wa watu waliojitokeza kufanyiwa uchunguzi hospitalini hapa leo, Bi. Nora Charles amewashauri Watanzania kujitokeza kwa wingi kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali na kupatiwa matibabu mapema.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...