Diwani wa Kata ya Utemini, Baltazar Kimario.


Na Ismail Luhamb,Singida.

DIWANI wa Kata ya Utemini Manispaa ya Singida, Baltazar Kimario, ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kujenga chuo kipya cha ufundi stadi cha kwa ajili ya watu wenyeulemavu mkoani hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari katika kikao cha baraza la madiwani kilicho keti mwishoni mwa wiki, Kimario, alisema chuo kinachoendelea kutumika kilijengwa miaka ya 70 hivyo miundombinu yake imechakaa inahitaji ukarabati wa mkubwa.

Kimario alisema chuo cha sasa kimezingirwa na maji, kitendo kinachohatarisha maisha ya wanafunzi na walimu wao.

Akifafanua alisema kwa muda mrefu amekuwa akiilalamikia mitaro ya maji zaidi ya mitatu kuelekezwa kwenye chuo hicho inayochangia mazingira ya chuo hicho yasiwe rafiki.

“Chuo hiki kinapokea wanafunzi wenye ulemavu kutoka mikoa mbalimbali nchini ambao wana ulemavu wa aina tofauti wakiwemo wenye uoni hafifu hivyo ni muhimu mazingira ya chuo yakaboreshwa”, alisema..

“Aidha,eneo limekuwa chepechepe kutokana na kufumuka kwa chemuchemu nyingi.Mlemavu anayetumia baiskeli ya tairi tatu, fimbo/ magongo au wenye uoni hafifu mazingira ya chuo kwa sasa, sio rafiki”.

Kutokana na hali hiyo Kimario, alisema kama kutakuwa hakuna uwezekano wa kujenga kipya kwa sasa,amependekeza mitaro iliyoelekezwa chuoni hapo itafutiwe mkondo mwingine.

Kwa upande wake mkuu wa chuo hicho, Fatuma Malenga, alisema mitaro hiyo imesababisha maji ya mvua kusambaa sehemu kubwa ya chuo na kusababisha changamoto ya kupitika.

“Kuna darasa maji yanatoka chini ya sakafu baadhi ya majengo misingi yake maji yametuama kwa muda mrefu na kwa miaka kadhaa nimekuwa nikiilalamikia mitaro hii, lakini ufumbuzi wa tatizo hili kuondoa au kuichepusha mitaro bado haujapatikana”. alisema Malenga.

Mwanafunzi wa fani ya uselemala, Jackson Nyamhanga, ametumia fursa hiyo kuiomba serikali iboreshe mazingira ya chuo hicho kikongwe ili kiwe kimbilio kwa walemavu kupata haki yao ya elimu.

Mwanafunzi huyo kutoka mkoani Geita, amesema endapo chuo kitafunguliwa na maji yakaendelea kusambaa chuoni hapo itawawia vigumu kuendelea na masomo kutokana na vyoo kujaa maji.

Wakati huo huo, Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Manispaa ya Singida, Mhandisi Lambert Bayona, alisema kwa ujumla chuo hicho kimejengwa kwenye eneo la maji lenye chemuchemu.

“Hii mitaro inayolalamikiwa inapitisha maji yanayotoka kwenye chemuchemu za sehemu mbalimbali katika eneo la Sabasaba. Maeneo hayo yapo juu au kwenye mwinuko. Chuo chenyewe kipo chini. Kwa hiyo sio kweli mitaro imeelekezwa chuoni, maji yanafuata mkondo wake ”, alisema Bayona.

Hata hivyo, Bayona, ameahidi kutatua changamoto hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...