PROGRAM ya mafunzo ya kuhusu namna bora ya kuendesha, kukuza na kutambua fursa zilizopo kwenye sekta ya utalii hapa nchini inatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni jijini  Mwanza.

Zaidi, mafunzo hayo yanalenga pia kuandaa wadau wa utalii hapa nchini ili waweze kutoa huduma zao kwa weledi huku wakizingatia kanuni za kiafya pindi sekta hiyo itakapoimarika baada ya kuathirika kwa kiasi kikubwa  kutokana na janga la ugonjwa wa homa ya mapafu (COVID0-19) unaosababishwa na virus vya corona ambalo limeyakumba mataifa  mengi.

Akizungumza mwishoni mwa wiki jijini Mwanza wakati wa hafla fupi ya kusaini hati ya makubaliano kuhusu utekelezaji wa program hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), Prof Costa Mahalu alisema program hiyo itatatekelezwa kwa ushirikiano wa karibu baina ya chuo hicho pamoja na Kampuni ya Real Pr Solutions (RPR).

Kulingana na makubaliano hayo,  Chuo cha SAUT kitahusika katika utoaji wa mafunzo hayo yanayotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu sambamba na kutoa vyeti kwa wahitimu huku kampuni  ya RPR ikihusika katika kutafuta fedha za uwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka kwa wadau mbalimbali hususani mashirika na taasisi  zinazohusika na sekta hiyo.

"Mlipuko wa COVID-19 ni kama umesababisha dunia isimame kwa muda kwa maana kuwa mataifa mengi hususani yale tunayoyategemea kwenye masuala ya utalii yamewafungia raia wake ndani na huduma za ndege pia zimefungwa. Hali hiyo imesababisha athari kubwa kiuchumi hususani katika sekta ya utalii hapa nchini kama ambavyo Waziri anaehusika na utalii nchini alivyobainisha hivi karibuni. SAUT na wadau wengine tumechukua hatua na mafunzo haya kwa wadau wa utalii utasaidia kuiboresha tena sekta hii muhimu’’. Alisema Prof Mahalu.

Alisema SAUT na RPR zinafanya kazi kwa mashauriano ya karibu  na washirika wengine ili kusaidia sekta ya utalii na kuhakikisha sekta hiyo inarejea kikamilifu huku pia wadau wakichukua tahadhari zote za kiafya dhidi ya virusi vya corona.  Aliongeza kwamba mpango pia unalenga kuwaandaa vizuri wakazi wa Kanda ya Ziwa ili wawe mstari wa mbele kuunadi  utalii uliopo Kanda hiyo.

“Tunatarajia kwamba awamu ya kwanza ya program yetu itaanza na jiji la Mwanza ambapo tunalenga kuwafikia wadau wengi iwezekanavyo watakaotoka wilaya zote za mkoa wa Mwanza ambapo tumejipanga kupokea watu wasiopungua 2000 watakaopata mafunzo kwa awamu,’’ alisema huku akiitaja mikoa itakayofuata kuwa itakuwa ni Geita, Simiyu, Shinyanga, Mara na Kagera .

Alisema katika utoaji wa mafunzo hayo umeandaliwa mpango kabambe utakaohakikisha washiriki wanajikinga dhidi ya maambukizi ya virus vya Corona ikiwemo kuendesha mafunzo hayo kwenye maeneo ya wazi ili kuepuka msongamano kwenye eneo dogo.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Real PR Solutions Kanda ya Ziwa Bi Magreth Laizer alisema kampuni hiyo yenye uzoefu kwenye masuala ya Mahusiano ya Umma, Masoko imejipanga kuhakikisha inafanikisha zoezi la ukusanyaji wa fedha kutoka kwa wadau mbalimbali hasa wa utalii kwa ajili ya kuwezesha uendeshaji wa program hiyo muhimu.

" Sekta ya Utalii ni miongoni mwa sekta muhimu zinazochangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wetu  hivyo tumeguswa sana na namna hali ilivyo kwa sasa na kwa kushirikiana na wenzetu wa SAUT pamoja na wadau wengine tunaamini tutaisaidia serikali yetu kuiboresha tena sekta hii kwa kuandaa nguvu kazi yenye weledi wa kutosha lakini pia itakayoweza kufanya shughuli za utalii kwa kuzingatia taadhari za kiafya kutokana na janga hili la Corona,’’  alisema.

 Mbali na mikoa ya Kanda ya Ziwa Bi Laizer aliitaja mikoa mingine itakayoguswa na program hiyo kuwa ni pamoja na mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, Songwe, Njombe, Mtwara, Ruvuma, Lindi, Dodoma, Singida, ,Tanga, Manyara, Dar es Salaam, Morogoro na Pwani.

Aidha, katika kuuboresha zaidi ufanisi wake, mpango huo pia utahusisha kampuni ya PEAL Performance iliyojikita kwenye masuala ya uendelezaji ustadi wa watu hususani katika sekta ya utalii .

“Jukumu letu kubwa kwenye hili ni kuhakikisha tunawasaidia washiriki hasa vijana kutambua fursa zilizopo kwenye sekta ya utalii na namna ya kuzitumia vizuri ili kupunguza pia tatizo la ajira kwenye jamii zetu,’’ alibainisha Bw Philemoni Kisamo,Mkurugenzi Mtendaji kampuni ya PEAK Perfomance.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), Prof Costa Mahalu (Kulia) pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni ya Real PR Solutions (RPR), Kanda ya Ziwa Bi Magreth Laizer (Kushoto) wakisaini makubaliano ya utekelezaji wa pamoja mpango wa mafunzo kwa wadau wa utalii ujulikanao  “Utalii Mpya Wakati Na Baada Ya Corona"  unaolenga kutoa mafunzo kuhusu namna bora ya kuendesha, kukuza na kutambua fursa zilizopo kwenye sekta ya utalii hapa nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...