Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani, akiwaonyesha kifaa cha Umeme tayari (UMETA) wakazi wa Kijiji cha Loya wilayani Uyui Mkoani Tabora, alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya usambazaji wa umeme vijijini, katika kijiji hicho, Mei 19,2020.
 Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani, akiwasha mashine ya kusaga na kukoboa nafaka ambayo sasa inatumia umeme badala ya mafuta mazito kujiendesha, inayomilikiwa na Mkazi wa Kijiji cha Loya wilayani Uyui Mkoani Tabora, wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya usambazaji wa umeme vijijini, katika kijiji hicho, Mei 19, 2020.
 aziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani,(katikati), Mbunge wa Igalula, Musa Ntimizi na Viongozi wengine walioambatana nao wakipita katika mitaa ya Kijiji cha Loya wilayani Uyui Mkoani Tabora, walipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya usambazaji wa umeme vijijini, katika kijiji hicho,na kuwasha umeme Mei 19,2020.
Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani, akiwasha umeme katika moja ya Ofisi za Kijiji cha Loya wilayani Uyui Mkoani Tabora, wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya usambazaji wa umeme vijijini, katika kijiji hicho, Mei 19,2020.

Na Zuena Msuya Tabora,
Wakazi wa Kijiji cha Loya wilayani Uyui mkoani Tabora, wameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kuwaunganisha na kuwawashia umeme katika kijiji hicho ambacho awali wakazi hao walikuwa wakiona kama ni ndoto.
Wakazi hao, wameeleza hayo baaada ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani kuwasha umeme katika kijiji hicho na kukagua maendeleo ya usambazaji wa umeme vijijini katika wilaya hiyo, Mei 19, 2020.
Wakazi wa Kijiji hicho walisema kuwa, miaka mingi wamekuwa wakipewa ahadi zisizotekelezeka na wakati mwingine wamekuwa wakikatishwa tamaa ya kupata umeme kwa kuwa kijiji hicho kiko umbali mrefu kutoka ilipo miundombinu ya umeme pia kuwa na jiografia isiyorafiki kufika maeneo hayo.
“Huyu Waziri ameandika historia hapa Loya, haijawahi kutokea kiongozi mkubwa ngazi ya Waziri kufika katika kijiji chetu tangu kimeanzishwa, wengi wanakuja katika wilaya hii lakini wanaishia huko mujini tu vijijini hawafiki, na amekuja kutuwashia umeme kabisa kwakweli tunamshukuru sana huyu Dkt. Kalemani, pia tunamshukuru Rais Magufuli kumkubalia huyu waziri kuja huku kwetu kutuletea umeme, abarikiwe sana”, alisema mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Josephat Wamalulu.
Kwa upande wake Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani alisema baada ya kusikia malalamiko na kuona uhitaji mkubwa wa umeme kwa kijiji hicho ambapo bado hakijafikiwa na mradi wa kusambaza umeme (REA) kwa kipindi hiki,nililiagiza Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kupeleka umeme kwa gharama zao katika kijiji hicho.
Alisema kijiji cha Loya kinawakulima wengi wa mpunga, karanga na wafanyabiashara ambao wanahitaji huduma ya umeme katika kuendesha shughuli zao za kiuchumi.
Kwa mantiki hiyo, TANESCO ilitenga zaidi ya shilingi Bilioni 3 ili kuhakikisha umeme unafika katika kijiji hicho, ambacho kiko umbali mrefu sana kutoka ilipopita miundombinu ya umeme.
“Niliwaagiza TANESCO kuleta umeme hapa Loya,kama mlivyoona Loya inawakazi wengi wakulima na wafanyabiashara ambao wanahitaji umeme katika shughuli zao, tumetenga zaidi ya shilingi Bilioni tatu kuhakikisha umeme unafika hapa na tutapeleka katika vijiji vingine cha msingi hapa ni ninyi wananchi kusuka nyaya katika nyumba zenu, na kulipia shilingi 27,000 tu umeme utawafikia”, alisema Dkt. Kalemani.
Aidha aliwaagiza TANESCO, kuendelea kusambaza na kuwawasha umeme kwa wakazi wa eneo hilo waliokwisha kulipia gharama za kuunganishiwa umeme ndani ya siku 7 baada ya kulipia. 
Aliwataka wakazi wa Loya kutumia umeme huo kujiendeleza kiuchumi badala ya kuutumia umeme huo kwa kuwasha taa peke yake.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Igalula, Musa Ntimizi aliwataka wafanyabiashara katika kijiji hicho kutanua wigo wa kibiashara na wakulima wa mpunga kuongeza thamani ya mazao yao ili kupata faida zaidi.
Pia wakazi hao wachangamkie fursa hiyo ya umeme kwa kuazisha biashara na viwanda vidogo vinavyotumia umeme, kama vile Saloni, Mashine za kusaga na kukoboa nafaka, kuchomelea vyuma na kadhalika.
“Umeme huu umekuja wakati muafaka kwa wakazi wa Loya, sasa hivi tutaanza kuuza mchele safi na bora badala ya mpunga ambao hata hivyo wafanyabiashara kutoka nje ya hapa walikuwa wakiwalangua kwa wakulima wa eneo hili, sasa hivi kutakuwa na mashine za kisasa za kukoboa mpunga na wakulima wataongeza thamani ya mazao yao na kunufaika zaidi na kilimo cha mpunga”, alisema Ntimizi.
Aliwaeleza wakazi hao kuwa wasikubali kuuziwa nguzo za umeme, pia watumie wakandarasi walioidhinishwa na TANESCO kufanya kazi ya kutandaza nyaya katika nyumba zao ili kuepuka vishoka.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...