KUTOKANA mahitaji na gharama kubwa za kuandaa majimoto kwa matumizi mbalimbali hususani maeneo yenye watu wengi (hotelini, nyumbani na hospitalini n.k), Jumbe Haruna amebuni mfumo unaopasha maji mengi kwa gharama nafuu.

Mbunifu Jumbe, ambaye ni mhitimu wa siku nyingi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) alikosomea masuala ya bomba na mifumo ya maji anasema alikuwa anafanya kazi hotelini ambako miongoni mwa changamoto alizokuwa anakutana nazo ni kuharibika kwa ‘heater’ jambo lililokuwa lina wagharimu fedha nyingi.

“Tenki moja la kuchemshia maji lilikuwa linauzwa si chini ya Shilingi laki tano, ni fedha nyingi. Mfumo ukisumbua wateja walikuwa wanalalamika. Hapo ndipo nilipoanza kuumiza kichwa kutafuta suluhu ya kudumu,” anakumbuka Jumbe.

Baada ya kufikiria sana, Jumbe alipata wazo na kutengeneza mfumo unaotumia taka ngumu au kuni chache kupasha kiasi kikubwa cha majimoto. Kwa tenki la kuchemsha lita 200, anasema zinahitajika lita nyingine 600 za maji baridi kukidhi mahitaji ya mteja kuoga.
Mbunifu Jumbe Haruna akizungumza na waandishi wa habari.

Kutokana ubunifu huu na unafuu wake, Jumbe amepata wateja ndani ya eneo lake anakotengenezea mfumo wake huku akiweka juhudi za kutafuta wateja wapya nje ya wilaya ya Kilosa.

Mfumo huo tayari unatumika katika hoteli ya kitalii Camp Bastian iliyopo wilayani kata ya Mikumi Wilaya ya Kilosa, Mussa Said ambaye ni meneja wa hoteli ya kitalii ya Camp Bastian anasema, wanatumia mfumo huo tangu mwaka 2013 hoteli hiyo ilipoanzishwa na hatujawahi kupata malalamiko yoyote.

“Tenki la kuchemshia linaweza likaa zaidi ya miaka mitatu mpaka minne lisiharibike. Hata ikitokea changamoto, unamwita mbunifu anakuja kurekebisha na linaendelea kufanyakazi kama kawaida,” anasema Mussa.
Ingawa alisoma VETA ya mjini Morogoro, Jumbe analelewa kitaaluma na VETA Mikumi Wilaya ya Kilosa ambako alipata nafasi ya kuwa mwalimu kwa muda kabla hajaacha kazi hiyo na kujielekeza zaidi kwenye ubunifu wake.
Mbunifu Jumbe akionesha mfumo wa zamani unaotumia taka ngumu na kuni ambao ameofunga katika Hotel ya Chuo cha Veta Mikumi.


Msimamizi wa vyumba katika hoteli ya VETA, anasema  hawachemshi maji siku zote kwani ukichemsha maji leo yanaweza yakatumika mpaka siku tatu bila kupoa, “Muda wote maji yanakuwa ya moto, mgeni akiingia chumbani hana haja ya kuomba msaada wa mhudumu kwaajili ya maji moto, kwani maji yanakuwepo tayari,” anasema msimamizi huyo.

Mfumo wa Jumbe hautumiki hotelini pekee, takwimu za Wizara ya Maliasili na Utalii zinaonesha kuwa mpaka mwaka 2017 kulikuwa na vyumba vinavyotosha wageni 38,000 tu katika hoteli za kitalii ingawa mahitaji halisi ni vyumba 70,000 nchi nzima.

Kundi jingine linaloweza kunufaika na mfumo huo, anasema ni hospitali hasa wodi za wazazi ambako kuna uhitaji mkubwa.

“Natamani Wizara ya afya inipatie fursa ya kutatua kero ya ukosefu wa majimoto kwa wanawake wanaojifungua. Nina uhakika wa kuimaliza kwa asilimia 100,” anasema Jumbe.

Mbunifu huyo aliyeshiriki Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) yanayoandaliwa kila mwaka na Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) anasema ruzuku aliyopewa imemsaidia kwa kiasi kikubwa kukamilisha na kukuza mradi wake.

Kutokana na ruzuku hiyo anasema ameweza kuboresha ubunifu wa mfumo wa tenki la kuchemshia maji na sasa anaandaa mfumo utakaotumia umemejua kuchemsha maji hivyo kukidhi mahitaji ya wateja wake wanaopenda kulinda mazingira kwa kutotumia mabaki ya miti, kuni wala mkaa.   
Mbunifu Jumbe akionesha mfumo mpya ambao ameubuni unaotumia jua kupata maji moto. 
Licha ya mfumo huo unaotumika kwenye maeneo yenye watu wengi, anao mwingine wa kuandaa maji ya moto kwa matumizi ya nyumbani.
“Huu unatumia tenki la lita 60 kuchemsha maji ambayo yanatakiwa kupozwa na lita 180 za maji baridi. Maji haya hupata moto wakati mtu anapika jikoni hivyo huhitaji chanzo kingine cha nishati,” anaeleza Jumbe.

Mfumo huo, anasema unafungwa jikoni na kinachotakiwa ni kuchukua vipimo vya ukubwa wa jiko husika kabla ya kuuweka na familia ikaanza kunufaika nao. Kwa jiko lolote lenye urefu wa walau mita mbili, anasema unaweza ukafungwa kwa matumizi.

Jumbe ni miongoni mwa zaidi ya wabunifu 50 waliopewa ruzuku na COSTECH mwaka 2019 ili kuendeleza miradi ya bunifu zao.

Mkurugenzi mkuu wa COSTECH, Dk Amos Nungu anasema inachofanya Serikali ni kuweka mazingira rafiki kwa watu wenye mawazo ya kibunifu kuonekana hivyo kujiweka kwenye nafasi ya kufanya uzalishaji wa kibiashara.

“Tunawaibua. Kwa mfano huyu wa majimoto anaweza akaonekana na wafanyabiashara wanaohitaji mfumo wake kwenye hoteli, hospitali au shule. Wakati akitatua changamoto za wafanyabiashara hao naye atakuwa anajiingizia kipato,” anasema Dk Nungu.

VETA wanena
Kaimu mkuu wa Chuo cha VETA Kata ya Kata ya Kata ya Kata ya Mikumi Wilaya ya Kilosa Wilaya ya Kilosa Wilaya ya Kilosa Wilaya ya Kilosa, Emmanuel Munuo anasema kwa uzoefu walioupata kwa kutumia mfumo wa majimoto ulioundwa na Jumbe, anaamini unaweza ukatumika mahali popote hata palipo na maji chumvi hata pasipo na umeme.

“Tumeutumia mfumo wake kwa muda mrefu, ni mzuri. Unapunguza gharama kwa kiasi kikubwa,” anasema Munuo.

Kutokana na jitihada binafsi za Jumbe, mkuu huyo wa chuo anasema wanafunzi wengi wamehamasika kuelekeza nguvu zao katika ubunifu na ujasiriamali kwani wanaiona fursa iliyopo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...