Kusikitishwa na taarifa
ya vitendo vya baadhi ya Madaktari na Wauguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa,
Mwananyamala kuwanyanyapaa na kuwasumbua Wagonjwa
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora (THBUB) imesikitishwa na taarifa ya vitendo vinavyofanywa na baadhi ya
Madaktari na Wauguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Mwananyamala vya
kuwanyanyapaa na kuwasumbua wagonjwa wanaoenda kupata matibabu kwa kuwataka
wagonjwa hao kwenda kufanya vipimo vya Korona kabla ya kuanza kupata matibabu.
Tume imesikitishwa na jambo hilo kwa
sababu kila mwananchi ana haki ya kufurahia haki ya afya kwa kupata matibabu
mazuri na ya uhakika. Madaktari na Wauguzi wanapaswa kutambua kuwa sio kila
Mgonjwa ana maambukizi ya Korona.
Tume inaamini vitendo vya namna hiyo ni
ukiukwaji wa haki ya afya kwa wananchi, na vinaweza kusababisha wagonjwa
kupoteza maisha.
Aidha, Tume inatoa pongezi nyingi kwa
Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu
kwa kuchukua hatua za haraka za kukemea vitendo hivyo vya baadhi ya Madaktari
na Wauguzi ambavyo vinaweza kuchafua taswira nzuri ya sekta ya Afya na jitihada
mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali.
Hata hivyo, Tume inaiomba Serikali iendelee kuhakikisha hospitali
zinaendelea kutoa huduma nzuri kwa Wagonjwa ili kuepusha malalamiko yasiyo ya
lazima.
Mwisho, Tume inaiomba Serikali kufanya
uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha vitendo hivyo vinavyofanywa na baadhi
ya Madaktari na Wauguzi ili kuvitafutia
ufumbuzi wa haraka.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...