Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Azzan Zungu akisoma tamko juu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, mbele ya waandishi wa Habari hii leo Jijini Dodoma. Kwa mwaka huu maadhimisho hayo yatafanyika kwa kutumia vyombo vya habari bila kuwapo kwa mikusanyiko.
Ndugu Wananchi,
Kila tarehe 5 Juni, nchi yetu huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha
Siku ya Mazingira Duniani. Maadhimisho ya Siku ya Mazingira duniani yaliamuliwa
mwaka 1972 katika mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa uliohusu masuala ya Mazingira,
uliofanyika katika Mji wa Stockholm
nchini Sweden. Mkutano huo uliazimia kwamba tarehe 5 Juni, kila mwaka iwe ni siku
ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani.
Ndugu Wananchi,
Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanatoa nafasi ya kutafakari kuhusu hali na umuhimu
wa hifadhi ya mazingira katika nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, kuelimisha
wananchi kushiriki katika shughuli za hifadhi mazingira na mbinu/njia
mbalimbali za kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi, kuenea kwa hali
ya jangwa na ukame, Upotevu wa bioanuai, uharibifu wa tabaka la ozone, na shughuli
nyingine mbalimbali zinazochangia uharibifu wa mazingira
Ndugu Wananchi,
Kama
mnavyofahamu Taifa letu linakabiliwa na changamoto kubwa ya uharibifu wa
mazingira unaotokana na matumizi yasiyoendelevu ya rasilimali za kimazingira.
Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na uharibifu wa ardhi, ufyekaji na
uharibifu wa misitu, uharibifu wa vyanzo vya maji, uharibifu wa makazi ya
viumbe wa majini na upotevu wa bioanuai. Changamoto hizi kwa ujumla
zinasababisha athari kubwa katika masuala ya kiuchumi na kijamii. Katika
kukabiliana na changamoto hizi serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali
imekua ikichukua hatua mbalimbali ili kupambana na hali hii. Mojawapo ya njia
za kupambana na changamoto hii ni kutumia Maadhimisho ya siku ya Mazingira
duniani ili pamoja na mambo mengine kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa
kuhifadhi mazingira kwa maendeleo endelevu.
Ni
kwa muktadha huu, Maadhimisho ya siku ya mazingira duniani kitaifa yalipangwa
kufanyika mkoani Lindi mwaka huu. Kauli mbiu ya maadhimisho haya kitaifa ni Tuhifadhi Mazingira: Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi. Kauli mbiu hii
inaakisi hali halisi ya nchi yetu kuathirika na mabadiliko ya tabianchi. Katika
miaka ya hivi karibuni nchi yetu imeshuhudia kuongezeka kwa matukio ya ukame
mkali na wa mara kwa mara pamoja na mafuriko ambayo yamekua yakiikumba nchi
yetu na kusababisha hasara kubwa ya miundombinu, makazi ya watu na hata vifo
katika baadhi ya sehemu za nchi yetu.
Mfano wa hivi
karibuni mafuriko yaliyoukumba mkoa wa Lindi na kusababisha hasara kubwa takriban vijiji 16 viliathiriwa na mafuriko hayo
pamoja na watu 19 kupoteza maisha kutokana na mafuriko hayo. Aidha, takriban
watu 15,000 wamekosa makazi pamoja na uhaba wa chakula na kuathiriwa na
magonjwa mbalimbali ya mlipuko. Kaulimbiu hii inahimiza jamii kutumia mbinu mbalimbali
za asili na za teknolojia rafiki za kuhifadhi mazingira ikiwemo kilimo cha
matone, nishati mbadala, ufugaji wa mifugo chotara na upandaji wa miti ya asili kwenye vyanzo vya
maji ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi nchini.
Ndugu
Wananchi,
Kama mnavyofahamu, Nchi yetu na dunia kwa ujumla
inakabiliwa na janga la ugonjwa wa COVID-19
unaosababishwa na virusi vya corona. Ugonjwa huu unaambukizwa kwa njia mbalimbali
ikiwemo mikusanyiko ya watu. Uwepo wa janga hili umesababisha kusitishwa kwa
shughuli zinazohusu mikusanyiko ya watu. Aidha, kutokana na hali hiyo, Serikali
imeamua kwamba mwaka huu hapatakuwepo na mikusanyiko kwa ajili ya maadhimisho
ya Siku ya Mazingira Duniani Kitaifa
yaliyopangwa kufanyika mkoani Lindi. Kwa muktadha huo, Serikali kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo wamekubaliana kuwa maadhimisho ya
wiki ya Siku ya Mazingira Duniani yatafanyika kwa kutumia vyombo vya habari pamoja na mitandao
ya kijamii kuelimisha na kuhamasisha jamii kutunza mazingira na kuzingatia njia mbalimbali za kujiepusha na
maambukizi ya ugonjwa wa corona. Aidha, kila Mkoa utafanya shughuli za
maadhimisho hayo kwa kutumia vyombo vya habari vilivyopo kwenye maeneo yao pamoja na mitandao
ya kijamii kwa kuzingatia kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ikiwa ni pamoja na:
mashindano ya
kuandika insha zinazohusu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hotuba za
viongozi, jumbe mbalimbali zitakazotumwa kwenye mitandao ya simu pamoja
mikutano ya kitaalamu kuhusu mabadiliko ya Tabianchi ambayo itafanywa kwa njia
ya mitandao kwa kuzingatia njia mbalimbali za kujiepusha na maambukizi ya
ugonjwa wa Corona.
Ndugu
Wananchi,
Ni
vyema ikafahamika kwamba hifadhi ya mazingira si kazi ya Serikali pekee yake
bali ni jukumu letu sote katika ngazi zote kuanzia ngazi ya kaya. Nitoe wito
kwa vyombo vya habari, taasisi zote za Serikali na asasi za kiraia tusaidiane
katika kuhifadhi mazingira. Watendaji wote katika ngazi zote hatuna budi
kushirikiana katika kutekeleza kwa ukamilifu Sheria na Kanuni za hifadhi ya
mazingira. Kila mmoja ana wajibu na fursa muhimu katika kukabiliana na
changamoto za uharibifu wa mazingira hapa nchini. Ningependa kusisitiza kuwa
tushirikiane katika kufanya jitihada mbalimbali ili kupambana na uharibifu wa
mazingira kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya
tabia nchi. Kila mwananchi akiwajibika katika nafasi yake, tutalinda mazingira
yetu na jamii kwa ujumla. Kwa muktadha huu, shughuli za maadhimisho ya Siku ya
Mazingira hapa nchini mwaka huu pamoja
na mambo mengine, zitalenga kuhamasisha jamii
kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na
kuelimishana jinsi ya kuepuka maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19.
Ndugu Wananchi,
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...