Na
Ismail Ngayonga,MAELEZO-DAR
ES SALAAM
MAZINGIRA
yanatajwa kuwa ni mojawapo ya chanzo kuu cha maendeleo ya sekta zote za
uzalishaji mali na ukuaji uchumi wa taifa lolote duniani na hivyo kuwa
rasilimali muhimu kwa ajili ya mahitaji ya sasa na vizazi vijavyo.
Katika
miaka ya hivi karibuni imedhihirika kuwa mazingira yetu si salama kutokana na shughuli
zisizo endelevu zinavyochangia kwa kiasi kikubwa katika uharibifu wa mazingira
na kusababisha uharibifu wa ardhi, uchafuzi wa mazingira n.k.
Maendeleo
endelevu hayawezi kupatikana bila kutunza mazingira, na ushahidi huo ni pamoja
na kuongezeka kwa hali ya jangwa na ukame, mafuriko na kuongezeka kwa matumizi
ya zebaki katika sekta ya madini hususani wachimabji wadogo wa dhahabu.
Mara
nyingi tumeshuhudia katika uzalishaji wa viwanda, mazingira asilia huharibiwa
sana, hususan kwa taka zitokanazo na uzalishaji na utupwaji wake unaopelekea
kuwapo kwa uharibifu mkubwa wa mazingira asilia, hususan ardhi na hewa.
Pamoja
na Serikali kuchukua jitihada kubwa katika utunzaji na usimamizi wa mazingira,
hali ya mazingira nchini bado si ya kuridhisha, hali inayochangiwa na
changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa rasilimali watu wa kusimamia utekelezaji
wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191 katika ngazi zote.
Akiwasilisha
Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2020/2021, Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Zungu anasema katika
mwaka 2019/20, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamzi wa Mazingira ( NEMC) limefanya
ukaguzi katika miradi ya kijamii na kiuchumi.
Anaongeza
kuwa katika ukaguzi huo jumla ya miradi 1,132 ilifanyiwa tathmini ya uzingatiaji
wa Sheria ya Mazingira nchini ili kuangalia iwapo inaweza kuwa na athari kwa
mazingira.
‘Katika
kipindi hiki, Baraza limepokea malalamiko 257 kuhusu uchafuzi wa Mazingira na
kufanya ufuatiliaji kuhusu malalamiko hayo, ambapo ukaguzi uliofanyika ulibaini
changamoto mbalimbali za kimazingira ikiwemo kutiririsha majitaka kwenye vyanzo
vya maji na makazi ya watu’’ anasema Zungu.
Waziri
Zungu anazitaja changamoto nyingine ni pamoja na Matumizi yasiyo endelevu ya
rasilimali kama misitu ya asili kwa ajili ya kuni na ujenzi, Ukosefu wa mifumo
ya kuhifadhi taka ngumu, Uzalishaji wa hewa chafu, Uzalishaji na usambazaji wa
mifuko mbadala isiyokidhi viwango.
Akifafanua
zaidi Zungu anasema NEMC kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa na
Jeshi la Polisi limetoa maagizo na maelekezo ili kukabiliana na changamoto hizo
na kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kufungua mashitaka ya uchafuzi wa mazingira,
amri za katazo na kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria ya Mazingira na Kanuni
zake.
Anaongeza
kuwa Amri na makatazo 79 kwa wavunja sheria ya mazingira zimetolewa na kufuatiliwa
pamoja na kuendelea kusimamia kesi 12 zinazohusu makosa mbalimbali ya
kimazingira.
Aidha
Zungu anasema katika mwaka 2019/2020, Serikali pia ilifanya mapitio ya Tathmini
ya Athari kwa Mazingira (TAM), usajili wa miradi na utoaji wa vyeti vya mazingira
kwa miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi nchini ili kujiridhisha na
viashiria vya madhara na ubainishaji wa awali wa athari za mradi.
Anasema
katika mwaka wa fedha 2019/20, Baraza limesajili jumla ya Miradi 887 ikiwemo miradi
556 ya Tathmini za Athari kwa Mazingira (TAM) na miradi 331 ya kufanyiwa
Ukaguzi wa Athari za Mazingira, ikiwa ni asilimia 74 ya miradi ambayo
imekusudiwa kufanyiwa mapitio kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/20.
Waziri
Zungu anasema katika mwaka 2019/2020 pia jumla ya miradi ipatayo 375 imepata
vyeti vya mazingira, ambapo miradi 225 ni miradi ya Tathmini za Athari kwa
Mazingira na Miradi 150 ya ukaguzi wa Athari za Mazingira na miradi mingine ipo
katika hatua mbalimbali za upembuzi.
Afya,
ustaarabu na ustawi wa taifa letu kwa ujumla vinategemea sana hali mazingira
yanayotuzunguka, uchafuzi wa mazingira unaathari kubwa kiafya hasa katika uenezwaji
wa magonjwa ya mlipuko, na kuilazimu serikali kutumia gharama kubwa katika
uwekaji wa miji katika mazingira ya usafi.
Mazingira
safi ni maisha yetu, mazingira safi ni uhai wetu, mazingira safi ni afya yetu,
mazingira safi ni uchumi wetu hivyo kila mmoja wetu ajitafakari namna
anavyoweza kuwa na mchango chanya katika kuyaweka mazingira yetu katika hali ya
usafi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...