Na Said Mwishehe, Michuzi TV
UTENDAJI kazi unaofanywa na Kamishna Jenereli wa Magereza Suleiman Mzee (pichani) umemkosha sana Rais Dk. John Pombe Magufuli ambapo amesema anafanya kazi nzuri sana na wakati mwingine amekuwa akimuona ameshika koleo kwa ajili ya kuchimba mchanga akishirikiana na wafungwa.
Akizungumza leo Mei 21 mwaka huu, akiwa katika Ikulu ya Chamwino Mjini Dodoma, Rais Magufuli amesema kuwa alifanya mabadiliko ya Kamishna Jenerali wa Magereza na kwamba aliyeko sasa anafanya kazi sana.
"Nilifanya mabadiliko ya Kamishna Jenerali wa Magerezai, yule bwana si yuko hapa, leo hayuko, anafanya kazi, mara leo anapiga koleo, anajaza mchanga kwenye tipa na wafungwa.
"Lakini katika kipindi cha miezi mitatu hajaomba fedha ya kulisha Magereza, wale waliokuwepo wa vyeo vyeo walikuwa wanamsumbua kidogo, akandika barua na huku ikachelewa, baadae nikamwambia Katibu Mkuu Kiongozi shughulikia hilo.
"Anafanya kazi, nasema anafanya kazi, hapo Magereza ameshapanda mpaka mikorosho, waliouwepo hapo awali wala hawakufanya hivyo, lazima iseme ili kusudi tunakoenda tukatimize yale ambayo watanzania wanapenda, mtu anayekupenda atakwambia ukweli , mtu ambaye hakupendi hakuelezi,"amesema Rais Magufuli.
Hivyo ametumia nafasi hiyo kuhimiza waliopata nafasi kutekeleza majukumu yao kikamilifu wakiwemo wale ambao amewaapisha leo, ambapo wamo mabalozi watatu ambao watakwenda kuwakilisha nchi yetu.
"Kwa hiyo ni matumaini makubwa hata ninyi mabalozi watatu ambao mmeteuliwa mtakwenda kufanya kazi,"amesisitiza Rais Magufuli.
Wakati huo huo ametumia nafasi hiyo kumtaka Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuendelea kufanya kazi na hakuna sababu ya kupunguza kasi yake katika utendaji.
Amesema kuwa Kamishna kwamba baada ya kumpa nafasi hiyo hatarajii baada ya kupata nafasi hiyo kwamba atarudi nyuma na badala yake anatarajia kumuoa akifanya kazi kwa bidii zaidi ya kupambana na kukomesha rushwa nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...