*Ni baada ya kupewa tangazo linalowataka kuondoka eneo hilo ndani ya siku 14


Na Said Mwishehe,Michuzi TV

WAFANYABIASHARA zaidi ya 600 waliopo kwenye Soko la Shekilango jijini Dar es Salaam ambao wamepewa siku 14 na Manispaa ya Ubungo kuondoa sokoni hapo ikiwa pamoja na kubomoa vibanda vyao wamesema hawapo tayari kuondoka lakini wanaomba kukutana na Mkurugenzi wa manispaa hiyo ili wazungunze kwa lengo la kupata muafaka.

Wamesema wameshangazwa kuona wanapelekewa tangazo la kutakiwa kuondoka bila kuelezwa sababu yoyote huku pia wakizungumzia tangazo la kutakiwa kusaini mkataba unaohusu kodi ya pango la fremu zilizopo katika soko hilo ambao hadi sasa hawajapewa wala kuuona.

Wakizungumza leo Mei 10,2020 jijini Dar es Salaam viongozi wa wafanyabiashara wa soko hilo wamesema hawana tatizo lolote na Manispaa ya Ubungo wala Mkurugenzi lakini tatizo lao ni kutoshirikishwa kwenye majadiliano yanayohusu soko hilo wakati nao ni sehemu ya wawekezaji kwani wanatambua ardhi ni mali ya Serikali lakini vibanda vya biashara ni mali za wafanyabiashara wenyewe ambao wamejenga kwa gharama zao.

Wamesema wapo tayari kutekeleza maagizo yote ambayo watapewa lakini ni baada ya kufanyika mazungumzo ya pande zote mbili tofauti na sasa wanaona tu matangaza ya kutakiwa kuondoka eneo hilo la soko.

Akizungumza kuhusu kinachoendelea kwenye soko hilo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya wafanyabiashara hao, David Mrisho amesema wamepokea tangazo kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo ambalo liliwataka kwenda ofisini kwake kusaini mikataba.

Pia amefafanua kwamba tangazo hilo linawataka wafanyabiashara hao kulipa Kodi ya shilingi 150,000 kwa frem za nje na shilingi 50,000 Kwa frem za ndani badala ya Kodi ya Sasa ya shilingi 15000 wanayolipa kwa kila mwezi mbali ya gharama zingine zikiwemo za leseni, na ushuru.

"Hizi gharama za kodi ambazo tunatakiwa kulipa ni kubwa sana kwetu sisi wafanyabiara lakini hata mchakato wake wa kupanga tozo hizo hatukushirikishwa ili nasi tuseme uwezo watu na changamoto tulinazo.Hivyo sisi tunaendelea kuwaomba manispaa tukae pamoja tujadiliane,"amesema.

Amesisitiza kuwa kimsingi wao ni sehemu ya wawekezaji katika soko hilo kwasababu vibanda ni mali yetu na ardhi mali ya serikali na wamekuwepo hapo tangu mwaka 1975 na hatuna matatizo na mamlaka huku akieleza wamekuwa wakilipa kila kinachotakiwa na serikali.Sasa wamepewa tangazo la kuambia wasaini mkataba wa pango za frem na mwisho wa kusaini ilikuwa Aprili 23 mwaka huu.

"Lakini chakushangaza hiyo mikataba ambayo tunatakiwa kusaini hatujawahi kuiona wala kuletewa na sasa tunaambiwa tuondoke ndani ya siku 14 kwa kile walichodai kukataa kusaini mkataba huo ambao hatujawahi kuuona,"amesema Mrisho.

Kwa upande wake Katibu wa soko la Jumuiya  ya wafanyabiashara Shekilango  Adamu Yusuph alisema kuwa kitendo cha kutaka kuondolewa katika soko hilo bila kufanya mazungumza ni kutaka kwenda kuathiri  maisha ya watu zaidi ya 600 ambao nao nyuma yao kuna kundi kubwa la watu wanaowategemea,hivyo nivema busara ikatumika ili kupata ufumbuzi sahihi.

Wakati huohuo mmoja wa wazee wazilishi wa soko hilo ambaye amekuwepo kabla ya soko kuhamishiwa hapo mwaka 1975 baada ya Rais wa awamu ya Kwanza kuwataka kwenda eneo hilo,Hija Bushiri amesema wanachotaka kukifanya manispaa sio haki na huenda kunamipango ya kutaka kumgombanisha Rais John Magufuli na wafanyabiashara hao.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Soko la Shekilango David Mrisho akionesha barua ambayo wafanyabiashara wameamuandikia Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo inayohusu kucheleweshwa kuona mikataba mipyaa pamoja na pandisho kubwa la ada ya pango.
 Mmoja ya waanzilishi wa Soko la Shekilango ambaye amekuwepo hapo tangu mwaka 1975 Hijja Bushiri akitoa ufafanuzi namna walivyohamishiwa eneo hillo enzi za Serikali ya Awamu ya Kwanza
 Katibu wa jumuiya ya wafanyabiashara wa Soko la Shekilango Adam Yusufu akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tangazo ambalo wamepewa na Manispaa ya Ubungo kuwataka kuondoka sokoni hapo ndani ya siku 14
 Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa soko la Shekilango jijini Dar es Salaam David Mrisho akifafanua jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari
 
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...