NA DENIS MLOWE,IRINGA
WALEMAVU wametakiwa kuwa makini kuepuka maeneo hatarishi ambayo yatasababisha kupata kwa urahisi virusi vya corona na kuzingatia elimu inayotolewa na wizara ya afya na wadau mbalimbali juu ya kupambana na kuenea kwa virus vya corona.
Wito huo umetolewa na Mratibu wa Mradi Juu ya kupambana na kuenea kwa Virusi vya Corona kwa Walemavu mkoani Iringa unaofadhiliwa na Taasisi ya Foundation For Civil Society (FCS), Philemon Kisinini wakati akizungumza na mwanahabari kuhusu mradi huo ambao una lengo la kuwapatia elimu namna ya kujikinga na maambukizi kwa walemavu.
Alisema kuwa Watu wenye ulemavu sio tu wanakabiliwa na hatari kubwa ya COVID-19 kutokana na hali walizokuwanazo hivyo wanahitaji kwa kiasi kikubwa elimu kwa njia zote ambazo zinatakiwa kuweza kuwaelimisha kwani walemavu wamegawanyika katika makundi mbalimbali wakiwemo walemavu wa macho.
Alisema kuwa hatua maalum zahitajika kuwalinda wenye ulemavu na COVID-19 na kutoa wito kwa serikali kuhakikisha kwamba wanawalinda wenye ulemavu na wao kuwa makini katika kujilinda dhidi ya janga la virusi vya corona au COVID-19.
Kisinini alisema kuwa watu wenye ulemavu wako hatarini majumbani kwao na mitaani ambako fursa ya msaada wa kila siku na huduma zinaweza kuwa haba kutokana na hatua za kutotembea kwa kusalia majumbani na baadhi huenda wakaathirika sana kwa kutengwa au kuwa peke yao kutokana na janga hilo.
Alisema ni muhimu kuhakikisha taarifa kuhusu COVID-19 zinapatikana kwa muundo ambao watu wenye ulemavu wanaweza kuzipata ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa elimu mtandaoni kwani kwa sasa kila jambo linapatikana na kuwe na elimu kwa walemavu wa kutosikia ambao wanahitaji wakalimani kuwapa elimu.
Kisinini aliongeza kuwa changamoto nyingine wanayokabaliana nayo ni walemavu wa macho ambao wanahitaji zaidi msaidizi pindi ambapo wanapokuwa kwenye matembezi au kwenye kazi hivyo linapokuja suala la kunawa mikono hali hiyo ndio inazidi kwa kuwa hawezi ona sehemu sahihi iliyotengwa kwa ajili ya kunawa mikono na vitakasa mikono
“Changamoto kwa walemavu ni kubwa sana na moja wapo ni walemavu wa macho wanahitaji msaidizi kuweza kumsaidia lakini kutokana na janga hili la corona nina wasiwasi kuhusu ubaguzi na unyanyapaa dhidi ya watu wenye ulemavu wakati huu kwani hali halisi inaonekana kwa watu kuwa waoga kwa kila mmoja kuambukizwa.
Aliongeza kuwa ni vigumu kwa mlemavu wa macho kujua sabuni na maji yalipo au kujua kemikali ya kuosha mikono iko wapi wakati unataka kuosha mikono, kulingana na eneo waliopo hivyo kuwa katika uhatarishi zaidi hivyo kuna umuhimu wa idara za serikali kuweza kuwabaini walemavu wa macho na kuwapa msaada.
Wakati wa mafunzo yaliyofanyika hivi karibuni kwa walemavu, Mganga mkuu wa Manispaa ya Iringa, Dk. Jesca Leba alisema kwamba kutokana na hali walizonazo walemavu wa macho kuna umuhimu mkubwa wa jamii kuwa nao sambamba kwani wako katika hali ya hatari zaidi kutokana na hali zao za kutokuona hivyo elimu na kuwaongoza namna ya kunawa mikono itasaidia katika mapambano hayo.
Alisema kuwa kama manispaa wametoa mafunzo kwa walemavu na wataendelea kutoa mafunzo kwa makundi mbalimbali ya walemavu kwa ajili ya kushikwa mkono kwani changamoto kubwa kwenye vyombo vya kunawia mikono wanashindwa kuelewa mahali ilipo.
“Kwa kweli kuna changamoto kubwa kwa walemavu na ndio maana tumeamua kufanya mafunzo kwao tena maalum kwa kundi la walemavu wa macho na tutafanya mafunzo haya kwa makundi yote kwa sababu watu wanaohitaji kushikwa mikono katika kuwaongoza” alisema
Aidha katika mafunzo hayo, Dk Leba aliwataka walemavu wa macho kuepuka kushika macho, pua na mdomo kwa mikono isiyo safi kwa sababu mikono ni rahisi kubeba vimelea vya maradhi na kuzingatia ustaarabu wa kuzuia pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya.
Alisema kuwa endapo binadamu atahisi kuwa na mafua makali, homa, kikohozi na kushindwa kuhema nenda hospitali kupata msaada wa kitaalamu na kuepuka kuwa sehemu yenye msongamano kama vyombo vya usafiri, maduka na maeneo yenye mgandamizo wa hewa.
Mratibu wa Mradi Juu ya kupambana na kuenea kwa Virusi vya Corona kwa Walemavu mkoani Iringa unaofadhiliwa na Taasisi ya Foundation For Civil Society (FCS), Philemon Kisinini akizungumza na mwanahabari juu ya mradi wa kupambana na virusi vya corona kwa walemavu (picha na Denis Mlowe)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...