WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na
virusi vya corona (COVID-19) kwa sasa yamepungua na idadi ya wagonjwa waliopo
nchini hadi leo ni 66.
“Anayestahili
sifa katika hili ni Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa msimamo
wake usiotetereka na maono ya mbali aliyokuwa nayo ambayo yamekuwa chachu
katika kupunguza maambukizi ya COVID-19 na kulinda uchumi wa nchi.”
Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Juni
15, 2020) wakati akihitimisha shughuli za Mkutano wa 19 wa Bunge jijini Dodoma.
“Mheshimiwa Rais ameifanya
Tanzania iwe ya kupigiwa mfano duniani kwa namna alivyoshughulikia ugonjwa huu”.
Waziri Mkuu
amesema “nchi nyingi duniani zikiwemo nchi za bara la Afrika zilichukua hatua
kadhaa za kudhibiti maambukizi zikiwemo watu kutotoka ndani ya nyumba zao
(Lockdown), kuzuia mikusanyiko kwa kufunga shule, vyuo, michezo, aina zote za
usafiri wa ndani na nje, maeneo ya ibada na shughuli za uzalishaji mali na
viwanda vilifungwa.”
Waziri Mkuu
aliongeza kuwa Tanzania ilianza kuchukua hatua kadhaa ili kukabiliana na
maambukizi kwa kuunda Kamati tatu za ngazi ya Mawaziri, Watendaji na Wataalam
wa Afya kwa lengo la kufanya tathmini ya hatua za kuchukua ili kupunguza
maambukizi na kulinda anguko la kiuchumi. Hatua zilizochukuliwa ni kupunguza
misongamano kwa kufunga shule, vyuo, mikutano, kunawa maji, matumizi ya
vitakasa mikono na kuvaa barakoa.
“Siku ya
tarehe 22 Machi, 2020 Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, akiwa Jijini
Dodoma na tarehe 03 Mei, 2020 akiwa Chato aliwataka Watanzania wawe watulivu
waondoe hofu ya ugonjwa huu na waone ni ugonjwa kama magonjwa mengine, kama
vile Malaria, UKIMWI, Kifua Kikuu na akawataka Watanzania wachukue tahadhari na
kuendelea na shughuli za uzalishaji mali, kufanya kazi ofisini, viwandani, mashambani
na kutofunga nyumba za ibada.”
Waziri Mkuu amesema Rais Dkt.
Magufuli alihutubia tena Taifa tarehe 16 Aprili, 2020 kwa kutoa maelekezo na
kusisitiza mambo matano ambayo ni pamoja na kuwasihi Watanzania kuondoa hofu
kwa kuwa Mwenyezi Mungu yupo nasi na hivyo, waendelee kuchapa kazi ili kunusuru
uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla na kuzingatia kanuni za afya.
Pia, aliwataka Watanzania watumie
siku tatu kumuomba na kumlilia Mwenyezi Mungu kwani Mungu yu pamoja nao na
atawasikia huku akiendelea kusimamia kauli yake ya kuwataka Watanzania wafanye
kazi kwa bidii na kumtegemea Mungu bila kujali kauli za kebehi na ukosoaji kutoka
pande mbalimbali za dunia.
Waziri Mkuu amesema Rais Dkt.
Magufuli aliwahimiza Watanzania wamtegemee Mwenyezi Mungu na kwamba Mwenyezi
Mungu pekee ndiye atakayewavusha na kuwaepusha na janga hilo. Pia, aliwahimiza
Watanzania kutopuuza umuhimu wa tiba mbadala katika mapambano dhidi ya COVID-19.
“Kauli hii, imekuwa chachu katika kuimarisha tafiti za dawa za asili ambazo
zimekuwa na mchango mkubwa katika kupambana na maradhi mbalimbali ikiwemo COVID-19”.
Amesema Waziri Mkuu.
Vilevile, Waziri Mkuu amesema Mei 20,
2020 akiwa Singida, Rais Dkt. Magufuli aliwaomba Watanzania watumie siku tatu
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa maajabu aliyoyafanya kwa Taifa la Tanzania kwa
kuliepusha na kusambaa kwa virusi vya COVID-19.
Amesema suala
la kudhibiti maambukizi ya COVID-19 litaendelea kuwa kipaumbele cha Serikali
kwa sasa sambamba na malengo ya muda mrefu ya kumaliza ugonjwa huo hususan
katika kipindi hiki ambacho WHO imebainisha kwamba si wa kuondoka mara moja
watu wajifunze kuishi nao.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Juni
9, 2020 Bunge lilipitisha Azimio la kumpongeza na kumuunga mkono Rais Dkt. John
Pombe Magufuli kwa namna alivyomudu kuivusha nchi katika janga la COVID-19.
Waswahili husema mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni.
“Katika
hili, nami naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa hotuba zake zote zilizohusu
ugonjwa huu ambapo alihimiza masuala muhimu kwa Watanzania katika kukabiliana
na janga hili na hivyo, kuondoa hofu na taharuki iliyokuwa imetanda kwa
Watanzania.”
“…leo
tunaona idadi ya wagonjwa wanaougua imepungua sana. Kwa mfano, taarifa ya leo,
Jumatatu tarehe 15 Juni, 2020 inaonesha kuwa tuna wagonjwa 66 kutoka katika
mikoa 10 huku mikoa mingine 16 ikiwa haina wagonjwa.”
Pia, Waziri
Mkuu ametoa pongezi maalum kwa Viongozi wa dini kwa namna walivyoshirikiana na
waumini katika mapambano ya ugonjwa wa COVID-19. Wakati wote viongozi hao
wamekuwa wakiwapatia faraja waumini na wagonjwa kwamba Mwenyezi Mungu
atawaponya. “Hatua hizo zimekuwa mhimili mkubwa wa upendo, umoja, mshikamano na
ujasiri miongoni mwa Watanzania. Tunawashukuru sana.”
Amesema taarifa
iliyotolewa na Taasisi ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (Organisation
for Economic Cooperation and Development - OECD) inabashiri kuwa kitendo cha
kuwafungia watu ndani yaani “Lockdown”
kitasababisha kusinyaa kwa uchumi wa nchi zilizoendelea kwa asilimia mbili kila
mwezi.
“Hivi sasa,
nchi nyingi zinakubaliana kuwa “Lockdown”
si hatua sahihi ya kukabiliana na COVID-19. Vilevile, kisayansi inakadiriwa
kuwa nchi ambazo ziliwafungia watu wake na mipaka yake zipo katika hatari ya
kukumbwa na madhara makubwa ya ugonjwa huo pindi utakapotokea mlipuko wa pili
na hata wa tatu.”
“…kwa
mantiki hiyo, mtizamo na hatua zilizochukuliwa na Tanzania katika kupambana na
COVID-19 zinaonesha upekee tulionao kama nchi. Serikali, inayo kila sababu ya
kuwapongeza Watanzania ambao si tu walipokea maelekezo ya Serikali lakini pia
walifanya hivyo kwa uaminifu mkubwa na kwa hiari yao wenyewe bila kushurutishwa
na mamlaka yoyote ya nchi.”
Waziri Mkuu
ametumia fursa hiyo kumpongeza Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Ummy Mwalimu, Katibu Mkuu, Mganga Mkuu wa Serikali pamoja na
wataalamu wa afya kwa usimamizi wa tatizo hilo kwani walitekeleza majukumu yao
bila kujali hatari ya virusi hivyo kwa maisha yao na wapendwa wao.
Vievile, Waziri
Mkuu ameishukuru sekta binafsi, mtu mmoja mmoja na wadau wote ambao waliitikia
wito wa Serikali kwa kutoa michango ya hali na mali katika kufanikisha vita
dhidi ya COVID-19 nchini. Pia wamiliki wa viwanda ambao waliitikia wito wa
Mheshimiwa Rais na kuanza kuzalisha vifaa kinga hapa nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...