Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar, Mahamoud Thabit Kombo akizungumza katika kikao na ujumbe
wa juu wa watendaji wa Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora (kushoto), Watendaji Wakuu wa Wizara hiyo(kulia),
pamoja na waandishi wa habari katika ziara ya tume hiyo iliyofanyika Zanzibar.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (wa pili kushoto), akifafanua jambo kwa Waziri
wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mahamoud
Thabit Kombo( kulia) katika ziara ya tume hiyo iliyofanyika Zanzibar.
Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar, Mahamoud Thabit Kombo, akipokea mpango mkakati wa Tume ya haki
za Binadamu na Utawala Bora ya mwaka
2018/2023 kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu katika
ziara ya uongozi wajuu wa tume iliyofanyika Zanzibar.
Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar, Mahamoud Thabit Kombo, akiwa kwenye picha ya pamoja
ujumbe wa watendaji wa juu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora katika
ziara ya tume hiyo iliyofanyika Zanzibar.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu akizungumza na Waandishi (pichani), katika
Ofisi za Habari, Utalii na Mambo ya Kale za Serikali ya Mapinduzi
Zanzibarkatika ziara ya tume hiyo iliyofanyika Zanzibar.
====== = ======== ======= =======
Na. Mwandishi Wetu-MAELEZO.
Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Mahamoud Thabit Kombo amesema kuwa tume ya haki
za binadamu ina wajibu mkubwa wa kufanya kazi na wanahabari, pamoja na Mamlaka
la Mawasiliano nchini (TCRA) kwa kuwa sekta hizo ni kiungo muhimu katika
utekelezaji wa haki za binadamu.
Akizungumza na ujumbe wajuu wa Tume hiyo wakiongozwa
na Mwenyekiti, Waziri Kombo alisema kuwa ugeni huo ni muhimu sana kwani habari
huchochea upatikanaji wa haki za binadamu kwa kuibua mambo mbalimbali ambayo
yako kinyume na haki za binadamu.
“Tume ya Haki za Binadamu wamekuja kututembelea sisi
kwa sababu sekta ya habari ni kiungo kimoja wapo kikuu katika haki za binadamu
na utawala bora kwa mujibu wa sheria na kanuni za haki za binadamu kimataifa na
miongoni mwa mambo tuliyoyazungumza ni kusisitiza tume hii kututembelea mara
kwa mara”, Waziri Kombo.
Alisema, kuwa mkutano wake na tume hiyo pamoja na
waandishi wa habari ni faida kubwa kwa pande zote kwani utaleta kujifunza jinsi
ya utekelezaji wa haki za binadamu ikiwemo upatikanaji wa habari kwa jamii
ambayo nayo ni moja ya haki za binadamu duniani.
Alibainisha, kuwa tume hiyo inawajibu mkubwa wa kuona
masuala ya haki za mtandao yanaenda vyema ili kuwezesha upatikanaji wa haki za
binadamu kwa kila mtu kutumia mtandao kwa kuzingatia sheria na haki za kila
mtu.
“Lakini pia tulizungumza masuala ya matumizi ya
mtandao, kwa sababu kwa siku za karibuni masuala haya yanavunja haki za
binadamu kwani watu wamekuwa wakitumia vibaya kutukana na kuwazalilisha wenzao
hususani viongozi, hadi viongozi wajuu kabisa wanatukanwa lakini hakuna
usimamizi wa haya mambo kwa hiyo tume mkifanya kazi pamoja na Mamlaka ya
Mawasiliano nchini (TCRA), mtatusaidia upatikanaji wa haki kwenye masuala
hayo”, Waziri Kombo.
Aidha, alisema kuwa masuala ya udhibiti wa redio,
televisheni na magezeti uko vizuri ila masuala ya mtandao ndiyo yamekuwa ni
magumu kidogo kwenye utekelezaji wa haki za binadamu kwani masuala haya yanatoa
haki na uhuru wa kujieleza lakini uhuru huo umekuwa ukitumika vibaya kwa baadhi
ya watu na kusababisha uvunjaji wa haki za binadamu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu, Jaji Mstaafu Mathew
Mwaimu alibainisha lengo la ziara hiyo visiwani Zanzibari kuwa ni kuona jinsi
gani tume hiyo inajijenga kwa kupata mahusiano mazuri kutoka kwa Serikali na
Taasisi zake ili kuwezesha utekelezaji wa haki za binadamu kuwa rahisi.
“Lengo letu kubwa katika Wizara ya habari ni kujua
utekelezaji wa haki za binadamu, tujue kwamba tunapozungumza haki za binadamu
vilevile haki za watu kupata habari na haki za vyombo vya habari kutoa habari
za utekelezaji wa haki za binadamu kwa uwazi zaidi”, Jaji Mstaafu Mwaimu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...