"USHUHUDA WA UTAJIRI NA UTALII WA KIHISTORIA ULIOPO KISARAWE"
Na Jokate Mwegelo, DC Kisarawe
WAUKAE ,Jumamosi ya Julai 28,2018 majira ya saa
10 alasiri, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli aliniteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe.
Hakika ilikuwa siku ya kihistoria kwangu, hasa
kwenye safari yangu ya kisiasa na uongozi nchini. Uteuzi huu umenipa nafasi ya
kutumia na kuonesha vipaji vyangu vya kiuongozi.
Sikuwahi kudhania kuwa ipo siku nitakuwa Mkuu wa
Wilaya, ilikuwa ni siku njema. Ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa mapenzi yake
kwangu na pia ninaendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniamini.Mengine
mengi juu ya siku hii adhimu nitaongelea siku nyingine, nikiwiwa.
Nikiri wazi, sikuwahi kufika Kisarawe kabla ya
uteuzi wangu. Hivyo basi, kabla ya kula kiapo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Pwani Injinia Evarist Ndikilo wilayani Kibaha Agosti 3, 2018, nilijaribu
kufanya utafiti kidogo kwa kushirikiana na timu yangu ya kipindi kile katika
kujaribu kutengeneza vipaumbele ambavyo ningeanza navyo mara baada ya kuanza
kazi rasmi.
Wajumbe kadhaa walifika mpaka Kisarawe na kuhoji
wananchi mbalimbali sambamba na kujionea mazingira kwa ujumla. Moja kati ya
vitu tulivyoweza kuibuka navyo ni utajiri wa historia na vivutio vya kiutalii
vilivyopo ndani ya Wilaya ya Kisarawe.
Nilianza kazi rasmi tarehe Agosti 6, 2018, kwa
bahati na kwa mapenzi ya Mungu, siku hiyo kazi niliianzia msituni hivyo
nilipata nafasi ya kuanza kuiona Kisarawe na utajiri wake.
Tuliingia hifadhi ya msitu wa Ruvu Kusini, hii
ni hifadhi ya msitu ambayo ni kubwa zaidi kwenye ukanda huu wa pwani ikiwa na
ukubwa wa hekta 30,633.
Tukumbuke kuwa hifadhi hizi za misitu na hasa
hifadhi za msitu wa Pugu na Kazimzumbwi ndizo zinazosaidia kuchuja hewa ukaa
iliyopo katika jiji la Dar es Salaam ambalo lipo karibu sana na wilaya ya
Kisarawe, hivyo utajiri wa Kisarawe una maana kubwa kwa nchi yetu.
Siku hii ilikuwa ni nafasi muhimu kwangu ya
kujithibitishia utajiri uliopo katika wilaya ya Kisarawe na jinsi gani tunaweza
kuibua fursa mbalimbali za maendeleo na hasa kwenye sekta ya utalii ambayo
inachangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa na kuingiza fedha za kigeni.
Ijumaa ya Mei 29,2020, ikiwa imepita mwaka moja na miezi
kumi tangu nilipoteuliwa na Mhe. Rais, nikiwa na timu ya chama cha waongoza
utalii kusini tuliamua kufanya ukaguzi wa barabara kuelekea hifadhi mpya ya
taifa ya Mwalimu Nyerere na pia kujaribu kuibua fursa za kiutalii njiani.
Katika hili naomba kupigia chepuo kidogo
barabara hii; barabara hii ndio njia fupi zaidi takribani kilometa 155 kutoka
Uwanja wa Ndege wa Kimaitaifa wa Julius Nyerere kwenda kwenye geti la Mtemere
Mloka, Rufiji kuingia kwenye mradi wa kufua umeme wa bwawa la Nyerere na kwenye
Hifadhi mpya ya Taifa ya Mwalimu Nyerere.
Hivyo, kama viongozi wa wilaya kwa kushirikana
na wenzetu kutoka TANROADS tumekuwa tukifanya jitihadi mbalimbali za kuboresha
viwango vya barabara hiyo ikiwa ni pamoja na kuifungua tena rasmi hii barabara
kuanzia November 2018 ili iweze kuanza kutumika.
Haya turudi kwenye safari yetu, moja ya sehemu
tulizosimama ilikuwa ni Boga; Boga ni kata mpya iliyozaliwa kutoka katika kata
kongwe ya Maneromango. Katika Kata ya Boga kuna sehemu wenyeji wanachonga
vinyago kwa kutumia miti ya mpingo inayopatikana mbele kidogo kwenye eneo moja
linaloitwa Boga Sangamzelu.
Pamoja na kuchonga vinyago, kuna huduma ya
chakula cha asili ambacho ni kivutio kizuri kwa watalii wanaopita hii njia
kuelekea kwenye hifadhi ya taifa ya Mwalimu Nyerere.
Katika ziara hii, sehemu iliyonisisimua zaidi ni
eneo la Mtunani ambapo kuna mlima na bonde kubwa sana. Ukiwa sehemu ya juu
kabisa ya mlima ukitazama upande wa Kusini Magharibi unaiona wilaya ya Rufiji
na bonde lake, upande wa machweo (magharibi) na upande wa Kaskazini Magharibi
ni bonde la Selous na Mkoa wa Morogoro unaona mpaka milima ya Uluguru. Hakika
inavutia mno!
Sasa leo naomba nielezee kidogo historia nzuri
sana niliyoikuta kwenye huu mlima ambao ni chimbuko la maeneo maarufu kama
Shule ya Kibasila Dar es Salaam, Kikosi cha Jeshi Kibasila Kisarawe na eneo la
Kamata jijini Dar es Salaam.
Historia inaeleza kuwa kijiji cha Kisangire
kilikuwa na tawala ya kimila iliyokuwa chini ya kabila la Kizaramo. Kisangire
kabla ya kuja Mjerumani mtawala alikuwa Chifu Kibasila, kipindi cha vita ya
Majimaji iliposhika kasi wajerumani walikimbilia Rufiji na huko walitembea pori
kwa pori na kufika kijiji cha Kisangire hapo ndipo walikutana na Chifu Kibasila
ambaye alikuwa na utawala wake katika kijiji hicho.
Historia inaeleza kuwa Chifu Kibasila alikuwa
mkarimu mno hivyo alimkaribisha Mjerumani katika himaya yake. Chifu Kibasila
kwenye eneo lake alipanda miti ya aina mbalimbali ikiwemo miembe, minazi,
mikungu na miti mingine ya matunda, pia shughuli za kilimo ziliendelea kwenye
mashamba ya Chifu huyo yaliyokuwepo katika himaya yake.
Historia inaonesha kuwa kilichomfanya Mjerumani
kufika Kisangire akitokea Utete Rufiji wakati Vita vya Majimaji imepamba moto
ni kutokana kuwa eneo la Kisangire lilikuwa mlimani hivyo kwa Wajerumani
Kisangire lilikuwa eneo muhimu kwao kwa mikakati ya kivita.
Tukumbuke kuwa vita vya Majimaji iliongozwa na
viongozi wa kimila kama Kinjeketile Ngwale na wengineo. Mjerumani alipofika
kijiji cha Kisangire aliomba hifadhi kwa Chifu Kibasila naye alimkubalia, baada
ya kukaa muda mrefu Mjerumani alianza kuita Wajerumani wenzake waje eneo la
Kisangire.
Hapo ndipo mvutano kati ya Chifu Kibasila na
Wajerumani ulipoanza na hatimaye Chifu Kibasila kushindwa na hivyo akaamua
kuikimbia himaya yake kutokana na kuzidiwa mbinu za kivita na Wajerumani.
Mjerumani akaanza kutawala kwa nguvu kwa kutoza
kodi ya kichwa kwa wananchi, na kama mwananchi alishindwa kulipa kodi ya kichwa
alikamatwa na kulazimishwa kufanya kazi ngumu au kuchapwa viboko 25 kwa kutumia
kiboko kilichotengenezwa kwa ngozi ya kiboko.
Kiboko hicho kiliitwa "Henzerani"
ambapo historia inaeleza kuwa kiboko hicho kikifika kwenye mwili wa mtu
kilikuwa kinatoa na nyama katika mwili wa mtu huyo. Kitendo cha watu wa
Kisangire kuchapwa viboko kuliongeza mgogoro kati ya Mjerumani na Chifu
Kibasila.
Japo Chifu Kibasila alijiimarisha na alionesha
upinzani mkubwa, Mjerumani alifanikiwa kutawala eneo hilo la Kisangire na
kujenga ngome yake iliyokuwa na mahandaki ya kujificha yeye na askari wake
wakati wa vita.
Inaelezwa kuwa baadhi ya mahandaki yalichimbwa
na kutokea Utete, Rufiji. Mjerumani alijiimarisha akajenga makazi yake vizuri
akawa na mahabusu, sehemu ya kuabudia, na mti wa mwembe uliotumika kunyongea
wale waliopinga utawala wake.
Mwembe huo ulikuwa maarufu kama mwembe kinyonga
ambapo wale waliondelea kukaidi amri alizotoa Gavana wa Kijerumani wakati huo
walikatwa vichwa mbele za watu na wengine walinyongwa.
Ili kujiimarisha zaidi, Mjerumani akamua kujenga
daraja kwa kuunganisha milima miwili kwa mawe na vifusi. Wananchi
walilazimishwa kujenga daraja hilo lililounga milima miwili kwa mateso makali
sana.
Wananchi waliamua kuliita daraja hilo
"Daraja la Mungu" kwa sababu ya mateso makali waliyoyapata.
Walipokuwa wakifanya kazi, jioni baada ya kumaliza kazi za siku hiyo walilipwa
ujira wa pesa rupia mbili, pesa hizo zote zilitumika kulipa kodi ya kichwa kwa
Mjerumani huyo huyo.
Historia ya Chifu Kibasila haikuishia hapo, bado
aliendelea kupambana kwa muda hadi pale watawala wenzake walipomgeuka. Maliwali
walionunuliwa na Mjerumani wakamgeuka Chifu Kibasila na hivyo kumpelekea
taarifa za uongo Chifu Kibasila kuwa -Mjerumani anataka tukae chini tukubaliane
ili tuache vita- kumbe hawa maliwali ambao majina yao yalikuwa Kiwambwa na Chaurembo
walikuwa wamenunuliwa na yeye pasina kujua alikubali ombi hilo la kukutana na
Mjerumani.
Hivyo ndivyo Chifu Kibasila alivyokamatwa na
kupelekwa Dar es salaam eneo la KAMATA ili anyongwe. Jina hilo la KAMATA
limetokana na kukamatwa kwa Chifu KIBASILA na kunyongwa Dar es Salaam katika
eneo hilo.
Kwa heshima ya Chifu Kibasila palianzishwa Shule
ya Sekondari Kibasila katika jiji la Dar es salaam, na kambi ya Jeshi ya JWTZ
ya Kibasila Kisarawe ambavyo vyote bado vipo hadi leo.
Utawala wa Mjerumani uliimarika sana pale
Kisangire hadi Vita ya Kwanza ya Dunia kati ya mwaka 1914 hadi 1918. Kwa wilaya
ya Kisarawe kambi kubwa ya Mjerumani ilikuwa Kisangire. Wakati wa vita hiyo ya
Kwanza Mwingereza alipambana vikali na Mjerumani lakini ngome ya Kisangire
ilikuwa haingiliki kutokana na eneo ilipojengwa ngome hiyo sambamba na uhodari
wa askari wa Mjerumani.
Mwingereza aliomba msaada kutoka maeneo mengi
lakini hakuweza kushinda vita katika eneo hilo ndipo kamanda wa Waingereza
bwana Hugh Charles Clifford (Alifariki 15.11.1916 kamanda huyu) alipoungana na
Wazaramo wa Mtunani kuishambulia ngome ya Mjerumani Kisangire.
Wananchi hao walimsaidia kamanda huyo wa
Kiingereza kujua njia za maficho zinazoweza kumfikisha kwenye ngome ya
Mjerumani. Lakini kabla hawajafika kwenye ngome ya Kisangire walimuonesha
kamanda huyo eneo ambalo anaweza akaipiga ngome hiyo akiwa mbali kabla ya
kuivamia na kupandisha bendera ya Mwingereza.
Hugh Charles Clifford alitumia guruneti
akaliweka kwenye pacha ya mti wa mbuyu uliopo Mtunani na kuishambulia ngome
hiyo.Baada ya kujihakikishia kuwa amepiga ngome akaamua kwenda kwa uongozi wa
wananchi wa Mtunani kutoa shukrani.
Kamanda wa Waingereza alifikiri Mjerumani
amekimbia kwenye ngome yake baada ya mashambulizi kadhaa hivyo, kwa bahati
mbaya ile anaingia ndani tu kumbe askari wa kijerumani alikuwa amejificha ndipo
walipokutana uso kwa uso wakashambuliana na wote wakafa hapo hapo.
Waingereza
waliona umuhimu kwa askari wao kuzikwa Mtunani kutokana na msaada waliopata
kutoka kwa Wazaramo.Hivyo walimpasua kamanda Hugh Charles Clifford
tumbo wakachukua vitu vya ndani wakazika pale kijijini na mwili waliutia chumvi
na kuusafirisha mpaka Uingereza kwa mazishi.
Wenyeji baada ya kuona Waingereza wamewapa
heshima hiyo waliamua kuunda kitongoji cha Pangala la Mwingereza, neno hili ni
la Kizaramo ambalo maana yake ni Kaburi la Mwingereza.
Kwa lugha ya Kizaramo Pangala ni 'Kaburi', lakini.
Kutokana na muingiliano wa jamii neno hili limebadilika badala ya kuwa
"Pangala la Mwingereza" panaitwa "Panga la Mwingereza."
Kaburi hilo la kamanda Hugh Charles Clifford lipo hadi leo.
Siku ukifika Kisarawe utafurahi kuona mandhari
mazuri na historia tamu ya Kisarawe kama hii niliyosimulia leo. Karibu ujionee.
Ila pia kuna la kujifunza kutokana na historia
fupi ya Chifu Kibasila. 1, unaweza kumtendea mtu wema, ukamkarimu lakini
wakatumia ule ukarimu kukuumiza. 2, huu ni msemo wa siku nyingi na hata Mr.
Nice aliwahi kuimba- kikulacho ki nguoni mwako, Chifu Kibasila alisalitiwa na
wenzake.
3, Waafrika tulikosa mshikamano Chief Kibasila alimkaribisha Mjerumani
licha ya vuguvugu la kumkataa huko kusini- ila mwisho wa siku nayeye
akashughulikiwa hakukuwa na mshikamano kati ya viongozi wa kimila.
Hata leo tunaona jinsi watu wenye nguvu ni
rahisi kupenyeza ajenda zao kwasababu ya tamaa ya baadhi ya watu na kukosekana
kwa mshikamano na uzalendo. Waafrika hatuwezi kuendelea pasi na mshikamano wa
kweli. Tunachosahau ni kwamba kwa kutojitambua kwetu ndio maadui wanapenya na
kutumaliza zaidi.
Imeandaliwa na;
Jokate Urban Mwegelo- DC Kisarawe
Kennedy Muhoza- Ofisa Utalii Kisarawe.
Hifadhi ya Msitu Ruvu Kusini
Kijiji cha Boga
Milima ya Pugu-Hifadhi ya Msitu
Milima ya Pugu-Hifadhi ya Pugu 2
Milima ya Pugu-Hifadhi ya Pugu-2
Milima ya Yombo Lukinga
Mlango wa Handaki kutoka kwenye jengo la Utawala la Mjerumani
Mto Kiimbwa -Jokate na Jumuiya ya waongoza wa watalii ukanda wa Kusini
Mtunani
Boma la Mjerumani Kisangire
Hifadhi ya Msitu Ruvu Kusini
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...