Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu (kulia) akionesha mwongozo wa taifa wa matibabu kwa watu wenye Sikoseli mara baada ya uzinduzi, kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Taifa Muhimbili prof. Lawrence Museru leo jijini Dar es Salaam
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akiwa na viongozi mbalimbali wa Wizara hiyo pamoja watoto wakionesha mwongozo wa taifa wa matibabu kwa watu wenye Sikoseli mara baada ya kuuzindua, leo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya watoto wenye Sikoseli waliohudhuria maadhimisho ya siku ya siku ya Sikoseli duniani yanayofanyika kila Juni 19, leo jijini Dar es Salaam.
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kuwa ni vyema vijana kabla ya kuanzisha mahusiano au kuoana ni vyema wakapima vinasaba vya Sikoseli (Seli mundu) ili kupunguza changamoto zinazowakumba watoto wanazaliwa na vinasaba hivyo.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati maadhimisho ya siku ya siku ya Sikoseli duniani iliyobeba kauli mbiu ya "Huduma Bora kwa kila Mhitaji,Chukua Hatua, Panua Wigo." Waziri Ummy amesema kuwa hiyo ni fursa kwa Wizara ya Afya Katika kujipima na kuboresha sekta hiyo huku wajibu wa kupunguza madhara ukielezwa ni wa kila mmoja kuanzia ngazi ya familia hasa kwa vijana wanaoanzisha mahusiano na ndoa kwa kupima vinasaba vya Sikoseli ili kuokoa watoto dhidi ya Sikoseli.
"Kila siku watoto 1000 huzaliwa na Sikoseli duniani, na hapa nchini watoto kumi na moja elfu huzaliwa na Sikoseli kila mwaka, na nchi yetu ni nchi ya nne duniani kwa kuwa na watoto wengi wanaozaliwa na Sikoseli lakini changamoto hizi tunaweza kuzimaliza kwa kushirikiana sote katika jamii" ameeleza Waziri Ummy.
Aidha amesema kuwa licha ya kuwa na changamoto za kitakwimu tafiti katika utatuzi zinafanyika huku akieleza kuwa vifo vya watoto vinavyosababishwa na Sikoseli vinakadiriwa kuwa kati ya asilimia 5 hadi saba.
Vilevile amewaagiza waganga wakuu wa hospitali za Mikoa na Wilaya kusimamia huduma zinazotolewa kwa wagonjwa wa Sikoseli katika hospitali hizo na hiyo ni pamoja kuanzisha kliniki maalumu za kuwahudumia wagonjwa wa Sikoseli na pia kushusha huduma za utambuzi katika zahanati na vituo vya afya.
Waziri Ummy pia ameagiza Mamlaka husika kuweka kipaumbele kwa kundi hilo kwa kuhakikisha wanapata damu salama na siku si nyingi watazindua mpango wa upakindizaji uloto na wale wenye Sikoseli watakaopandikizwa hawatalazimika kutumia dawa.
Awali akitoa takwimu Mkurugenzi wa hospitali ya Taifa Muhimbili prof. Museru amesema kuwa kliniki ya Sikoseli hospitalini hapo hupokea watoto 50 hadi 70 kwa siku na takribani watoto 200 hadi 300 kwa mwezi na kwa watu wazima kuanzia miaka 14 na kuendelea huwa 30 hadi 40 kwa siku huku wote wakiwa na changamoto za kuumwa kifua na mifupa.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Abel Makubi amesema kuwa upatikanaji wa dawa bado ni ghali kwa watoto wa watu wazima na kueleza kuwa Sikoseli ni moja ya ugonjwa usioambukiza unaochangia asilimia 70 ya vifo vinavyotokea ulimwenguni huku na kushauri ushirikiano zaidi ili kupunguza changamoto hizo.
Maadhimisho hayo yalienda sambamba na uzinduzi wa mwongozo wa taifa wa matibabu kwa watu wenye Sikoseli.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...