MKUU
wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Mhandisi Zephania Chaula
amezindua hospitali ya Wilaya hiyo hivyo waliokuwa wakisafiri umbali wa
zaidi ya kilomita 180 hadi 200 kufuata huduma hiyo jijini Arusha au
Mkoani Kilimanjaro wataondokana na adha hiyo.
Mhandisi
Chaula akizungumza jana wakati akizindua hospitali hiyo alimshukuru
Rais John Magufuli kwa kuwapatia fedha za ujenzi huo uliogharimu
shilingi bilioni 1.8 zilizotumika hadi sasa.
Alisema
tangu wilaya hiyo ianzishwe mwaka 1994 haikuwa na hospitali ya wilaya
ila hivi sasa Rais Magufuli alitoa fedha hizo na kujengwa kati ya
hospitali mpya 67 zilizojengwa nchini na nyingine 27 za awamu ya pili.
Aliwashukuru
wananchi wa kijiji cha Nadosoito kata ya Langai kwa kutoa ekari 50 kwa
ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo mpya ya wilaya.
"Kipekee
nimpongeze mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hii Yefred
Myenzi kwa usimamizi wake mzuri hadi kukamilika kwa hospitali hii ambayo
leo (jana) ninazindua," alisema Chaula.
Alisema
awali baadhi ya wananchi wa kijiji hicho hawakutaka kutoa eneo hilo
wakidai kuwa diwani wao Jackson Sipitieck ameuza kwa serikali jambo
ambalo siyo kweli kwani serikali imelichukua bila kulipia.
Mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Yefred Myenzi alisema majengo
saba ya hospitali hiyo yamekamilika kwa ajili ya kutoa huduma za afya
kwa wananchi wao.
Myenzi alisema hospitali hiyo ina majengo ya utawala, wodi ya wazazi, wagonjwa wa nje, famasi, la kufulia, mionzi na maabara.
Mwenyekiti
wa halmashauri ya wilaya hiyo, Jackson Sipitieck alisema baraza la
madiwani lilipitisha azimio la kila kata kuchangia shilingi milioni 3.5
kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za madaktari.
Sipitieck
alisema wananchi wa kijiji cha Narosoito kata ya Langai wameibeba
wilaya hiyo kwa kutoa eneo hilo na kujengwa hospitali hiyo
itakayowanufaisha kizazi cha sasa na kijacho.
Mkazi
wa eneo hilo Martha Okida alimshukuru Rais Magufuli kwa kutoa fedha za
ujenzi huo kwani waathirika wakubwa wa ukosefu wa hospitali ya wilaya
walikuwa wanawake na watoto.
Okida
alisema hivi sasa hakuna haja ya kusafirishwa wagonjwa kwani huduma za
hospitali ya Wilaya zitakuwa zinapatikana hapo tofauti na awali.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi
Zephania Chaula akipima afya yake wakati wa uzinduzi wa huduma ya
hospitali mpya ya wilaya hiyo iliyopo Kata ya Langai.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...