Na Mwandishi Wetu, Manyara
MWENYEKITI
wa chama cha wachimbaji wa madini Mkoani Manyara, Justin Nyari amesema
watamuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu mbunge wa Jimbo la
Simanjiro James Ole Millya (CCM) aliyemaliza muda wake kutokana na namna
alivyokuwa anawatetea Bungeni wachimbaji madini ya Tanzanite.
Nyari
aliyasema hayo jana mji mdogo wa Mirerani kwenye kikao cha wachimbaji
wa madini ya Tanzanite cha kujadili mikakati mbalimbali ya uchimbaji
ikiwemo usalama migodini na kuchangia chama hicho.
Alisema
wachimbaji madini wa mkoa huo wanatambua jitihada za dhati za Ole
Millya alipokuwa anawatetea bungeni hivyo ili kurudisha fadhila kwake
watamuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba 25
mwaka huu.
Alisema
wanatambua vikwazo mbalimbali alivyokuwa anavipata Ole Millya lakini
alisimama kwa miguu miwili na wachimbaji wadogo wa madini hivyo
watahakikisha wanamuunga mkono ili arudi bungeni kuendelea kuwatetea.
"Mchezaji
mahiri ni yule ambaye anacheza vizuri uwanjani na anasaidia timu kupata
ushindi hivyo hatuna sababu ya kuchagua mbunge mwingine ili hali huyu
tuliyekuwa naye alikuwa anatusaidia sisi wachimbaji madini," alisema
Nyari.
Alisema
wachimbaji madini wanatambua kuwa Ole Millya alikuwa halali usingizi
pindi wakimshirikisha matatizo mbalimbali ya wachimbaji madini hivyo cha
kumlipa ni kuhakikisha wanaendelea kumuunga mkono ili achaguliwe tena
kuongoza jimbo hilo.
Kaimu
ofisa madini mkazi wa Mirerani, Hamis Kamando alisema Ole Millya ni
kiongozi makini kwani walifanya kazi mbalimbali wakati mbunge huyo akiwa
mjumbe wa kamati ya bunge ya nishati na madini.
"Waziri
wa madini Dotto Biteto, Naibu waziri Stanslaus Nyongo na mbunge wa
jimbo la Simanjiro Ole Millya nawaombea washinde uchaguzi wao kwani ni
viongozi mahiri wenye uzalendo wanaotanguliza mbele maslahi ya Taifa,״
alisema Kamando.
Kwa
upande wake, Ole Millya alisema anashukuru namna wachimbaji madini
walivyoshirikiana naye wakati akiwa bungeni na kuhakikisha wanapata haki
zao na ataendelea kuwa nao kwani ana imani kubwa atachaguliwa tena kuwa
mbunge wa jimbo la Simanjiro.
"Namshukuru
kila mchimbaji niliyeshirikiana naye katika kutetea wachimbaji wadogo
ikiwemo Marema, Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani Adam
Kobelo na Mwenyekiti wa Tamida Sammy Mollel kwa kweli tulipambana,״
alisema Ole Millya.
Alisema
anampongeza Rais John Magufuli kwa namna anavyowajali wanyonge hasa
wachimbaji wadogo kwani alipojenga ukuta kwa ajili ya kulinda rasilimali
za nchi baadhi walichukia hilo lakini kutokana na mafanikio
yanayopatikana wote wamekubali.
Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa
Manyara, Justin Nyari akizungumza na wamiliki wa migodi ya Tanzanite
kwenye kikao kilichofanyika ukumbi wa Kazamoyo kwa Luka Mji mdogo wa
Mirerani Wilayani Simanjiro jana.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...