Na Said Mwishehe, Michuzi TV, Tabora
MBUNGE Mteule wa Jimbo la Bukene mkoani Tabora Selemani Zedi amesema kwa niaba ya wananchi wa jimbo hilo wanatoa salamu za pongezi pamoja na shukrani kwa Rais Dkt.John Magufuli kutokana na kupeleka maendeleo jimboni humo.
Zedi ameyasema hayo leo mbele ya Rais Dkt. Magufuli ambaye kwa sasa ni Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu alipokuwa katika mkutano wa kuomba kura Nzega Mjini ambapo maelfu ya wananchi walihudhuria.
”Nimesimama mbele yako Rais Magufuli kwa niaba ya wananchi wa jimbo la Bukene kutoa salamu za shukrani na pongezi kwa mambo makubwa uliyotufanyia, chini ya utawala wako leo hii Bukene kuna barabara za lami ambazo zinatuunganisha na maeneo mengine ya Tabora.
Kwa sasa kuna fedha Sh.milioni 789 ambazo zimepitishwa na Bunge kwa ajili ya kufanya usanifu wa kina, Usanifu wa kina umekamilika , kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kiwango cha lami,”amesema Zedi.
Kuhusu huduma ya maji , Zedi amefafanua kazi kubwa ambayo inafanyika ambapo ameuzungumzia mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria kuja Tabora na kisha kufika jimbo la Bukene.
”Umetupatia mradi wa Sh.bilioni 6.5 kutoa maji tanki la Ushirika mpaka Bukene Mjini umbali wa kilometa 36,mradi huu utasaidia vijiji zaidi ya 20 na hayo ni mafanikio makubwa,”amesema Zedi.
Ameongeza kuwa jambo la tatu ambalo Rais Magufuli amelifanya na sasa wanamshukuru ni kuingiza umeme vijiji vyote 82 kwenye mpango wa Mradi wa Umeme Vijijini(REA).Pia kata 13 kati ya 17 za Bukene tayari zina huduma ya umeme na zimebakia kata nne tu.”Kwa hayo makubwa sisi wananchi wa Jimbo la Bukene tutafanya kampeni kata kwa kata, nyumba kwa nyumba, mlango kwa mlango.Tuhakikisha kura zako zinakuwa za kumwaga,”amesema Zedi.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...