Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Iringa

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Dk.John Magufuli ameeleza mipango iliyopo katika kuboresha sekta mbalimbali nchini ikiwemo ya kilimo, madini, uvuvi, kilimo, biashara, ufugaji na utalii huku akisisitiza katika miaka mitano ijayo Serikali imeweka mkazo mkubwa kuendeleza sekta hizo.

Dk.Magufuli amesema hayo leo Septemba 28 mwaka 2020 wakati akizungumza na maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Iringa katika mkutano wake wa kampeni wenye lengo la kuomba ridhaa ya wananchi kumchagua tena kwa miaka mitano kuongoza nchi katika kuiletea maendeleo.

Kuhusu sekta ya kilimo amesema kuna kila sababu ya kuhakikisha sekta hiyo inasimamiwa vema ili nchi kuwa na chakula cha kutosha kwani nchi isipokuwa na chakula hata watu wake hawawezi kufanya kazi.

Amekumbusha alipoingia madarakani mwaka 2015, alitoa kauli ya kwamba asiyefanya kazi na asile na asipokula atakufa kwa njaa. "Leo hii hatuna njaa katika nchi yetu, wananchi wameendelea kulima na kupata chakula, huo ndio ukweli, hata maandiko yanasema asiyefanya kazi na asile."

Pia Dk.Magufuli amesema wameweka mkakati kuhakikisha dawa za mifugo, matrekta, mbolea viwe vinapatikana kwa bei ya chini ili kuwawezesha wakulima kuendelea na shughuli zao vizuri na katika Ilani ya mwaka huu wamepanga kuongeza nguvu katika kilimo cha umwagiliaji ili kupunguza utegemezi katika kilimo cha mvua.

"Tutaanzisha mifumo ya bima kwa watu wanaojihusisha na sekta ya kilimo, tutaendelea kuhamasisha watu kuanzisha viwanda vidogo vidogo, tumepanda kurejesha rotuba ya udongo katika hekta 300,000,"amesema Dk.Magufuli.

Kwa upande wa sekta ya mifugo Dk.Magufuli amesema wataendelea kupima na kuongeza maeneo ya ufugaji na wataanzisha mashamba darasa ya mifugo na zaidi ya hapo watahakikisha kila Wilaya kunakuwa na daktari wa mifugo, kila Kata kunakuwa na daktari wa mifugo, kutakuwa na majosho na hayo yapo katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu katika ukurasa wa 48 hadi ukurasa wa 52.

Katika uvuvi amesema wataendelea kuboresha miundombinu katika sekta hiyo ikiwemo ya kuimarisha masoko ya samaki katika bahari, kuboresha mialo tisa, watahamasisha sekta binafsi katika ununuzi wa meli tano.Watarajesha mazalio ya samaki yaliyoharibika na kuendelea kudhibiti uvuvi haramu kwani haukubaliki.

Kuhusu sekta ya biashara Dk.Magufuli amesema wataendelea kufanya mapitio ya sera,wataratibu masoko ya kimkakati katika maeneo ya mipakani na wataongeza kasi ya majadiliano ya kikanda ."Tanzania ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, pia ni mwanachama wa SADC, tunataka kutumia masoko hayo kufanya biashara. katika miaka mitano Tanzania ndio inasambza dawa kwa jumuiya ya SADC,"amesema.

Pia amesema katika sekta ya madini nayo haikuachwa nyuuma na hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa ikiwa pamoja na kudhibiti madin na waliamua kufanya madini kuwa mali ya Watanzania na sio mali ya kuibiwa.Madini yetu yamekuwa yakilindwwa wakati wote, yametengenezewa sheria.

"Wakati namzungumzia kujenga ukuta katika madini ya Tanzanite kule Mirerani kuna watu waliona ni kichaa, fedha inaingia pale, heshima imerudi, wakati tunaingia nchi iliyokuwa inaongoza kwa kuuza Tanzanite haikuwa Tanzania, tulikuwa tunauza asilimia tatu tu, hatukuwa wa kwanza wala wa pili.

"Tunataka kuitengeneza Tanzania yetu, tunataka kulinda wafanyabiashara wadogo wadogo wa madini, wakipata madini yao ni mali yao.Hata matajiri ambao ambao wapo Ulaya wametengenezwa.Ukurasa 108 hadi 110 wa Ilani imeeleza vizuri sana kuhusu madini,"amesema Dk.Magufuli.

Kwa upande mwingine Dk.Magufuli amezungumzia sekta ya utalii ambapo wataongeza idadi ya watalii hadi kufikia watalii milioni tano kwa mwaka kutoka watalii milioni 1.5 kwa sasa."Ndio maana tumetangaza hifadhi nyingi za taifa.Tumeendelea kukarabati viwanja vya ndege katika maeneo mbalimbali nchini ili watalii waje kwa wingi, mtalii haji kwa bajaji anakuja kwa ndege, kwa hiyo tutaendeleza sekta ya utalii."

Pia amesema Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika uwekezaji na kuna ripoti ambayo imetolewa mwaka 2019 ambayo imeonesha Tanzania iliongoza kwa Afrika Mashariki katika kuhamasisha uwekezaji na kwamba katika eneo hilo Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...