Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (wa tatu kulia), akikata utepe ikiwa ni alama ya kuzindua rasmi ujenzi, ukarabati na upanuzi wa viwanja vinne vya ndege vya Shinyanga, Tabora, Sumbawanga na Kigoma, utakaogharimu Euro milioni 50 sawa na Sh. bilioni 136.85 zikiwa ni mkopo nafuu kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB), katika ukumbi wa Benki Kuu Tanzania (BoT), jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, Mkurugenzi wa Miundombinu TAMISEMI Mhandisi Gilbert Mwoga na Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Viwanja vya Ndege -TAA, Bw. Hamisi Amiri.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (katikati), akijiandaa kukata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa ujenzi, ukarabati na upanuzi wa viwanja  vinne vya ndege vya Shinyanga, Tabora, Sumbawanga na Kigoma, utakaogharimu Sh. bilioni 136.85, zikiwa ni mkopo nafuu kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB), kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi, Patrick Mfugale na kulia ni Mkurugenzi wa Miundombinu TAMISEMI, Mhandisi Gilbert Mwoga

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Benny Mwaipaja,  akielezea kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa miradi katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Tano yaliyoko kwenye kijitabu alichokishika (kinachopatikana kwenye tovuti ya Wizara ya Fedha na Mipango www.mof.go.tz) wakati akizindua rasmi ujenzi, ukarabati na upanuzi wa Viwanja vinne vya ndege vya Shinyanga, Tabora, Sumbawanga na Kigoma, utakaogharimu takribani Euro milioni 50 sawa na Sh. bilioni 136.85, zikiwa ni mkopo nafuu kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar es Salaam.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi, Patrick Mfugale, akieleza mchanganuo wa matumizi ya Euro milioni 50 sawa na Sh. bilioni 136.85 zitakavyotumika katika ujenzi wa Viwanja vinne vya ndege vya Shinyanga, Tabora, Sumbawanga na Kigoma Pamoja na manufaa ya mradi kwa Taifa na jamii, katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa ujenzi, ukarabati na upanuzi wa viwanja  vinne vya ndege vya Shinyanga, Tabora, Sumbawanga na Kigoma, utakaogharimu Sh. bilioni 136.85. Hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Museum ulioko Benki Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam.

Meza Kuu ikiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi, Patrick Mfugale (kushoto), Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Shaaban (wa tatu kulia waliosimama nyuma), wawakilishi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, TAMISEMI na Maafisa waandamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango, baada ya kuzinduliwa rasmi kwa mradi wa ujenzi, ukarabati na upanuzi wa viwanja vinne vya ndege vya Shinyanga, Tabora, Sumbawanga na Kigoma, utakaogharimu takribani Euro milioni 50 sawa na Sh. bilioni 136.85, katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar es Salaam.

Meza Kuu ikiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (wa tatu kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi wa Kapuni zilizopata zabuni ya ujenzi wa Viwanja vya ndege vya Shinyanga, Tabora, Sumbawanga na Kigoma, kutoka kampuni za M/S China Henan International Corporation Group Ltd (Chico); M/S Sino- Shine Overseas Construction and Investment East Africa Limited na Beijing International Corporation Group C. Ltd).

 (Picha na WFM, Dar es Salaam)

**************************************

Na. Ramadhani Kissimba na Peter Haule, Dar es Salaam

Serikali imezindua mradi wa ujenzi, ukarabati na upanuzi wa viwanja vinne vya ndege vya Shinyanga, Tabora, Sumbawanga na Kigoma ili viwe na kiwango cha kimataifa, utakaogharimu shilingi bilioni 136.85.

Akizindua ujenzi wa mradi huo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, amesema kuwa fedha hizo zimetolewa kama mkopo wenye masharti nafuu na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank) kwa ajili ya kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji wa abiria katika maeneo hayo ya kimkakati.

‘’Nichukue nafasi hii kuwashukuru sana Wadau wa Maendeleo hususan Benki ya Uwekezaji ya Ulaya kwa kukubali kufadhili mradi wa Viwanja vya Ndege vya kimkakati kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’’Alisema Bw. James

Bw. Doto James alieleza kuwa uboreshaji wa viwanja hivyo vya kimkakati unalenga kuvipa uwezo viwanja vya ndege vya mikoa ya Shinyanga, Tabora, Sumbawanga na Kigoma ili kutumia fursa nyingi zilizopo kwenye maeneo hayo na kukuza uchumi ambao utakuwa chachu ya maendeleo katika Sekta ya Uchukuzi, Utalii, Kilimo na Anga katika mikoa husika na nchi kwa ujumla.

“Kukamilika kwa mradi huu kutaongeza uhakika wa kufikika, kurahisisha usalama, mawasiliano, na kuboresha biashara na nchi jirani na kuvifanya viwanja hivyo vitumike wakati wote kwa kuweka miundombinu ya taa na kuvipa hadhi ya Kimataifa ili ndege kubwa kama “Dreamliner” ziweze kutua” aliongeza Bw. James

“Ni matumaini ya Serikali kuwa utekelezaji wa miradi hii utakuwa chachu ya maendeleo katika Sekta ya Uchukuzi, Utalii, Kilimo na Anga katika mikoa husika na nchi kwa ujumla” alifafanua Bw. James

Alisema Kiwanja cha ndege cha Shinyanga kitajengwa kwa gharama ya dola za Marekani 19,087,558 (sawa na shilingi bilioni 44.07), Sumbawanga, dola za Marekani 21,699,083 (sawa na shilingi bilioni 50.11) Tabora, dola za Marekani 10,491,745 (sawa na shilingi bilioni 24.23), Kigoma kitajengwa kwa kutumia dola za Marekani 11,794,876.62 (sawa na shilingi bilioni 27.24) .

Aidha, Bw. James alifafanua kuwa gharama za washauri elekezi katika mradi huo ni dola za Marekani 2,208,803 (sawa na shilingi bilioni 3.69) kwa Viwanja vya ndege vya Shinyanga na Sumbawanga na dola za Marekani 1,599,034.30 (sawa na shilingi bilioni 3.69) kwa Viiwanja vya Ndege cha Kigoma na Tabora.

Bw. James aliwataka wakandarasi waliopewa kazi ya ujenzi wa viwanja hivyo ambao M/S China Henan International Corporation Group Ltd (Chico); M/S Sino- Shine Overseas Construction and Investment East Africa Limited; Beijing International Corporation Group C. Ltd).

Alimwagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania-TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale, kusimamia kwa karibu ujenzi wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati kwa mujibu wa mikataba waliyoingia na wakandarasi hao ambao ni kipindi cha kati ya miezi 12 na 18 na kwamba hakutakuwa na muda wa nyongeza.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania-TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale, alisema ujenzi wa viwanja hivyo utahusisha upanuzi wa njia za kurukia ndege, majengo ya abiria, barabara za lami za kuingia uwanjani na ujenzi wa maegesho ya magari.

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa Mikoa ya Kigoma, Tabora, Shinyanga na Rukwa ambao watanufaika na mradi huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Bw. Rashidi K. Mchata, alisema kuwa ukamilishaji wa miradi hiyo utasaidia kuunganisha shughuli za uchumi katika mikoa ya pembezoni ya nchi kwa kuwa viwanja hivyo vitakuwa na uwezo wa kuwahudumia wananchi saa 24 kwa majuma 52 na siku 336 kwa mwaka.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...