Rais mteule John Pombe Magufuli amekabidhiwa cheti cha ushindi wa wadhfa wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu 2020.

Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu pia nae amekabidhiwa cheti cha ushindi cha Makamu Rais.

Jaji mstaafu na mwenyekiti Tume ya Taifa ya Uchaguzi Semistocles Kaijage ndiye anayeongoza sherehe hizo baada ya chama tawala cha Mapinduzi kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28.

Katika hotuba yake, Rais mteule John Pombe Magufuli amewashukuru wananchi kwa kumchagua kwa miaka mingine mitano na kusisitiza kwamba atashirikiana na Watanzania wote waliompigia kura na ambao hawakumpigia.

Aidha, ameongeza kwamba ushindi mkubwa alioupata ni deni kubwa kwake kuhakikisha kwamba anatimiza matarajio ya Watanzania.

Bwana Magufuli amewashukuru Watanzania kwa kukipa ushindi chama chake cha Mapinduzi (CCM) katika nafasi ya Urais, Ubunge na kule Zanzibar katika nafasi ya uwakilishi na nafasi ya Udiwani.

''Kupata asilimia 84.4 ni imani kubwa sana kwa Watanzania na nasema kwa dhati nina deni kubwa sana kwa Watanzania, imani yao nitaitimiza kwa kufanya kazi sana usiku na mchana'', Bwana Magufuli amesema.

Bwana Magufuli hakusita kuwashukuru viongozi wa dini ambao kwa kipindi chote cha uchaguzi waliweza kuwaongoza kwa dua na sala na hatimae kumaliza uchaguzi kwa usalama na taifa lao kuendelea kubaki kwa amani.

''Navishukuru pia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kufanya kazi kwa weledi mkubwa na kuhakikisha amani na usalama vinatawala katika kipindi chote cha uchaguzi,'' amesema Bwana Magufuli huku akielezea matumaini yake kuwa usalama utaendelea hata baada ya uchaguzi.

Pia Bwana Magufuli amesema kuwa uchaguzi umeisha na sasa ni wakati wa kufanya kazi.

"Siasa sio vita siasa sio ugomvi sisi sote ni Watanzania napenda kuwaahidi nitashirikiana nanyi katika kuhakikisha tunasukuma mbele gurudumu la maendeleo ya nchi yetu. Tanzania kwanza mambo mengine baadae" Magufuli amesema.

Amewashukuru viongozi wa nchi nyingine waliomtumia salamu za pongezi.

KWA HISANI YA BBCSwahili

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...