Mmoja wa walimu wa darasa la Jifunze akiwafundisha wanafunzi wake darasani, ikiwa ni mradi wa majaribio unaoendeshwa na Uwezo Tanzania kwa kushirikiana na Halmashauri ya Ludewa.

Mdhibiti Mkuu Ubora wa Shule Wilaya ya Ludewa, Bw. Florian Mtweve akizungumza na mwandishi wa habari hizi(hayupo pichani).

Wanafunzi wa darasa la Jifunze wakishangilia na walimu wao baada ya kumaliza kipindi chao. Darasa hili ni moja ya darasa la majaribio linaloendeshwa Shule ya Msingi Maholong'wa.

Na Joachim Mushi, Ludewa
HALMASHAURI ya Wilaya ya Ludewa Mkoa wa Njombe inafanya utaratibu wa kutaka kuutumia mradi wa darasa Jifunze katika shule zake zote ikiwa ni kujaribu kutokomeza idadi ya watoto wasiojua kusoma na kuandika kuanzia darasa la tatu hadi la sita.

Taarifa zinaonesha shule nyingi za msingi katika halmashauri hiyo zimekuwa zikiongoza ukilinganisha na maeneo mengine ya mkoa huo kwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wasiomudu kusoma na kuandika kuanzia darasa la tatu hadi la sita, jambo ambalo lilisababisha Taasisi ya Uwezo kutambulisha mradi wa darasa Jifunze ambao umetekelezwa kwa majaribio katika shule tano eneo hilo kujaribu kukabiliana na changamoto hiyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni, Mjini Ludewa Mdhibiti Mkuu Ubora wa Shule Wilaya ya Ludewa, Bw. Florian Mtweve alisema baada ya kuona mradi wa darasa la Jifunze umepata mafanikio katika kipindi cha majaribio kwa baadhi ya shule wanafanya mazungumzo na wakufunzi wa Uwezo ili washirikiane kuwaandaa walimu wa serikali kwa gharama za halmashauri kuendesha mpango huo.

“..Tunampango wa kuomba wataalam wa Uwezo wa tatu au wanne ambao tutawaunganisha na walimu ambao tayari walipewa mafunzo ya namna ya kuendesha darasa la Jifunze, pamoja na viongozi wa wilaya tuwafundishe walimu wote wa shule zetu za msingi za Serikali ambazo ni 113, tuwafundishe kwa siku tatu hadi tano ili walimu wetu waweze kufundisha kwa mfumo huo katika shule zote za halmashauri,” alisema Bw. Mtweve.

Alisema mpango wao ni kuhakikisha wanakamilisha kutoa mafunzo kwa walimu wao mwezi wa Desemba, ili kati ya mwezi Januari na Februari 2021 aina hiyo ya ufundishaji iweze kutumika kwa madarasa ya awali, darasa la kwanza na darasa la pili. “…lengo letu ni mfumo huu wa darasa la Jifunze tuuhamishie kwenye shule zetu zote za serikali, maana tumeona mafanikio yake,” alisisitiza mkaguzi huyo wa ubora wa elimu.

Aidha alisema mradi huo maalum wa darasa la Jifunze unaotekelezwa katika Shule tano za Msingi ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa kwa majaribio ulio kuwa na lengo la kuwasaidia wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika wa kuanzia darasa la tatu hadi la sita umeonekana kuwa na mafanikio makubwa kwa muda mfupi tangu kuanzishwa kwake na Taasisi ya Uwezo Tanzania.

Alibainisha kuwa mafanikio ya utekelezaji wa mradi huo yanaridhisha kwa kiasi kikubwa kwani ukitolea mfano tu kwa Shule tatu zinazofanyiwa majaribio, kati ya wanafunzi 231 ambao walibainika hawajui kusoma na kuandika kwa shuleza msingi Maholong'wa, Shaurimoyo na Matika ndani ya siku 30 baada ya kutekelezwa mradi huo ni wanafunzi 30 tu ndio walisalia hawajui kusoma na kuandika.

Mradi wa Jifunze unaoendeshwa kusaidia wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika kwa darasa la tatu hadi la Sita umekuwa ukitekelezwa kwa baadhi ya wilaya zenye changamoto ya ujifunzaji kwa wanafunzi, na umekuwa ukiwatumia walimu waliopata mafunzo kufundisha kwa muda wa ziada kuwasaidia wanafunzi wenye changamoto hiyo, ukitekelezwa kwa siku 30, kabla ya kufanya tathmini kila baada ya siku 10.

Mradi umekuwa ukitekelezwa kwa walimu kutoa mada kwa vitendo na ukaribu zaidi na wanafunzi, kujenga urafiki, kutumia vifaa rahisi kufundishia, kuimba na kucheza na kutoa motisha kwa wanafunzi wanaojifunza jambo ambalo limekuwa na mabadiliko makubwa katika kujifunza kwa wanafunzi eneo hilo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...