Na Grace Gurisha, Michuzi Tv

TAASISI inayohusika na michezo kwa watu wenye ulemavu wa akili Tanzania  (Special Olympics Tanzania), imesema  jamii inatakiwa kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata nafasi sawa na wenzao ya kushiriki katika michezo, burdani, mapumziko na shughuli zote za kijamii.

Hayo yamesemwa Leo Desemba 1, 2020 na Mkurugenzi  wa Taasisi hiyo, Charles Rays wakati wa mafunzo ya siku mbili kuhusu Michezo Jumuishi (Unified Sports) mkoani Mtwara katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Mtwara, ambapo washiriki 45 walishiriki kupata mafunzo ya Michezo Jumuishi.

Rays amesema watoto hao wanatakiwa wajumuishwe katika shughuli zote za michezo ikiwemo ile ambayo ipo kwenye mfumo wa kishule, lengo ni kuhakikisha watoto wenye ulemavu na wasio walemavu wanacheza na kufurahi pamoja bila ubaguzi.

"Jitahidini muwachanganye watoto katika michezo yote bila kujali kuwa wana ulemavu, watoto huwa wanaelewana mapema sana, naamini wakichanganywa pamoja watafurahia michezo bila ubaguzi kwa sababu watajiona kuwa wote ni sawa," amesema Rays

Amesema watoto wenye ulemavu wa  akili wanakuwa na haki kwa msingi wa usawa na watoto wengine kutambuliwa na kuungwa  mkono.

Mafunzo hayo yamefadhiliwa na  Stavros Niarchos Foundation (SNF) wenye dhima ya kuleta ukaribu wa kujifunza na wa kucheza kwa watoto wenye ulemavu na wasio walemavu," amesema Rays

Mkurugenzi huyo, amesema katika mafunzo  hayo wameshiriki walimu wa shule za Msingi, makocha, viongozi wa ngazi za juu, maafisa michezo na maafisa elimu maalumu, ambapo yamefanyika kwa siku mbili.

Pia, Rays amesema washiriki ambao ni walimu kutoka kwenye shule maalumu walipata nafasi ya kushiriki mafunzo ya uwanjani kwa lengo la kuwajenga zaidi.

Kwa upande wake, Mwalimu/Mkufunzi Chuo cha Ualimu Mtwara, Fadhil Kaganda ameishukuru taasisi hiyo kwa mafunzo waliyowapatia, kwa sababu yamewaongezea maarifa ambayo yatawasaidia katika masuala ya michezo kwa watoto wenye ulemavu na wasio walemavu.

Naye, Naelijwa  Kimbwereza ambaye ni Mwalimu Elimu maalum  kitengo cha Shangani Mtwara, amesema mafunzo hayo ni muhimu sana kwake ambapo wameweza kujikumbusha mambo mengi na pia kupata maarifa mapya kuhakikisha wanawachanganya watoto hao katika michezo mashuleni.

Mkurugenzi wa Taasisi inayohusisha na michezo kwa watu wenye ulemavu wa akili (Special Olympics Tanzania), Charles Rays akitoa mafunzo kwa walimu wa shule za msingi, makocha, maofisa Elimu maalumu, maofisa michezo (hawapo pichani) kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya Special Olympics yalifanyika mkoani Mtwara
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya Special Olympics wakifuatilia mafunzo yaliyokuwa yakitolewa na Mkurugenzi wa Taasisi inayohusisha na michezo kwa watu wenye ulemavu wa akili (Special Olympics Tanzania), Charles Rays ( hayupo pichani).
Ofisa Michezo Halmashauri, Wilaya ya Mtwara, Nicholaus Mmuya ambaye alikuwa mgeni rasmi, akifungua mafunzo ya Special Olympics kwa walimu, makocha, maafisa elimu maalumu na maafisa michezo yaliyoandaliwa na Special Olympics Tanzania, ambapo washiriki 45 waliyopata mafunzo hayo walipatiwa vyeti vya kushiriki.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...