Na Mwandishi wetu, Kiteto
MADIWANI
na Wakuu wa idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, wamepatiwa
mafunzo ya ushiriki wa kila mmoja kupambana na rushwa, yaliyotolewa na
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Manyara.
Mkuu
wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza kwenye
mafunzo hayo amewahimiza madiwani kusimamia miradi ya maendeleo katika
maeneo yao ili kufanikisha ilani ya CCM ambayo ndiyo inaongoza Serikali.
Makungu
amesema popote pale wakibaini miradi yenye dalili za kuhujumiwa na
wakandarasi wasio waadilifu au inayoonekana kujengwa chini ya kiwango,
watoe taarifa TAKUKURU kwa simu namba 113 ambayo haihitaji kulipiwa.
Amesema
TAKUKURU ndicho chombo chenye mamlaka kwa mujibu wa sheria ya kuzuia na
kupambana na rushwa namba 11/2017 kuongoza vita dhidi ya rushwa
Tanzania bara.
Amesema
sheria ya manunuzi inazuia halmashauri kufanya manunuzi kwa waajiriwa wa
halmashauri au makampuni ya madiwani au kampuni za wabia wa madiwani.
"Hapa
watendaji kama Mkurugenzi wa halmashauri, mhasibu, mhandisi, mkuu wa
kitengo cha manunuzi huingizwa kwenye uhalifu huo ambao mara nyingi
manunuzi na zabuni hutolewa kwa makampuni ya madiwani au jamaa zao ambao
huwa asilimia 10," amesema Makungu.
Amesema
matokeo yake miradi husika hujengwa chini ya kiwango kwa kuwa fedha
nyingine haziendi kwenye miradi hiyo zinaingia mifukoni mwa madiwani na
hakuna wa kumfunga paka kengele.
"Ndiyo
maana utashangaa miradi iliyo chini ya kiwango baadhi yenu hufumbia
macho hadi iibuliwe kwenye ziara ya Mkuu wa Mkoa, Waziri Mkuu, Makamu wa
Rais au Rais mwenyewe, wakati madiwani wapo na miradi hiyo ipo maeneo
yenu," amesema Makungu.
Hata
hivyo, amesema pia tatizo lipo kwenye mazingira ya baadhi ya madiwani
waliopita kwa njia ya rushwa, ikitokea watendaji wa halmashauri
wamekataa kuwa sehemu ya uovu utasikia kikao cha madiwani kimewaazimia
kwa kudai hawapati ushirikiano kwani kuna baadhi ya maeneo wakurugenzi
na wakuu wa idara wamefanyiwa hivyo na ukiuliza madiwani wanadai
Mkurugenzi au Mkuu wa idara hana ushirikiano.
Amesema
katika baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto lililopita
baadhi ya madiwani walishirikiana na wenyeviti wa vijiji na vitongoji
na baadhi ya watendaji wa serikali ngazi ya vijiji na kata walikuwa
chanzo cha migogoro ya ardhi baina ya wafugaji na wakulima, kijiji na
kijiji au mtu na mtu.
"Ukiwa
wewe ni Diwani unahamasisha wananchi wakalime msitu wa hifadhi ya jamii
kama vile Suledo, wakalime WMA au Emboley Murtangos fahamu kuwa
unatumia mamlaka yako vibaya na unaweza kushtakiwa chini ya sheria
kifungu cha 31/PCCA 2007," amesema Makungu.
Amesema
baadhi ya madiwani kwenye baraza lililopita wanaotoka kwenye kata zenye
minada wanarudisha nyuma maendeleo kwa kuweka watu wao wanaowapa sehemu
ya fedha za ushuru badala ya kukusanya na kufikisha halmashauri.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...