Na Mwandishi wetu Mihambwe
Mkuu
wa Mkoa Mtwara Mhe. Gelasius Gasper Byakanwa ameungwa mkono na Wananchi
wa Tarafa ya Mihambwe na viunga vyake kupitia kampeni aliyoianzisha ya
kuondoa mapori na kuongeza uzalishaji wa zao la Korosho na mazao
mengineyo.
Hayo
yamejidhirisha kupitia mkutano uliofanyika Kijiji cha Misufini
uliotangaza rasmi kampeni hiyo ambapo RC Byakanwa amesisitiza ni lazima
kila Mtu apanie kuongeza uzalishaji kwa kupanda kwa utaratibu,
kupandikiza Mikorosho na kufufua mashamba yaliyotelekezwa.
"Kila
Mwananchi ni lazima awe na shamba la kulima na alime kisasa ikiwemo
kupanda kwa utaratibu, kuondoa mikorosho mizee na kulima mazao
mchanganyiko. Nataka Watu mfanye kazi usiku na mchana." alisisitiza RC
Byakanwa.
RC Byakanwa
aliambatana na timu ya Wataalamu wa kilimo ambao walienda kutoa elimu ya
namna ya kuongeza uzalishaji wa Korosho na Wananchi wengi wamempongeza
RC Byakanwa kwa ubunifu wake huo kwani ilikuwa ni kiu yao ya siku nyingi
kupata elimu ya kilimo kufuatia uzalishaji wa Korosho kuzidi kushuka
siku hadi siku.
"Mkuu wa
Mkoa Mtwara Mhe. Byakanwa amevunja rekodi ya viongozi wote kwa
kutuletea elimu ya kuongeza uzalishaji wa Korosho, Wananchi wa Tarafa ya
Mihambwe tunamuunga mkono sana kwa hili. Nami nipo tayari kabisa shamba
langu litumike kama shamba darasa kwani nimechoka kila siku uzalishaji
kuzidi kupungua." Alisema Ndugu Awadhi Rashid mkazi wa Kijiji cha
Mihambwe.
Akizungumza na
Mwandishi wetu baada ya mkutano huo, Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel
Shilatu amempongeza sana RC Byakanwa kwa kuja tena kivingine ambapo
safari hii amekuja kuongeza uzalishaji wa Korosho.
"Mhe.
Byakanwa ni kiongozi mbunifu sana. Alianza na kampeni ya shule ni choo
ambayo ilifanya vyema sana na leo hii kero ya vyoo shuleni imepungua
sana. Leo hii kaja na kuongeza uzalishaji wa Korosho ambayo natumai
itasaidia sana kumkomboa Mkulima wa Korosho. Kampeni hii inaenda kukata
kiu ya elimu ya kilimo bora cha Korosho na hivyo tunatarajia uzalishaji
kuzidi kuongezeka. Kwa niaba ya Wakazi wa Tarafa ya Mihambwe
tunampongeza sana na tunamuunga mkono Mhe. Byakanwa." Alisema Gavana
Shilatu.
RC Byakanwa
amekuja na kampeni ya kuondoa mapori na kuongeza uzalishaji ambapo
imelenga kuondoa mikorosho mizee na isiyozaa, kuondoa mikorosho
iliyopandwa bila ya utaratibu, kufufua mashamba yaliyotelekezwa na
kuanzisha mashamba mapya sanjali na kuongeza uzalishaji wa mazao
mengineyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...