Na Said Mwishehe, Michuzi TV
MWILI wa muigizaji mkongwe katika tasnia ya sanaa ya uigizaji wa filamu 'Bongo Movie' Mohamed Fungafunga maarufu kwa jina la Jengua umepumzisha leo Desemba 16,2020 katika makaburi ya Mburahati jijini Dar es Salaam.
Fungafunga alifariki dunia jana Desemba 15,2020 wilayani Mkuranga mkoani Pwani na kifo chake kimetokana na ugonjwa wa kupooza mwili upande mmoja.
Wakati wa kuupumzisha mwili wake katika nyumba yake ya milele, wasanii mbalimbali, wananchi wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Abu
bakar Kunenge wameshiriki katika tukio hilo la mazishi. Fungafunga amezikwa leo saa saba mchana.
Akizungumza kwa kifupi mbele ya waombolezaji waliokuwa makaburi ya Mburahati, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Aboubakari Kunenge amesema kuwa muigizaji huyo wa filamu mchango wake katika nchi yetu hautasahaulika kwani amefanya kazi kubwa na nzuri huku akitoa rai kwamba hiki ni kipindi cha kuzungumzia mema yake aliyofanya enzi za uhai wake kwani ndivyo dini inavyoagiza.
Wakati huo huo waigizaji mbalimbali wamepata nafasi ya kumzungmzia Fungafunga ambapo wengi wao wamesema alikuwa mcheshi, mkarimu na mwenye upendo na kuhusu kazi ya uigizaji aliipenda kutoka moyoni, hivyo aliifanya kwa ufanisi mkubwa.
Akimzungumzia Fungafunga, Muigizaji Rashid Mwinshehe 'Kingwendu' amesema mzee Jenguo enzi za uhai wake alikuwa mpole sana mtaani na alikuwa tofauti na namna ambavyo anaigiza kwa ukali. "Alikuwa anaongea na watu vizuri na aliheshimu kila mtu lakini akiwa kazi alikuwa makini na asiyependa masihara, lengo ni kuhakikisha anafanya kazi iliyo bora."
Kwa upande wake Muigizaji Steve Mengele 'Steve Nyerere' amesema sanaa ya uigizaji wa filamu ina wazee wachache na ndio hao wanaondoka, hivyo kuna hatari ya kukosekana wazee wa kuwakanua vijana na kuwalekeza nini ambacho wanatakiwa kukifanya kulinda hesima ya tasnia ya sanaa ya uigizaji filamu.
"Kwetu sisi ni pengo kubwa lakini pia ni mtu ambaye mimi nimefanya naye filamu ya Mke mwema, kwa hiyo namjua.Nikumbushe tu Jengua ni miongoni mwa waanzilishi wa hii tasnia kupitia kundi la Kidedea kwa wanaokumbuka, Mambo hayo na Kaole, nilipenda sana kuangalia kazi anazofanya yeye pamoja na wengine."
Kwa upande wake muigizaji Fadhili Msisiri amesema Fungafunga enzi za uhai wake alikuwa pacha wake, na alikuwa karibu naye sana na msiba huo ni pengo kubwa katika tasnia hiyo ya uigizaji wa filamu."Jengua alikuwa mshauri wangu.
"Tulikuwa tunasaidia katika kila jambo.Jengua amenisaidia katika kazi zangu bila kumpa chochote,"amesema huku akitumia nafasi hiyo kuwataka wasanii kuungana na kushikamana.
Wakati huo huo Muigizaji Seif Sulemain 'Seif Pembe' amesema anafahamu Jengua kama msanii mwenzake na hakuwa msanii wa mchezo bali ni gwiji katika uigizaji, na alikuwa na uwezo mkubwa wa kuigiza.
"Kwa mfano mkiwa mnarekodi filamu alikuwa anawaweka watu wakae vizuri, alikuwa hapendi masihara wakati wa kazi , labda kazi iwe imekwisha.Pia alikuwa hataki kushindwa na kitu, kwa mfano kitu kimeandikwa na mwandishi yeye atakipitia zaidi ya mara tatu kujiridhisha kama kiko sawa.
Akizungumzia maisha yake ya kawaida nje ya kazi, amesema alikuwa mkarimu sana, alikuwa mcheshi na hakuwa akileta mambo ya filamu katika maisha yake ya kawaida."Alikuwa mtulivu sana, aliipenda Yanga na mimi naipenda Simba , tuliishi naye vizuri."
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Aboubakari Kunenge akizungumza kwa kifupi mbele ya waombolezaji waliokuwa kwenye mazishi ya muigizaji mkongwe katika tasnia ya sanaa ya uigizaji wa filamu 'Bongo Move' Mohamed Fungafunga maarufu kwa jina la Jengua aliyepumzishwa leo Desemba 16,2020 katika makaburi ya Mburahati jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...