Na Muhidin Amri,Songea
WANANCHI wa kijiji cha Mgazini kata ya Mgazini halmashauri ya wilaya Songea mkoani Ruvuma,wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza idadi ya watumishi wa sekta ya Afya na dawa katika zahanati ya kijiji hicho ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi na dawa.
Hayo yameelezwa jana na baadhi ya wananchi wa kijiji hicho waliohudhuria mkutano wa kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi juu ya ufuatiliaji wa Uwajibikaji jamii uliofanywa na shirika lisilo la kiserikali ROA kupitia mradi wa SAM unaofanya kazi katika sekta ya Afya kwenye kata tano za wilaya ya Songea.
Lucius Bula na Damian Mwenda wamesema, katika zahanati ya kijiji hicho kuna mganga mmoja na wauguzi watatu,hivyo kutokana na idadi kubwa ya watu inakuwa vigumu kwa watumishi hao kutoa huduma kwa wakati muafaka na kusababisha wagonjwa kutumia muda mwingi wakiwa foleni ya kuonana na Daktari.
Bula alisema,kwa sasa idadi ya watumishi waliopo ni ndogo kufuatia watu wengi hasa wageni wanaofika katika kijiji hicho na mikoa mingine hapa nchini kwa ajili ya shughuli mbalimbali kama kilimo na ufugaji ambao pindi wanapougua wanakimbilia zahanati ya Mgazini kupata huduma ya matibabu.
Kwa mujibu wa Bula,kuingia kwa wageni hao kumesababisha watumishi hao kuzidiwa na idadi ya wagonjwa na hivyo kusababisha baadhi ya wananchi kukimbilia Hospitali ya St Joseph Peramiho na wengine Hospitali ya mkoa Songea umbali wa km 45.
Damian Mwenda amesema, awali zahanati hiyo ilijengwa kuhudumia wananchi wa Mgazini tu, lakini sasa inalazimika kuhudumia wananchi wa vijiji vya jirani na ndiyo maana hata dawa zinazoletwa hazitoshelezi, kwa kuwa serikali inapeleka dawa kwa ajili ya kuhudumia wananchi wa kijiji kimoja na sio wa vijiji vingine.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...