Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisikiliza maelezo kuhusu uzalishaji wa mkonge kwenye shamba la Amboni Kigombe lililopo wilaya ya Muheza leo. Katikati ni Mkurugenzi wa kampuni hiyo Cuthbert Neil na kulia kwake ni Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa ameshika nyuzi za mkonge wakati alipokagua utendaji kazi wa kiwanda cha kuchakata mkonge cha Amboni Spinning Tanga leo .

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (wa pili toka kulia) akizungumza na mwekezaji wa shamba la mkonge Amboni Kigombe Cuthbert Neil (katikati) leo alipotembelea shamba hilo wilayani Muheza ambapo amewataka wamiliki wa shamba hilo kuanzisha mashamba zaidi na kujenga kiwanda kikubwa cha kuchakata bidhaa za mkonge.

Nyuzi za mkonge zikiwa zimeanikwa mara baada ya kuchakatwa kwenye kiwanda cha Amboni Spinning cha Tanga.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ( katikati) akitazama mashine ya kufunga robota la mkonge wakati alipotembelea kiwanda cha Amboni Spinning wilaya ya Muheza leo. Kulia ni Mkurugenzi wa kiwanda hicho Cuthbert Neil.
( Habari na picha na Wizara ya Kilimo

………………………………………………………………………………….

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje kuja Tanzania na kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamanai ya mazao ya kilimo ikiwemo zao la mkonge.

Ametoa wito huo leo (21.01.2021) wakati akikagua shamba la mkonge la mwekezaji Kigombe Estate la Muheza wilayani Tanga ambapo amempongeza mwekezaji huyo kwa kazi nzuri ya kilimo cha kisasa cha mkonge na kumtaka afungue kiwanda cha kuchakta bidhaa zitokanazo na mkonge.

Waziri Mkuu Majaliwa aliwaambia wakazi wa Muheza kuwa serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuhakikisha nchi inaendelea kuwa yenye amani na usalama ili wawekezaji na wananchi wafanye shughuli zao za kujiletea kipato ikiwemo kilimo.

“ Tanzania ni nchi iliyo salama,hivyo tunawaalika wawekezaji kuja kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo ikiwemo zao la mkonge hapa mkoani Tanga” alisisitiza Waziri Mkuu 

Akizungumza na wakulima na wafanyakazi wa shamba hilo la mkonge Majaliwa alisema ziara yake mkoani Tanga ni mahususi kwa ajili ya kuhamasisha kilimo cha mkonge kutokana na faida zake kiuchumi kwa kuwa hapo zamani wakulima wengi walianza kukata tamaa.

Akitaja faida za kiuchumi za zao la mkonge ,Waziri Mkuu Majaliwa alisema zao hilo hutoa nyuzi zinazotumika kuzalisha vifungashio ikiwemo magunia ambayo ni muhimu kwa utunzaji mazao.

Faida zingine zitokanazo na zao la mkonge ni pamoja na uzalishaji dawa za kuua wadudu, sukari, mbolea kwa ajili ya shambani na pombe (vileo) hivyo wawekezaji wa viwanda vya kuchakata zao la mkonge wanaalikwa kuja Tanzania.

Majaliwa aliongeza kusema serikali inatilia mkazo ujenzi wa viwanda ili kukuza ajira kwa watanzania,kuongeza mapato yatokanayo na tozo na kodi na upatikanaji wa elimu juu ya kilimo cha mkonge kwa wananchi wengi.

“Tumieni maeneo haya ya Handeni, Pangani ,Muheza na Tanga yaliyowazi kulima mkonge. Mkonge si zao la matajili pekee,hata wananchi mmoja mmoja anaweza kulima na kupata kipato cha uhakika huku mkiendelea kulima mazao ya chakula” alisisitiza Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu huyo ametoa agizo kwa wawekezaji wote waliochukua mashamba ya makonge toka miaka ya 1970s lakini sasa hawalimi, kuwa waanze mara moja kuyafufua na kupanda mkonge vinginevyo serikali itawanyanganya na kuyagawa kwa wakulima wadogo wadogo.

Ili kuhakikisha wakulima wengi nchini wanalima zao la mkonge Waziri Mkuu ameagiza Bodi ya Mkonge nchini kuwatembelea wakulima mashambani na kutoa elimu na hamasa pia huduma za ugani.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigella amewapongeza wawekezaji wa shamba la mkonge Kigombe Estate kwa uzalishaji mzuri ikiwemo kuajili wananchi zaidi ya mia tatu shambani hapo.

Shigella ameongeza kusema wataendelea kutoa ushirikiano na mazingira wezeshi kwa wawekezaji wengi zaidi watakaokwenda Tanga kuanzisha mashamba ya mkonge na mazao mengine ili wakuze uchumi wa nchi na kusaidia wananchi kupata kipato.

Naye Mkurugenzi wa Shamba la Mkonge Kigombe Cuthbert  Neil alipongeza serikali kwa ushirikiano inaotoa kuwezesha kampuni hiyo kufanya kazi zake  kwa amani na utulivu.

Neil aliongeza kusema shamba la Kigombe limepokea maelekezo ya serikali ya kuzalisha miche bora ya mkonge na kugawa kwa wakulima wanaozunguka pia kutoa elimu kwa wakulima.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...