Na Shukrani Kawogo, Njombe.
Imeelezwa kuwa wanafunzi 989 kati ya 3012 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wilayani Ludewa mkoani Njombe hawajaripoti kuanza masomo yao katika shule walizopangiwa.
Akisoma taarifa ya maendeleo ya elimu ya sekondari wilayani humo afisa elimu vifaa na takwimu wa wilaya ya Ludewa Samson Machibya mbele ya kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo baada ya kamati hiyo kuanza wiki ya maadhimisho ya chama hicho kinachotimiza miaka 44 tangu kuanzishwa kwake kwa kutembelea na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mpaka kufikia Januari 28 mwaka huu ni wanafunzi 2028 tu ndio walioripoti kuanza masomo hayo katika shule walizopangiwa huku wengine kati ya hao wakienda kusoma shule binafsi.
Amesema hali hii husababishwa na wazazi kutowajibika katika maendeleo ya kitaaluma ya watoto wao huku wengine wakifika mbali zaidi kwa kuwazuia watoto hao wasiendelee na masomo.
Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa ya idara ya udhibiti ubora wa elimu wilayani humo iliyosomwa na naibu mdhibiti mkuu wa ubora wa elimu John Haule imeeleza moja kwa moja baadhi ya shule ambazo zimebainika wazazi kuwashawishi watoto wao kufanya vibaya.
Haule amezitaja shule hizo kuwa ni shule ya msingi Madope, Lupingu, Luvuyo, Ilawa pamoja na shule ya msingi Mlangali.Aidha kwa upande wa katibu wa CCM wilayani humo Bakari Mfaume amesema inapaswa kufanyika upelelezi wa kuwatambua wazazi wanao wazuia watoto wao kufanya vizuri na watakaobainika wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Ameongeza kuwa wazazi wanatakiwa kupatiwa elimu juu ya faida ya kufuatilia Maendeleo ya watoto wao kwa kushirikiana na afisa Maendeleo ya jamii kwakuwa wao ndio wanahusika kwa sehemu kubwa kwa kukutana na wazazi hii inaweza kuleta matokeo chanya kwa wazazi na wanafunzi hao.
"Nyinyi watu wa elimu kamwe hamuwezi kufanikiwa katika hili endapo mtafanya kazi pasipo kushirikiana na watu wa Maendeleo ya jamii, mnategemea ni mazazi gani atakayekuelewa mwalimu endapo ukimfuata mzazi kumueleza haya? Labda kupitia vikao vya mashuleni na wazazi lakini kwa kuwaelimisha wazazi mitaani afisa Maendeleo ya jamii anahusika kwa sehemu kubwa", Alisema Mfaume.
Naye mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo Sunday Deogratius amesema ushauri uliotolewa na kamati ya siasa wameupokea na wameahidi kuyafanyia kazi ili kukuza kiwango cha elimu katika wilaya hiyo.
Ameongeza kuwa wamejipanga vyema katika kuboresha elimu wilayani humo katika nyanja mbalimbali ambapo wanatarajia kufanya mkutano wa wadau wa elimu Februari 15 mwaka huu utakaolenga kujadili mikakati ya uboreshwaji wa elimu kwa ujumla.
Kamati hiyo ya siasa ikiongozwa na mwenyekiti wa CCM wilaya Stanley Kolimba ilitembelea idara hiyo ya elimu, shule ya sekondai pamoja na hospitali ya wilaya ya Ludewa ili kukagua miradi mbalimbali iliyopo katika maeneo hayo.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa Sunday Deogratias (Aliyesimama) akizungumza na kamati ya siasa ya CCM wilaya hiyo pamoja na wakuu wa idara ya elimu katika ofisi za uthibiti ubora wa elimu.
Afisa elimu vifaa na takwimu sekondari Samson Machibya akisoma taarifa ya Maendeleo ya elimu ya sekondari wilaya ya Ludewa kwa kamati ya siasa ya CCM wilayani humo pamoja na mkurugenzi wa halmashauri hiyo Sunday Deogratias (hawapo pichani)
Mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Ludewa Stanley Mlay (kushoto) akiwa ameongozana na kamati ya siasa ya CCM wilaya pamoja wakuu wa idara mbalimbali wakati wakikagua jengo la idara ya wagonjwa wa nje.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ludewa Stanley Kolimba(kulia) akimuelekeza jambo mkurugenzi wa halmashauri ya Ludewa Sunday Deogratias walipotembelea kukagua hospitali ya wilaya hiyo.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ludewa Stanley Kolimba akisalimiana na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo Sunday Deogratias pamoja na wakuu wengine wa idara ya elimu walipowasili katika ofisi ya uthibiti ubora wa elimu. Kushoto ni katibu wa CCM wilaya Bakari Mfaume pamoja na katibu wa wazazi wilaya Veronica Bilia.
Kamati ya siasa ya CCM wilaya ya Ludewa ikiwasili kakati hospitali ya wilaya hiyo kukagua utoaji huduma ya afya pamoja na miundombinu ya utoaji huduma hizo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...