WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameipa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ifuatilie Halmashauri zilizopaswa kuhamia
kwenye maeneo yake na impatie taarifa ifikapo Jumamosi, Februari 6,
2021.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Februari 4, 2021) wakati
akijibu swali la mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma katika
kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu bungeni jijini
Dodoma.
Mbunge huyo alitaka kujua Serikali inatoa kauli gani kuhusu watumishi
hao walioshindwa kutii agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli
alilolitoa Oktoba 24, 2019 akiwataka wahamie kwenye makao makuu ya
Halmashauri zao kabla ya Oktoba 30, 2019.
Musukuma amesema kitendo hicho kinaitia Serikali hasara kwani
watumishi hao walihamisha ofisi tu kwenda makao makuu ya Halmashauri
lakini wanaendelea kuishi mijini.
Waziri Mkuu amesema anahitaji kupata taarifa juu ya halmashauri ambazo
watumishi wake wanaishi nje ya vituo vyao vya kazi ili hatua za
kinidhamu zichukuliwe. “Serikali inataka watumishi wote waishi kwenye
vituo vyao vya kazi ili waweze kuwahudumia wananchi kwa ukaribu.” Amesema Majaliwa.
Amesema anatambua uhaba wa nyumba za watumishi uliopo lakini kwenye
makao makuu ya Halmashauri kuna nyumba za wenyeji ambazo watumishi hao wanaweza kupanga ili waweze kutoa huduma karibu na wananchi
wanaowaongoza.
Kufuatia hatua hiyo, Waziri Mkuu amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Makatibu
Tawala wa Mikoa wasimamie na kuhakikisha watumishi wote wanaoishi nje
ya vituo vyao vya kazi wanaondoka mara moja na kuhamia katika maeneo
husika. “Simamieni watumishi hao waondoke mara moja, baada ya tamko
hili. Hatuwezi kuwapa muda zaidi sababu umeshapita. Endapo hawatafanya
hivyo, Mkuu wa Mkoa husika achukue hatua.” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imeweka mkakati wa
kukuza zao la mkonge ikiwa ni pamoja na kudhibiti uingizwaji wa bidhaa
za nyuzi za plastiki kutoka nje ili kulinda viwanda vinavyozalisha
nyuzi za mkonge na kuchochea shughuli za uwekezaji.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Korogwe
Vijijini, Timotheo Mnzava aliyetaka kujua mkakati gani umewekwa na
Serikali kuvutia wawekezaji wa viwanda vya kuchakata zao hilo ili
kuwezesha kuwa na masoko ya uhakika.
Amesema Serikali inadhibiti uingizaji wa bidhaa zikiwemo nyuzi
zilizotengenezwa kwa plastiki na kuhamasisha matumizi ya nyuzi
zilitengenezwa kwa kutumia mkonge ili kumlinda mzalishaji anayetumia
zao la mkonge na kuvutia zaidi wawekezaji.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...