NA FARIDA SAIDY, MOROGORO
WAJASIRIAMALI wakiwemo wachoma mahindi, wauza mbogamboga, matunda pamoja na mamalishe katika eneo la Feli Kata ya Magole Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro wamesitisha kwa saa kadhaa shughuli za biashara zao ili kuungana na Watanzania wote kushiriki mazishi ya Hayati Dokta John Pombe Magufuli wakikumbuka alivyo wajengea vibanda vya kufanyia biashara katika eneo hilo.
Michuzi Tv na Blog imefika katika eneo hilo la Feli na kushuhudia shughuli za biashara zikiwa zimesimama huku wafanyabiashara hao wakiwa wamekusanyika kwa ajili ya kufanya maombi maalumu ikiwa ni ishara ya kushiriki maziko ya mpendwa wao Hayati Dk. Magufuli.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wajasiriamali hao wamesema wanamkumbuka Hayati Magufuli kwa vitu vingi hususani kwa kuwa na maamuzi magumu katika kuwasaidia wananchi wa hali ya chini kama alivyowafanyia wao katika Kata ya Magole kwa kuwajengea vibanda vya kufanyia biashara eneo la Feli katika Barabara kuu ya Morogoro-Dodoma.
Aidha, wafanyabiashara hao wamesema wataendelea kuchapa kazi ili kumuenzi huku wakimuomba Rais Mama Samia Suluhu Hasan kufuata nyendo za Hayati Dk. Magufuli
Hata hivyo, katika viunga mbalimbali vya mji wa Morogoro Wananchi walifuatilia moja kwa moja mazishi ya Hayati Dokta Magufuli kupitia Luninga pamoja na mitandao ya kijamii ikiwa ni moja ya njia ya kumuaga Jemedari huyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...