Benki ya CRDB imetajwa kuwa mshindi katika tuzo za FiRe kwa upande wa Tanzania kutokana na uandaaji wa taarifa bora za matokeo ya kifedha kwa mwaka wa fedha 2020.
Katika
tuzo zilizofanyika tarehe 26 Machi 2021 kupitia mitandao, Benki ya CRDB
pia ilitajwa kuwa mshindi wa tatu Afrika Mashariki kwa uandaaji taarifa
za fedha ambapo mshindi wa kwanza ilikuwa ni Benki ya KCB na kufuatiwa
na kampuni ya SCB zote za Kenya.
“Tuzo
hizi zinadhihirisha jitihada kubwa ambazo Benki inazifanya katika
kuboresha kuimarisha ripoti zetu, ili kuongeza uwazi na uwajibikaji.
Sasa hivi tunatumia mfumo wa Ripoti Jumuishi ambazo zinagusa sehemu
kubwa ya taarifa za biashara yetu kwa faida ya wadau wetu wote,” alisema
Afisa Mkuu wa Fedha Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo akielezea sababu
zilizopelekea benki hiyo kushinda tuzo hizo.
Aidha,
Nshekanabo alisema Benki ya CRDB imefanya uwekezaji mkubwa katika
mifumo ya kidijitali ikiwa ni pamoja na kuboresha mifumo ya ukusanyaji
na uandaaji wa taarifa. Benki ya CRDB pia imeuunganisha mfumo wake wa
utoaji taarifa za fedha na mfumo wa kimataifa wa kuandaa taarifa za
fedha (IFRS), na hivyo kupelekea kuwa bora zaidi katika utoaji wa
taarifa za fedha.
FiRe
ni tuzo mashuhuri zaidi Afrika Mashariki kwa ripoti za kifedha. Tuzo ya
FiRe hizi zinakusudia kukuza utoaji wa taarifa kwa njia ya kuongeza
uwajibikaji, uwazi, na uadilifu. Nshekanabo alisema kuwepo kwa tuzo hizi
kumesaidia kuhamasisha taasisi na mashirika ndani ya Afrika Mashariki
kufuata mfumo unaofaa wa utoaji wa taarifa za kifedha.
Tuzo
za Fire zinaandaliwa kila mwaka na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji (CMA)
Kenya kwa kushirikiana na Taasisi ya Wahasibu wa Umma a Kenya (ICPAK),
Soko la Hisa Nairobi (NSE) na Bodi ya Viwango vya Uhasibu wa Sekta ya
Umma (PSASB) Kenya.
Tuzo
hii inazidi kuzihirisha ubora wa taarifa za fedha za Benki ya CRDB
ikizingatiwa kuwa mwishoni mwa mwaka jana 2020, Benki ya CRDB
ilitunikiwa tuzo ya taasisi ya fedha iliyoongoza kwa kuwasilisha Taarifa
ya Fedha bora kwa mwaka 2018/2019 kwa kuzingatia viwango vya kimataifa
na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...