Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Mhe. Dkt Faustine Ndugulile akihutubia Mkutano wa 41 wa Mashirika na makampuni ya mawasiliano katika nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC) unaojulikana kama Southern African Telecommunications Association (SATA) ambao umefanyika kwa njia ya mtandao jijini Dodoma ambapo nchi 23 zimeshiriki kikao hicho.
Mwenyekiti Mpya wa SATA Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania, Waziri Kindamba akitoa maelezo mafupi kuhusu SATA kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi kufungua Mkutano wa 41 wa Mashirika na makampuni ya mawasiliano katika nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC) unaojulikana kama Southern African Telecommunications Association (SATA.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt Faustine Ndugulile akimsikiliza Mwenyekiti anayemaliza Muda wake wa SATA, Afisa Mtendaji Mkuu Bw.Sherry Singh wakati akiwasilisha Maelezo yake kuhusu SATA. Kulia kwake Mwenyekiti Mpya wa SATA Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania, Waziri Kindamba.
====== ======= ======= =========
DKT. NDUGULILE ATAKA NCHI ZA SADC KUONGEZA KASI YA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA YA MAWASILIANO ILI KUKUZA UCHUMI.
Na. Mwandishi Wetu
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile amezitaka Mashirika na makampuni ya mawasiliano katika nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika kuhakikisha zinaongeza kasi ya matumizi ya mawasiliano na TEHAMA katika kuleta maendeleo ya Uchumi katika ukanda huu wa Kusini mwa Afrika.
Dkt. Faustine Ndugulile ameyasema hayo baada ya kufungua Mkutano wa 41 wa Mashirika na makampuni ya mawasiliano katika nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC) unaojulikana kama Southern Africa Telecommunications Association (SATA) ambao umefanyika kwa njia ya mtandao jijini Dodoma ambapo nchi 23 zimeshiriki kikao hicho.
Dkt Ndugulile amesema kuwa nchi wanachama katika SADC watumie fursa mbalimbali zinazopatikana kutokana na kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano hasa matumizi ya intaneti kuwa yanawezesha kufanyika kwa shughuli za biashara, uchumi na maendeleo kwa ujumla.
“kama tukiboresha mawasiliano katika nchi zetu za SADC, hii itasaidia kuongeza na kukuza biashara katika nchi zetu, baada ya mimi kwenda benki kulipia niweze kutumia simu yangu kuweza kununua bidhaa kutoka nchi wananchama” amesema Dkt. Faustine Ndugulile, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Dkt. Ndugulile amesema kuwa anatamani kuona gharama za mawasiliano baina ya nchi hizo za Afrika zinapungua kwa kutengeneza mfumo madhubuti wa kuwa na mawasiliano ya ndani ya Afrika (Regional Hub) badala ya kusafirishwa kwenda nchi za ulaya na marekani ndipo yarudi na kumfikia mlengwa.
“Serikali imewezesha kuwa na mawasiliano ya ndani kama nchi hivyo kushusha gharama za huduma za mawasiliano ambapo miongoni mwa zinazofanya vizuri sana kwenye huduma za kifedha kupitia makampuni ya simu ni Tanzania ikiwa ni moja ya nchi zinazoongoza katika bara la Afrika”, alizungumza Dkt. Ndugulile
Ameongeza kuwa, kumekuwa na mafanikio makubwa kama nchi kwa kufikisha huduma za kifedha kwa wananchi wengi nchini kupitia mitandao ya simu ambapo zaidi ya watu milioni 32 wanatumia huduma hiyo na kiasi cha zaidi ya shilingi trilioni 15 hadi trilioni 20 zinazunguka kwenye mitandao hiyo kwa mwezi.
“Tukiwa na mawasiliano ya ndani kwa nchi za SADC yatapunguza gharama za mawasiliano na kuwezesha kufanyika kwa shughuli za kiuchumi na maendeleo ikiwa ni pamoja na kuwezesha kutuma na kupokea fedha ndani ya nchi za SADC kupitia makampuni ya simu”, amesema Dkt. Ndugulile
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Waziri Kindamba amesema kuwa ndani ya miezi 12 watahakikisha umoja wa SATA unakuwa na Regional Integration hub itakayosaidia kurahisisha na kupunguza gharama za huduma za mawasiliano baina ya nchi hizo na kuahidi kuwa watakaa na mamlaka za usimamizi wa fedha kuangalia namna ya kuhamisha fedha kutoka nchi moja kwenda nyingine za umoja huo kupitia makampuni ya simu
Ameongeza kuwa, Serikali imefanya
uwekezaji mkubwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambao TTCL ndio
msimamizi wa Mkongo huo na hivi karibuni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari Dkt. Faustine Ndugulile atazindua Kituo cha Mkongo wa Taifa wa
Mawasiliano unakaounganisha nchi ya Tanzania na Msumbiji sambamba na
kukamilisha upembuzi yakinifu(feasibility study) wa kuunganisha na kupeleka
hudumza za Mkongo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...