Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mheshimiwa Dkt. Leonard Chamuriho, akizungumza na Wakurugenzi wa Wizara, Wakuu wa Vitengo,  pamoja na Viongozi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara yake (hawapo pichani), katika kikao kazi kilichofanyika jijini Dodoma. Kulia ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mheshimiwa Mwita Waitara.

Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mheshimiwa Mwita Waitara, akisisitiza jambo katika kikao kazi kilichowakutanisha Wakurugenzi wa Wizara, Wakuu wa Vitengo pamoja na Viongozi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo jijini Dodoma. Kushoto ni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mheshimiwa Dkt. Leonard Chamuriho. 

Wakurugenzi wa Wizara, Wakuu wa Vitengo pamoja na Viongozi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mheshimiwa Dkt. Leonard Chamuriho (hayupo pichani),  katika kikao kazi kilichowakutanisha viongozi hao jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Gabriel Migire (Wakwanza kushoto), akitoa maoni yake kuhusu uboreshaji wa Utendaji wa Wizara hiyo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mheshimiwa Dkt. Leonard Chamuriho, katika kikao kazi kilichofanyika jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandsi Patrick Mfugale akishauri jambo katika kikao kazi kilichowakutanisha Wakurugenzi wa Wizara, Wakuu wa Vitengo pamoja na Viongozi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi jijini Dodoma. PICHA NA WUU

************************************

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, amewataka Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara yake kuhakikisha wanaandaa taarifa kila mwezi zinazoelezea utekelezaji wa majukumu yao ili kusaidia Wizara kufahamu kwa undani utendaji wa Taasisi hizo ikiwemo mafanikio na changamoto zake.

Hayo aliyasema Waziri huyo, jijini Dodoma, katika kikao kazi cha kumtambulisha Naibu Waziri wa Wizara hiyo  Mhe. Mwita Waitara, kwa mara ya kwanza kwa viongozi wa Taasisi hizo ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza kuwa Wizara itakuwa inaandaa vikao kama hivyo  mara nne kwa mwaka ili kujadiliana kwa pamoja na kupata tathmini na  mwelekeo wa Wizara katika ufanisi wake wa utendaji kazi.

“Nimeamua leo kuitisha kikao hiki ili kumtambulisha Naibu Waziri kwa wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara yangu, pia kukumbushana kuhusu utekelezaji wa masuala mbalimbali yaliyo katika Taasisi zao”, amesema Waziri Chamuriho.

Aidha, Chamuriho amezisisitiza Taasisi hizo kushirikiana na kuwajibika ipasavyo katika miradi wanayoitekeleza kwani mingi huigusa jamii ambapo ameongeza kuwa, kufanya hivyo kutapelekea maendeleo kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe.Mwita Waitara, amewataka viongozi hao wa Taasisi kumpa ushirikiano wa kutosha na kwamba ofisi yake itakuwa wazi kwa ajili ya kupokea ushauri na maoni mbalimbali  lengo likiwa ni kusaidia kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyo chini ya Wizara hiyo ili kuleta maendeleo kwa wananchi.

“Naomba Wakuu wa Taasisi wanipe tu ushirikiano wa kutosha na niwabainishie kuwa Ofisi yangu itakuwa wazi wakati wote kwa ajili ya kupokea ushauri lengo likiwa ni kuleta tija na maendeleo kwa wananchi”, amefafanua Naibu Waziri Waitara.

Naye, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi, Arch.Edwin Nunduma,  amesema kuwa agizo hilo la Waziri la kuleta taarifa za utekelezaji Wizarani litawafanya kuwajibika zaidi kutokana na kuwa Wizara itafuatilia kwa karibu utendaji wao.

“Utaratibu huu ni mzuri, kwani hata changamoto zikitokea itakuwa ni rahisi kuzitafutia ufumbuzi mapema na kwa haraka kuliko kusubiri kuleta taarifa ya robo mwaka  kwa kila kota kama ilivyo awali”, amesema Nunduma.

Kikao hiki cha siku moja ambacho kimemkutanisha Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mheshimiwa Dkt. Leonard Chamuriho, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe.Mwita Waitara, Menejimenti ya Wizara hiyo pamoja na viongozi wakuu wa Taasisi 23 zilizo chini ya Wizara hiyo , kilikuwa na lengo la kutambuana na kukumbushana kuhusu uwajibikaji katika Taasisi zao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...