Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akitazama fomu za madai ya malimbikizo ya mishahara ya Watumishi wa Umma, mara baada ya kuitembelea Idara ya Usimamizi wa Rasilimali watu Serikalini inayoshughulika na madai hayo. Kushoto ni Katibu Mkuu-UTUMISHI Dkt. Laurean Ndumbaro akishuhudia.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na watumishi wa ofisi yake waliopo UDOM mara baada ya kuwatembelea kwa lengo la kuhimiza Uwajibikaji. Kulia kwake ni Katibu Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akisalimiana na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Bw. Elisante Mbwilo (wa kwanza kushoto) mara baada ya kuwasili katika Ofisi yake iliyopo UDOM kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu-UTUMISHI Dkt. Laurean Ndumbaro.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akielekea Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu ili kuona na kuhimiza utekelezaji wa majukumu ya Idara hiyo. Katikati ni Katibu Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro.

 

………………………………………………………………………………………..

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ameielekeza Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu ya Ofisi yake kuhakikisha inawatafutia Watumishi wa Umma na Viongozi nafasi za mafunzo ya kuongeza maarifa na utaalamu ndani na nje ya nchi ili kuwajengea uwezo kiutendaji.

Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo hayo, alipoitembelea Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu yenye jukumu la kuandaa sera, miongozo na mifumo ya Usimamizi wa maendeleo ya rasilimaliwatu katika Taasisi za Umma ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mhe. Mchengerwa amesema, Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuwapatia mafunzo ya kutosha Watumishi wa Umma na Viongozi katika Taasisi za Umma ikiwa ni pamoja na Wakuu wa Mikoa na Wilaya ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Ili kuunga mkono azma hiyo ya Mhe. Rais, amesisitiza kuwa Ofisi yake kupitia Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu itahakikisha Watumishi wa Umma nchini wanapata mafunzo yatakayowajengea morali na hali ya kutoa huduma bora kwa wananchi. 

Waziri Mchengerwa ameitaka Idara hiyo kuongeza jitihada za kutafuta Taasisi za Kitaifa na Kimataifa ambazo ziko tayari kutoa ufadhili wa mafunzo kwa Watumishi na Viongozi wa Taasisi za Umma na kuwasilisha fursa zilizopatikana kwa Katibu Mkuu-UTUMISHI ili aone namna bora ya kuzitoa kwa walengwa kwa kuzingatia mahitaji ya Utumishi wa Umma na vipaumbele vya Serikali.

Aidha, amewataka Watumishi na Viongozi watakaopata fursa ya mafunzo kuwajengea uwezo Watumishi na Viongozi wengine ambao hawajabahatika kupata fursa ya mafunzo ili nao waweze kuboresha utendaji kazi wao.

Akipokea maelekezo ya Mhe. Mchengerwa, Kaimu Mkuu wa Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu Bw. Elisante Mbwilo amesema Idara yake itaendelea kutafuta fursa za mafunzo kwa wadau wa ndani na nje ya nchi ili Watumishi na Viongozi wanufaike na fursa zitakazopatikana kwa lengo la kuboresha utendaji kazi.

Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inatekeleza jukumu la kuwajengea uwezo Watumishi wa Umma kwa kuzingatia Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 Kifungu G.1 (Kifungu kidogo cha 7, 9, 10 &11), Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2008 Kifungu cha 4.8 na Sera ya Mafunzo katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2013.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...