Na Mwandishi Maalum, Songwe
MAHABUSU na Wafungwa waliopo katika Gereza la Mbozi Mkoani Songwe, wameiomba Serikali
kuangalia uwezekano wa kutunga sheria ya ukomo wa upelelezi ili pamoja
na mambo mengine kuhakikisha utoaji wa hakijinai unakwenda kwa wakati lakini pia kupunguza na kuondoa
msongamano wa mahabusu na wafungwa
katika magereza mbalimbali nchini.
Wametoa ombi hilo leo
( Jumanne) mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Profesa Sifuni
Mchome aliyeambatana na Katibu Mkuu
anayeshughulikia masuala ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. John Jingu walipotembelea
Gereza hilo kujifunza, kutambua kero na
changamoto wanazokabiliana nazo watendaji wa Magereza, Wafungwa na Mahabusu.
Katika risala yako iliyosomwa na mmoja wa mahabusu hao Jumanne Athuman Ali, wamesema, kumekuwapo na ucheleweshaji mkubwa
wa utoaji wa haki kwa watuhumiwa kutokana
kuchelewa kwa upelelezi wa kesi ambao
unachukua zaidi ya miaka mitano na kuendelea kwa baadhi
ya kesi hasa zile za mauaji na uhujumu uchumi.
“Mheshimiwa
Makatibu Wakuu, sisi ( mahabusu
na wafungwa) tumefurahishwa sana na ujio wenu, na wewe Katibu Mkuu wa Sheria
ndiyo mwenyewe, tunakuomba basi, uangalie uwezekano wa kutungwa kwa sheria ya
ukomo wa upelelezi ili haki iweze kutendeka mapema, na mtuhumiwa
ajue hatima yake kama anafungwa
au anaachiwa huru wengi wetu humu tumeshakaa muda mrefu inauma na inasikitisha
sana, na sisi tuna familia zetu, tunashughuli zetu, tusaidie katika hili”.
Pamoja na kuomba
kutungwa kwa sheria ya ukomo wa kipindi cha
upelelezi, mahabusu na wafungwa
hao pia wamewaeleza Makatibu Wakuu hao,
kwamba, ucheleweshaji wa upelelezi wa kesi umepelekea kuwa na mlundikano mkubwa wa mahabusu na
wafungwa katika gereza hilo ambalo uwezo wake ni kuhifadhi wafungwa 100 lakini
hadi wakati huo kulikuwa na wafungwa na mahabusu wapatao wapatao 448.
“Waheshimiwa, hatuna shida ya
chakula wala matibabu katika Gereza hili, shida yetu kubwa ni msongamano
tunalazimika kulala watu 160 katika chumba kimoja chumba kile
kidogo Mhe. Watu 160 fikiria tunalalaje mle , na hali hii inachangiwa na ucheleweshwaji wa upelelezi wa kesi zetu
tunaomba sana kwa ujio wenu mtusaidie kuitatua changamoto hii.”
Pamoja na changamoto ya
mlundikano, changamoto nyigine walizozieleza ni pamoja na ubambikizwaji wa kesi ambao wameeleza
hufanywa zaidi na Polisi,masharti magumu
ya dhamana, na uhaba mkubwa wa maji katika
Gereza hilo jambo ambalo wamesema ni hatari kwa afya zao.
Wakielezea zaidi juu
ya changamoto kubwa
ya ukosefu wa maji ,
hawakusita kumshukuru na kutoa
shukrani za pekee kwa Mkuu wa
Gereza hilo ACP Bosco
Lupala kwa namna ambavyo amekuwa
akilishughulikia tatizo hilo kwa kadri ya uwezo wake hata hivyo wakasema Mkuu huyo wa Gereza naye
amefikia ukomo wake wa kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo.
“Mkuu wetu wa Gereza
hili kwa kweli anajitahidi sana kutusaidia katika kukabiliana na uhaba mkubwa
wa maji na kwa kweli tunampongeza sana sana lakini na yeye anafikia mahali ana
kwama. Tunaomba basi kupitia ujio wenu muangalie
namna ya kutusaidia katika suala
hili la maji ili nasi tupate angalau maji ya kuoga hata kama ni kwa kugawana kidogo kidogo” wakasema wafungwa
na mahabusu hao .
Awali Mkuu wa Gereza
hilo ACP Bosco Lupala katika taarifa
yake fupi kwa Makatibu Wakuu hao alielezea pamoja na mambo mengine changamoto
hiyo ya upatikanaji wa maji hasa wakati wa kiangazi.
Katibu Mkuu Profesa Sifuni Mchome pamoja na kusikiliza na
kupokea risala ya mahabusu na wafungwa hao, pia alitoa fursa kwa baadhi ya
wafungwa na mahabusu waliokuwa na shida kubwa kujieleza mbale yake.
Akijibu na kutolea ufafanuzi baadhi ya changamoto
zilizowasilishwa na mahabusu hao na
wafungwa wa Gereza la Mbozi ambalo pia linahifadhi mahusubu kutoka Mahakama za
Ileje na Momba, Katibu Mkuu Mchome amesema, Serikali imekuwa ikifanya na
inaendelea kufanya marekebisho ya sheria
mbalimbali ili kupitia marekebisho hayo
hali ya utoaji haki jinai iweze kutekelezwa kwa tija inayotakiwa.
Akawaeleza mahabusu na wafungwa hao kwamba, Serikali inafanya
kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba, haki
za watuhumiwa zinalindwa kwa kile alichosema ingawa ni mahabusu au
wafungwa bado wao ni sehemu ya Jamii.
Kuhusu changamoto ya
kubambikiwa kesi, Katibu Mkuu amesema
Serikali inaitambua changamoto
hiyo na hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa ili kuidhibiti hali hiyo
ambayo alisema haileti taswira nzuri
Kuhusu shida kubwa ya
maji katika Gereza hilo, Profesa Mchome ameahidi kulishughulikia baada ya kuelezwa pia na Mkuu wa Gereza hilo kwamba, ufatifi uliofanywa unaonyesha kwamba
eneo lilipo gereza hilo kuna maji ya kutosha kuweza kuchimba kisima.
Pamoja na kuzungumza na mahabusu na wafungwa wanaume,
Makatibu hao pia waliwatembelea wafungwa wanawake ambao wapo katika gereza hilo na kusikiliza shida
zao.
Wafungwa na mahabusu
wanawake wapatao 18 huku wawili kati yao wakiwa na watoto wadogo walipopewa nafasi ya kuelezea shida zao,
baadhi yao walisema wapo pale kwa kesi za kumbambikiwa na kuomba wasaidiwe kwa kuwa wameshakaa muda
mrefu gerezani humu na wamewaacha watoto wao ambao wengine ni wadogo na
wanahitaji malezi ya mama zao.
Mfungwa mwingine yeye
alitaka kufahamu kwa nini nakala ya hukumu yake hajaipata mpaka sasa.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba
na Sheria amemtaka Mwendesha Mashtaka
Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoani Songwe kwa kushirikiana na wadau
wengine kuangalia namna watakavyoweza kushughulikia kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu
baadhi ya mashauri ambayo yanaweza kumalizwa bila kufika Mahakamani.
Aidha ametaka kufuatilia na kwa mujibu wa sheria kesi zote
ambazo watuhumiwa wake wapo mahabusu na kuangalia kama kunauwezekano hasa kwa
makosa yale madogo madogo kama kupigana yanaweza kumalizwa kwa njia ya adhabu
mbadala.
Katibu Mkuu Mchome, amesema katika mambo ambayo anayasisitiza
anapokutana na wadau wanaohusika na utoaji wa haki ni kuangalia namna bora zaidi ya kumaliza
baadhi ya mashauri nje ya vyombo vya sheria kwa njia ya majadiliano na kwa kutoa adhabu mbadala ili wale wanaotakiwa
kwenda Magerezani basi wawe ni kweli wale wanaostahili kwenda huko.
Akiwa Mkoani Songwe
katika siku ya pili ya Ziara ya Kikazi ya Kawaida ya Makatibu Wakuu hao, wamepata fursa ya kuitembelea Mahakama ya
Wilaya ya Momba ambayo inatekeleza
shughuli zake katika majengo ya Mahakama ya Mwanzo. Ambapo alipata fursa ya kubadilishana mawazo na
watendaji wa Mahakama hiyo.
Vile vile Katibu Mkuu
Mchome alipata fursa ya kutembelea mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi . Ujenzi wa Mahakama
hiyo unaogharimu shilingi milioni
768,270,116 unatarajiwa kukamilika mwezi
Agosti 2021.
Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wapo katika ziara ya pamoja ya kuitembelea Mikoa Mipya na ile ya Pembezoni ambayo ni Songwe, Rukwa na Katavi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...