Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto
anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Mwanaidi Ali Khamis ameziagiza
Taasisi na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini kujitangaza kupitia vyombo
mbalimbali vya
habari ili kuwawezesha wananchi kunufaika na Huduma za vyuo hivyo.
Naibu Waziri Mwanaidi ametoa agizo hilo Jijini
Arusha mara baada ya kufanya ziara katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru
kwa lengo la kukagua Maendeleo ya miradi ya Ujenzi chuoni hapo.
Amesema pamoja na ongezeko la udahiri wa wanachuo,
Taasisi inatakiwa kujitangaza na kusambaza taarifa zaidi kuhusu huduma na
mafunzo yake kwa Jamii ili kuwezesha wanufaika wengi kupata ujuzi.
"Naomba niseme kwamba mnafanya kazi kubwa na nzuri
kwa Jamii ya Watanzania, lakini bado Jamii inahitaji kupata taarifa zaidi na
kwa kufanya hivyo, wananchi wataelimika, wataweza kujiajiri na kuajiri wengine" alisema Naibu Waziri Mwanaidi.
Akizungumza kuhusu ujenzi wa mabweni na kumbi za
mihadhara katika Taasisi hiyo, Mwanaidi amesema Serikali ameanza kutenga fedha
kwa ajili hiyo na hivyo ni muhimu kusimamia matumizi yake.
"Shilingi Bilioni 2.7 zinazotarajiwa
kutumika kwa ajili ya Ujenzi wa ni fedha nyingi hivyo ni muhimu kuzitumia kadri
ilivyokusudiwa na mimi nitarudinkuhakikisha zimetumika kama ilivyolengwa" aliongeza.
Amefafanua kuwa hadi sasa tayari Sh Bilioni moja
zimetolewa na Serikali kwa ajili ya Mabweni ya wanafunzi wa Kike na Ukumbi
wa mihadhara.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry
Muro amesema Taasisi hiyo ni muhimu sana kwani inatoa fursa kwa vijana kupata elimu kutoka maeneo
mbalimbali nchini na kuwasaidia vijana kuajiriwa, kujiajiri na kuajiri wengine.
Aidha ameishukuru Serikali kwa hatua ya kutoa shilingi
Bilioni moja za Ujenzi na kuahidi kwamba Wilaya yake itashirikiana na Taasisi
kutimiza azima ya Serikali katika kuona fedha za miradi zinafanya kazi iliyokusudiwa.
"Ni muhimu kujipanga sisi wenyewe na
kuhakikisha vifaa vya ujenzi vinapatikana kwa bei za jumla kuwatumia wataalam
wa ndani katika utaratibu wa ujenzi" alisema.
Awali akitoa taarifa kwa Naibu Waziri, Mkuu wa
Taasisi hiyo, Dkt. Bakari George amesema Taasisi hiyo inaongeza udahiri wa
Wanafunzi Kutoka wanafunzi 1167 hadi wanafunzi 2,608 huku mpango ukiwa ni
udahiri wa wanafunzi 5000.
Ameongeza kuwa uwepo wa Kituo cha ubunifu cha
kidigitali kimesaidia kulea na kuatamia
mawazo ubunifu ili wahitimu na watu wa maeneo jirani waweza kutumia fursa ya
kujiajiri na kuwaajiri wengine.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto
anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Mwanaidi Ali Khamis akipata maelezo ya
Miradi ya ujenzi wa Mabweni ya Wasichana na Kumbi za Mihadhara kutoka kwa Naibu
Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Utawala na Fedha Janeth Zemba
wakati alipotembelea Taasisi hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...