Na Mwandishi wetu Mihambwe

Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu amekemea vikali tabia ya hujuma ya upigaji na uchezeaji wa miradi ya ujenzi ya kimaendeleo.

Hayo yamejitokeza kwenye ziara aliyoifanya Gavana Shilatu ya kutembelea mradi wa ujenzi Zahanati ya Miuta ambao haujanza kutumika lakini "gypsum boards" zimeanza kuanguka zenyewe huku nyaya za umeme zikitandazwa pasipo kuwekwa kwenye bomba.

"Mwenyekiti ujenzi huu una mashaka, unaona mwenyewe jengo halijaanza kutumika tayari "gypsum boards" zimeshaanza kuanguka, nyaya hazijapita kwenye bomba na nyie mpo mkishuhudia haya ambapo kimsingi ni mradi wenu. Hili halikubaliki, lazima haya madudu yarekebishwe." Alisema Gavana Shilatu.

Gavana Shilatu aliamua kuwatuliza Wananchi waliokuwa na hasira kwa  kusisitiza upigaji hautavumilika ndani ya Tarafa ya Mihambwe na atazidi kuanika madudu endapo wanaopewa dhamana hawatajirekebisha na kusisitiza ujenzi urudiwe.

"Haiwezekani Watu walioharibu kule ndio hao hao wanaharibu na huku, sitovumilia madudu haya  ambayo hata Wananchi hawayapendi, ni shetani pekee anaweza kuvumilia ubadhirifu huu. Hivyo marekebisho ya haraka yafanyike na Wananchi mtulie kila kitu Serikali itasimamia ipasavyo na tuendelee kushirikiana ." Alisisitiza Gavana Shilatu.

Mwenyekiti Kijiji cha Miuta Ndugu Hamad Asali  aliwaeleza Wananchi kuwa hawakubaliani na madudu hayo na watasimamia ujenzi huo urudiwe ipasavyo ndio wakubali kuupokea.

"Mradi huu unaendelea kujengwa na pale penye mapungufu tunaendelea kuwakaba Mafundi warekebishe ndipo tuupokee." alisisitiza Mwenyekiti wa Kijiji Miuta Ndugu Asali.

Akizungumza kwa niaba ya Wananchi Ndugu Muhibu Ally Lisakasi alifurahishwa na ujio wa Afisa Tarafa Mihambwe ambapo amepata fursa kueleza kero za mradi huo na kutamani uishe kwa haraka na ufanisi ili uanze kutumika.

"Nimefurahi sana kutembelea walau na kiongozi wa ngazi ya juu kwani hili la Zahanati ni kero kwetu, tunataka ujenzi mzuri ukamilike na jengo lianze kutumika. Afisa umetufurahisha sana kututembelea leo kwani tunapata fursa kueleza shida zetu na utatuzi tunaupata, Mwenyezi Mungu azidi kukubariki." Alisema Ndugu Lisakasi.

Katika ziara hiyo Gavana Shilatu aliambatana na Mwenyekiti Kijiji, Mtendaji Kijiji, kamati ya ujenzi, fundi pamoja na Wananchi waliojitokeza kueleza kero zao mara baada ya kumuona Afisa Tarafa Mihambwe.




 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...