Serikali
ya Tanzania, Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) waungana na
Mabalozi wa nchi za Nordic (Sweden, Denmark, Finland na Norway)
kwenye kongamano la siku moja kujadili mwelekeo wa Tanzania katika
mageuzi ya kidigitali katika zama za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda
(Fourth Industrial Revolution).
Kongamano
hilo lililofanyika katika Hoteli ya Ramada, jijini Dar es Salaam
lilihudhuriwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt.
Faustine Ndugulile, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia
(Uwekezaji) Profesa Godius Kahyarara, Dr. Jim Yonazi Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari likiwa na kauli mbiu
“Tanzania’s Path towards Prosperity: Balancing the State, Market and
Community” likishirikisha wadau kutoka serikalini, taasisi za huduma,
viongozi wa dini, sekta binafsi, wafanyabiashara na wadau wa uchumi.
Akichangia
katika kongamano hilo, Mheshimiwa Dkt. Ndugulile alisema, Serikali ipo
kwenye mkakati wa kuhakikisha inakwenda sambamba na mabadiliko ya
kidigitali duniani.
Aliongeza
kwamba kwa sasa Serikali kufanya maboresho ya mifumo ya utoaji huduma
za kiserikali kwa jamii kwa kuihusisha jamii yenyewe kwenye kujiletea
maendeleo ya kiuchumi kwa kutumia mitandao katika kufanikisha shughuli
zao za kiuchumi na kijamii katika nyakati hizi za mapinduzi ya
kidigitali.
Kwa
upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia
uwekezaji Profesa Godius Kahyarara amesema kuwa serikali inatumia kwa
kiasi kikubwa teknolojia ya TEHAMA (ICT) katika kuhamasisha uwekezaji
nchini.
“TEHAMA
imekuwa msaidizi mkubwa wa kuongeza uwekezaji nchini ambapo tumekuwa
tukitumia teknolojia hii kuweza kutangaza maeneo yetu ya uwekezaji na
hivyo tumeweza kupata wawekezaji wengi kupitia ICT,” alisema.
Akitoa
neno la utangulizi katika Kongamano hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF
Dkt. Tausi Kida alisema, tangu kuanzishwa kwake 1993 Taasisi yake imetoa
mchango mkubwa katika uandaaji wa sera na mikakati mbalimbali ya
maendeleo nchini Tanzania.
Sambamba
na hilo, Mkurugenzi wa ESRF alifafanua pia kwamba Taasisi yake imekuwa
ikiendesha tafiti na kuendeleza programu mbalimbali zenye kuchochea
matumizi ya kidigitali katika mchakato mzima wa kuwaleta wananchi
maendeleo. Baadhi ya shughuli hizo ni pamoja na kutengeneza mfumo wa
kuwasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi kupata taarifa na shughuli za
ugani kwa kupitia simu za mkononi.
Pia
ilianzisha Maktaba Mtandao (TzOnline) ambayo umesheheni machapisho
mbalimbali yahusuyo maendeleo katika Tanzania. Mtandao huu unasaidia
sana watumiaji kupata machapisho na taarifa mbalimbali kirahisi kwa
kupitia mtandao bila kulazimika kufika Maktaba
Naye
Mheshimiwa Balozi wa Sweden Anders Sjöberg kwa niaba ya mabalozi
wengine wa nchi za Nordic aliwakaribisha washiriki wote ambao
waliohudhuria katika kongamano hili ambalo ni sehemu ya wiki ya Nordic
nchini Tanzania.
“Shukrani
za pekee ziwaendee Dkt. Tausi Kida Mkurugenzi Mtendaji ESRF na ESRF kwa
ujumla kwa ushirikiano wetu wa pamoja katika kuandaa kongamano hili”
alisema Balozi wa Sweden.
“Kama
Mabalozi wa Nordic wakati mwingine tunakumbushwa kwamba sisi pamoja na
Tanzania tuna matarajio na malengo sawa. Wote tunataka jamii zenye
usawa kiuchumi, kijamii na mazingira endelevu. Na sisi kama Mabalozi wa
Nordic tunafurahi kuona Tanzania ina nia ya kufanya madadiliko katika
maeneo haya,” Mheshimiwa Balozi Anders Sjöberg aliongeza.
Wadau
mbalimbali walioshiriki katika kongamano hili wameshauri kuwa Tanzania
lazima iende sambamba na mabadiliko ya Mapinduzi ya Nne ya Viwanda
Duniani ambapo matumizi ya Teknolojia hususani mitandao lazima yapewe
kipaumbele katika kukuza uchumi wa nchi.
Kongamano hilo hufanyika kila mwaka ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Nordic kusherehekea uhusiano wa maendeleo ya muda mrefu kati ya Tanzania na nchi za Nordic. Maadhimisho hayo huambana na shughuli mbalimbali kwa wiki zima.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...