Na Judith Mhina-MAELEZO

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Kichezo  Innocent Bashungwa amewaomba Wahisani kuendelea kusaidia Tasnia ya Habari hapa nchini.

Ameyasema hayo leo wakati akikabidhi seti 16 za redio zenye thamani ya Euro 172,943.76 sawa  na Shilingi za Kitanzania Milioni 400 kwa Shirika lisilo la kiserikali la Mtandao wa redio za kijamii (TADIO) lenye jumla ya redio za kijamii zaidi ya 35 nchi nzima.

“Tunapongeza na kulishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni-UNESCO kwa kuona umuhimu wa kuhakikisha habari zinawafikia wananchi walio wengi hususani kwa makundi yaliyosahaulika wakiwepo Wanawake na Watoto wa Vijijini, pia tunathamini mchango wenu na tunaomba ushirikiano huu uendelee ili kuhakikisha tasnia ya habari inakua nchi nzima.”

Aidha Waziri Bashungwa amekumbusha mambo muhimu ya kujadiliwa katika mijadala ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari kimataifa, na kueleza kuwa  kuna haja ya kuhakikisha uhuru huo ujikite katika mambo makuu matano ambayo ni uhuru wa vyombo vya habari vinavyofaa, kuendeleza nguvu kazi, mazingira mazuri ya sheria na sera ikiwa ni pamoja na  ubora wa kazi, ulinzi na usalama wa waandishi na  pamoja na uelewa wa matumizi ya kidigitali.

Kwa upande wake Mwakilishi wa UNESCO Nchini Tanzania Bw. Tisso De Santos amesema ili kuhakikisha malengo 16 ya agenda za Mkutano wa Umoja wa Mataifa-UN utakaofanyika Septemba mwaka huu katika makao makuu ya Umoja huo Jijini New York Marekani kwa ajili ya kuamua rasmi kuhusu ajenda ya mwaka 2030 yanafanikiwa Tanzania iwe miongoni mwa nchi zitakazotekeleza malengo hayo ili kufikia lengo la Dunia.

Aidha amesema kuwa lipo jukumu kubwa kwa Tanzania kujadili ajenda hizo za kimataifa ambazo zitakuwa katika kipindi cha mpito katika kuelekea Tanzania yenye mageuzi na maendeleo makubwa ikiwepo Tasnia ya Habari.

Pia Balozi wa Sweden Nchini Tanzania Anders Sjoberg amesema sekta ya habari ni muhimili wanne hapa nchini Tanzania ikitanguliwa na Serikali, Bunge na Mahakama, huku tasnia hiyo ikifanya kazi ya kutoa taarifa kwenye sekta zote nchini katika kufuatilia mwenendo wa Serikali na utekelezaji wake na maoni ya wananchi kuhusu utekelezaji huo.

Amesema kulingana na kaulimbiu ya mwaka huu ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari kimataifa ambayo ni ''Habari kwa manufaa ya Umma' imekuja kwa wakati sahihi ambapo nchi zote duniani zinatakiwa kuwa nchi za kidemokrasia, kuwa na uhuru wa habari kama ilivyo kwa nchi ya Sweden iliyopata uhuru huo mwaka 1776.

“Kwa kuwa Dunia inabadilika kiteknolojia kwa kasi sana kuna umuhimu mkubwa kuwa na nchi zenye demokrasia” amesema.

Aidha amebainisha kuwa nchi ya Sweden ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza tasnia ya habari katika masuala yote yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo na kutolea maamuzi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...