Na Mathew Kwembe, Mtwara

Timu ya soka ya wavulana kutoka mkoa wa Dar es salaam imeyaanza kwa kishindo michuano ya UMISSETA mwaka huu baada ya kuinyuka timu ya soka kutoka mkoa wa Kigoma kwa magoli 2-0 katika mchezo mkali na wa kusisimua uliofanyika leo katika uwanja wa Chuo cha Ualimu Mtwara.

Magoli ya washindi katika mchezo huo yamefungwa na washambuliaji machachari wa Dar es salaam Juma Ahmad na Ibrahim Hussein.

Nyota wa mchezo huo alikuwa ni kiungo wa Dar es salaam Ahmad Said ambaye mara kwa mara amekuwa akiisumbua ngome ya timu ya kigoma iliyokuwa ikiongozwa na beki wao mahili Ally Kassim.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo kocha wa timu ya Dar es salaam Abel Mtweve amesema vijana wake wamecheza vizuri kutokana na maandalizi waliyoyafanya kabla ya kuanza mashindano hayo.

Mtweve ambaye pia ni Mwalimu kutoka shule ya sekondari ya Kibasila ya jijini Dar es salaam amejigamba kulichukua kombe hilo kama walivyofanya wadogo zao wa UMITASHUMTA.

Kwa upande wake kocha wa timu ya soka ya mkoa wa Kigoma Waziri Mbugi amesema vijana walijitahidi katika mchezo huo ili kurudisha magoli lakini walizidiwa kimbinu na Dar es saalam kwani wapinzani wake hao waliweka mtu mmoja kati mwenye spidi kubwa ya kukimbia na mpira na hivyo kushindwa kurejesha magoli hayo.

Mbugi ambaye anafundisha shule ya sekondari Buhanda huko Kigoma ameahidi kufanya vizuri katika michezo yao inayofuata kwani mkoa wa Kigoma una vipaji vingi vya soka.

Katika matokeo mengine ya mechi za ufunguzi wa michuano hiyo mabingwa watetezi wa soka kutoka mkoa wa Ruvuma wamelazimishwa sare na Pwani ya magoli 1-1, Morogoro imefungwa na Katavi magoli 2-0, Kilimanjaro imeichapa Mbeya magoli 2-0,

Matokeo mengine kwa soka wavulana yanaonyesha Rukwa na Mwanza wametoka sare ya bila kufungana, Singida imefungwa na Manyara 1-0 na Geita imefungwa na Kagera goli 1-0, Lindi imechapwa na Simiyu magoli 1-2, Pemba na Mtwara 0-0 na Unguja na Tanga 1-1

Katika mchezo wa mpira wa Netiboli, Dar imeichapa Mbeya 22-11, Mwanza imeibugiza Lindi magoli 48-2, Morogoro imefungwa na Geita 42-18 na Mara imeichakaza Tanga 21-5.

Katika mchezo wa mpira wa wavu Lindi imefungwa na Tabora kwa seti 1-3, Simiyu nayo imechapwa na Mbeya kwa seti 0-3, Tanga imeifunga Singida seti 3-0 na Kilimanjaro imeitoa jasho Songwe kwa kuifunga seti 3-0.

Kwa upande wa matokeo ya mpira wa kikapu kwa wavulana Morogoro imeifunga Pemba 84-61, Unguja imepata vikapu 48 dhidi ya 30 vya Tanga,

Matokeo mengine ya mechi za ufunguzi wa UMISSETA kwa mpira wa wavu wavulana Tabora imeifunga Tanga seti 3- 0, Mbeya imeifunga Rukwa 3-0, Mara imeichapa Manyara seti 3-0 na mchezo kati ya Dar es salaam na Iringa umeahirishwa kutokana na giza.

Kwa upande wa mpira wa mikono matokeo Morogoro 11 Dodoma 3, Mara 10 Unguja 30 na kwa timu za wasichana mpira mikono Simiyu 5 Shinyanga 9, Tanga 40 Iringa 8, Songwe 39 Kigoma 3.

Mchezaji wa mpira wa wavu kutoka mkoa wa Dar es salaam Said Omary akijaribu kupiga spike dhidi ya timu ya mkoa wa Iringa. Mchezo huop uliahirishwa kutokana na giza kutanda uwanjani hapo. Hadi mchezo unaahirishwa Dar es salaam ilikuwa inaongoza kwa seti 2-1
Mchezaji wa mpira wa kikapu wa timu ya mkoa wa Tanga Bakari Juma akijiandaa kufunga huku wachezaji wa Unguja wakiongozwa na mchezaji Ahmed Omari (jezi namba 5 ya bluu) katika mchezo mkali ambapo Unguja waliifunga Tanga vikapu 48-30
Nahodha wa timu ya soka ya mkoa wa Dar es salaam Ahmad Said (jezi nyeupe) akichungwa kwa karibu na beki mahiri wa kigoma (jezi nyekundu) Ally Kassim wakati timu zao zilipopambana leo katika mojawapo ya mechi za ufunguzi wa michuano ya UMISSETA iliyofanyika katika Uwanja wa Chuo cha Ualimu Mtwara.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...